Huu msemo ulianza kama utani kwamba kama una nafasi ya ziada katika kipato, basi unapohitaji kufurahisha moyo wako, kula kitu kizuri ambacho unakipenda na haushurutishwi na mtu na hauna shida ya kukipata. Hii ndiyo maana halisi ya ‘kula kitu roho inapenda.’

Leo nimeukumbuka huu usemi ambao wengi wetu tulikuwa tunasikia ukizungumzwa kutoka kinywa cha mtu katika maeneo ya starehe wakati huo wa kucheza na madili ya mjini na kisha unachukua fedha katika masandarusi. Historia ni nzuri sana japo inakera kuikumbuka katika kipindi hiki.

Waraka wangu wa leo umejikita katika jambo moja dogo sana, la baadhi ya wanasiasa kurudi au kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu iliyopo madarakani. Ni jambo jema sana ingawa kwa upande wa pili kuna kitu ambacho kimejificha ndani ya mioyo ya watu na kinawakera kwelikweli.

Mtaji wa chama chochote ni wanachama wake, si majengo wala fedha. Wanachama ndio wanaochagua viongozi walioko madarakani kwa wakati huo. Vyama vingi vinavyoshiriki katika uchaguzi vinategemea wingi wa wanachama wao katika ushindi wa eneo lao. Tunaona jinsi ambavyo wapiga kura wakiwanadi na kuwasifu viongozi wao kabla na baada ya uchaguzi.

Katika kipindi cha miaka minne kuelekea mitano sasa, kulikuwa na ushindani mkubwa katika majimbo mengi na kata nyingi nchini. Vyama mbalimbali vilishiriki katika uchaguzi na kuwasimika viongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano. Waliamini kuwa viongozi wao watalisukuma gurudumu la maendeleo katika kipindi hicho mpaka uchaguzi mwingine unapofika.

Mambo mengi yamekuwa tofauti kidogo hasa katika vyama vya siasa ambavyo vingi havijashika dola. Tumeshuhudia viongozi kadhaa, hasa wa upinzani, wakiachia ngazi katikati ya safari bila makubaliano na waliowachagua kwa kisingizio cha kukubaliana na uongozi uliopo madarakani.

Naweza kukubaliana nao kwa hoja ya kula kitu roho inapenda lakini siwezi kukubaliana nao kama hawajwashirikisha waliowapigia kura kuwataka kurudi katika chama kilichoshika dola kwa maana ya kuunga mkono juhudi ambazo zinafanywa na serikali ambayo alipaswa kuikosoa na kuisimamia katika maendeleo.

Mimi si muumini kabisa wa siasa ya kupinga kila kitu, hasa jambo ambalo ni kwa ajili ya maendeleo yetu. Mimi si muumini wa kiongozi anayetaka madaraka katika vyama tofauti kwa muda mmoja wa uongozi na si muumini wa kuamini kwamba uongozi ni kazi ya kufanywa na mtu mmoja tu bila wengine kupewa nafasi ya kujaribu ili kuona karama zao katika kutuongoza.

Najua kwamba wapo ambao wamehama na uchaguzi ulipofanyika wakashinda tena kupitia chama kingine. Najua kwamba kura zinatosha kwa mtu wanayempenda. Hoja yangu ni kwamba iwapo unaona umechoshwa na tabia ya viongozi wako wa ngazi za juu, basi wataarifu waliokupigia kura kwa njia ya mkutano na toa mwongozo kwamba twende ambako roho inapenda, si kuwaacha wakiwa hawajui hatima yao.

Inawezekana kabisa mabadiliko ya kiuongozi yakakukosha hata wewe ambaye ulikuwa chama kingine, lakini haitoshi kukufanya uwakimbie waliokuunga mkono katika uchaguzi. Tumia muda huo kwanza kuwaeleza wapiga kura wako dhamira na lengo la kuondoka nao kwenda ambako kitu roho inapenda.

Nina umri wa kutosha ulioniwezesha kuona mambo mengi katika maisha yangu. Nawajua wenye tamaa ya maisha ya utawala na wenye nia njema ya kuwaona wengine wakiongoza. Nchi yetu imepata neema hii ya kukabidhiana vijiti, ni dhahiri kuwa tumewaona ambao baadhi yao wakiwa hawataki kubadilishana vijiti mpaka wanaanguka katika mstari wa mashindano.

Sasa tumemaliza ngwe ya kwanza na watu wameunga mkono juhudi za serikali katika awamu hii inayokwisha. Tukubaliane ukweli kwamba iwapo mliounga mkono juhudi msipochaguliwa na wananchi tena kwa awamu nyingine, basi msihame vyama, mbaki katika chama mlichohamia kwa kuwa chama hicho bado kimeshika dola na kinaendelea  na maendeleo yake. 

Iwapo mtaanza kutoa visingizio tutajua kwamba nyinyi ni wagombea masilahi ya uongozi na si wapenda maendeleo, bali ni wanafiki, hamkuja kwenye chama hicho ili muwe wanachama bali mlikwenda ili mkapate vyeo.

Najua hii ni ngumu kumeza, lakini pia najua kila mtu anapenda ile kitu roho inataka. Basi tumerudi kwa kuwa roho inataka na tutameza kwa kuwa ni dawa ili tupone, huko ni kazi tu siasa peleka kwingine.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.