Kila kukicha siku hizi ni mpango madhubuti wa kodi mpya. Sasa nasikia inataka kuibuka kodi ya simu, yaani tuwe tunalipia kila mwezi Sh 1,000. Kwa kweli tutakoma, maana hiyo sayansi ya mawasiliano mlivyoileta kwa kasi ilitufanya tujisahau mambo mengi. Kumbe ulikuwa ni mtego wa kutuingiza katika tatizo hili.
Tulisahau kuandika barua, tukazoea kutuma meseji hata kama ni mkoani na faida yake tuliona kwamba ni papo kwa hapo, tofauti na barua ambayo ilikuwa ikichukua muda mrefu kupata majibu.
Nakumbuka wakati fulani miaka kama 20 nilikuwa Uyole, nafanya biashara ya viazi kuvileta Dar es Salaam, nikaandika barua kwa dalali wangu kujua bei iliyoko sokoni, dalali alinijibu kuwa nipeleke viazi haraka kwa kuwa soko lilikuwa zuri na bei ilipanda mara kumi kidogo.
Nilipofika mjini na gari la kukodi nilikutana na kizaazaa kwani bei ilikuwa imeshuka mara hamsini ya bei ya kawaida, nilijuta kuzaliwa. Kwanza nilikuwa nafikiria jinsi ya kumtoroka mwenye gari na pili nilikuwa nafikiria kuvikimbia viazi ambavyo nilivinunua kwa mtaji wangu mwenyewe. Hii ilitokana na mawasiliano duni ya wakati huo ambao haukuwa wa kidotcom kama wa leo.
Nimeyapenda mawasiliano yalivyo ya kisayansi zaidi lakini nataka kuyachukia kama yatakuwa ghali kuyatumia kwa nia ya kurahisisha maisha na mawasiliano yenyewe. Sasa tunataka wakulima wanaotegemea mauzo ya mara moja kwa mwaka waweze kulipa kodi hiyo ya mawasiliano baada ya kuingia kwa nguvu na kuona urahisi wake. Lakini pia mkulima huyu ndiye anayepangiwa bei ya mazao yake na bado halipwi kwa wakati stahiki.
Leo nimeamua kuchukua mfano mmoja tu wa kodi mpya ya simu ambayo iko mbioni kuanza kutumika kwa mujibu wa mawazo ya waheshimiwa wetu; wawakilishi katika jengo la kutunga sheria. Sina hakika katika siku zijazo itakuwaje katika kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kuiendesha serikali yetu.
Wasiwasi wangu ni kuwa kama tumeweza kufikiria kodi hii kirahisi hivyo, sitaona ajabu nitakapoambiwa juu ya kodi ya baadhi ya barabara, kwamba hutaruhusiwa kupita kwa miguu ama gari barabara fulani bila kulipia. Nahisi tutatakiwa kulipia kodi ya makaburi ya ndugu zetu kwa kuwa wamelazwa katika eneo la nchi hii, tutatakiwa kulipia kodi za harusi, unyago na kadhalika ili kukwepa hoja ya kila wakati bajeti kutegemea vileo.
Katika moja ya barua zangu, nilipata kuhoji kodi ya baiskeli imeishia wapi? Cha ajabu katika Bunge la Bajeti la mwaka huu mmeamua kuondoa kabisa hata kodi ya bodaboda na matoyo. Sielewi ni kwa kigezo gani ama cha kuongeza ajira, au kupunguza na kukatisha maisha ya vijana ambao ni taifa la kesho na wapenda mapinduzi.
Kwa mtazamo wangu wa kizamani, nilifikiri ni vyema tukaangalia kwa makini mapato ya uhakika na yanayoweza kuimarisha pato la taifa na kuweza kuiendesha serikali yetu. Najaribu kufikiria kodi ya chumba cha hoteli imeishia wapi ama ndiyo mambo ya kulipa kwa hiyari?
Sitaki kukumbusha rasilimali ambazo peke yake zingeweza kuiendesha serikali yetu na kuleta maendeleo bila kuwabana wakulima na simu zetu za vitochi. Kuna majengo ya wawekezaji hayalipi kodi na yako katika misamaha miaka nenda miaka rudi na kwa bahati nzuri tunayajua majengo hayo.
Tunashindwa kupandisha kodi katika maelfu ya vitalu ambavyo wanaoitwa wawekezaji wanagombania kila siku kutokana na faida kubwa wanayopata, faida inayoletwa kwa kupunguza wanyama wetu katika mbuga zetu.
Tuna migodi ya ajabu, hadi migodi ya mchanga lakini hatuwezi kuongeza kodi kwa kisingizio cha wawekezaji kukimbia hapa nchini, wawekezaji wanaojua maana ya kulipa kodi, sina hakika lakini unaweza kuwa utani kwamba migodi peke yake ingeweza kuiendesha serikali yetu kwa gharama zote.
Kwa hakika napata taabu ninapoona wasomi wetu waliobobea katika uchumi wanapopelekwa kwa nguvu ya maji, nilitarajia watoe ushauri mzuri wa kisayansi ndani ya uchumi wa taifa letu, ili tuweze kutumia bongo zao badala ya bongo za kisiasa ambazo siku zote zinategemea nguvu ya wapiga kura imelala wapi, na ndiyo maana sikushangaa kuona kodi ya pikipiki na matoyo inashangiliwa kama vile kodi ya vileo imeongezwa.
Wananchi tupewe uwanja ili tuchangie maeneo tunayodhani yanaweza kuongeza mapato ya serikali. Kwangu mimi kufuta kodi katika pikipiki na matoyo na kuweka kodi ya laini katika simu naona hiyo ni hesabu ya magazijuto ambalo jibu lake lazima liwe hasi kiuchumi.
Teknolojia ya nini kama haiwezi kuharakisha uchumi? Basi ni bora tubaki analogi kuliko huko tunakotaka kwenda huku tukijua tunawaumiza akina Mzee Zuzu na wengineo.
Mzee Zuzu,
Kipatimo.