Nadhani kuna wakati kufikiria ndoto za Alinacha kwa maana za mchana kweupe, ni sawasawa na uendawazimu, lakini ndoto hizo hizo kuwaza kwa nia njema kunasaidia kuchukua hadhari kwa siku zijazo.
Leo nimeamka na ndoto ambayo kwa kila atakayeguswa na wazo langu, ajaribu kufanya kama anaota ili aone jinsi ndoto yangu inavyoweza kuwa na ukweli ndani yake na avute taswira halisi ya wakati huo na athari ambayo inaweza kuwa imejitokeza.
Siku zote nimekuwa nikizungumzia mambo makubwa ya zamani, nimeonekana kama mtu aliyepitwa na wakati na sitaki kwenda na wakati, lakini kitu kibaya zaidi naweza nikachukiwa na watu kutokana na mlengo wangu wa fikra za kizamani.
Kizazi hiki kimepata neema ya kufunguliwa vitu vingi, ni kizazi ambacho kinaweza kuwasiliana na dunia kutoka chumbani, ni kizazi ambacho unaweza ukavuna mamilioni ukiwa umekaa katika sebule yako ukinywa mvinyo (wine) na miguu juu.
Hiki siyo kizazi cha kusubiri mafanikio, ni kizazi cha kutumia kilichopatikana au kutumia cha mkopo ili kitakapopatikana kirejeshwe. Kwa ufupi ni kizazi cha kutumia kivulini na hakina uhusiano na jua la mateso ya kufanya kazi.
Kizazi hiki ndicho kinachotumiwa na wajanja wachache wanaocheza mchezo wa siasa za upatu, wanawatumia kwa faida zao na kisha kuwatelekeza baada ya mafanikio yanayoambatana na hasara ya maisha au mali.
Hiki ni kizazi ambacho hakiamini katika kuishi maisha ya kutegemeana, ni kizazi ambacho kinafikiria tumbo lake na la mwenzi wake, ni kizazi cha maisha ya wanyama waliokosa utashi, kizazi ambacho kinawaona wazee kama misukule ambayo haikupaswa kufunguliwa katika jela ya wachawi.
Ni kizazi ambacho kinawaona wazazi wazee kama mizigo inayopaswa kuondolewa katika familia, na ni kizazi kinachosahau nafasi yao katika jamii kwamba nacho kesho kinaweza kuzeeka.
Kizazi hiki fikra zake ni leo na siyo kesho wala jana, hakitaki kujifunza yaliyotokea na yatakayotokea, kipo kidigitali zaidi kwamba ili maisha yaende unahitajika kubofya zaidi na siyo kulima, unahitajika kuchati zaidi na siyo kuwinda.
Ni kizazi kinachofikiria kusoma kwa kukariri na siyo kusoma kwa kuelewa, ni kizazi kinachofikiria kuajiriwa na siyo kuajiri na kujiajiri, ni kizazi kinachofikiria fedha na siyo mazao, kizazi kinachofikiria starehe na siyo kazi, kizazi cha utapeli!
Kizazi hiki katika miongo michache ijayo kitakuwa kichekesho, kitafikiria kutumia teknolojia kujinasua katika maisha ya kweli, kujitibu kwa kutumia kompyuta, chakula kwa kutumia kompyuta na elimu kwa njia ya mtandao.
Ni kizazi ambacho hakijui mbinu mbadala ya kukabiliana na mambo, badala yake kitakuwa bendera fuata upepo, mafanikio ya mmoja yanageuka kuwa ya wengi na pengine kuwa funzo kwa wengine hata kama njia inayotumika siyo sahihi.
Ni kizazi cha kazi nyepesi nyepesi kama kuimba, kuendesha bodaboda au pikipiki, kuuza vocha, kuwa madalali wa wasafiri, kuwa madalali wa viwanja, nyumba, magari na mwishowe ukuwadi.
Ni kizazi kinachotegemea bahati nasibu zaidi kuliko kutafuta, kuwa freemason kama kweli wapo, kuwa waganga wa kienyeji wanaogawa majini ya bahati na kadhalika, kuwa waganga wa kutoa elimu kwa njia za giza, unaweza kufaulu bila kusoma ni njia ya mkato!
Ni kizazi cha wategemezi kwa kila kitu, kinachoweza kuishi kwa nguvu ya wachache, kuishi kwa matamasha, siasa, vurugu, maandamano, midahalo, mihadhara na sherehe, siyo kizazi kinachoweza kujitegemea kwa kufanya kazi za kutoka jasho.
Najua nimepitwa na wakati na ninafikiria vitu ambavyo ni ndoto za Abunuasi, ndoto za mchana, lakini tujipe muda halafu tutafakari kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa na tuone ukweli uko wapi.
Wasalaam
Mzee Zuzu
Kipatimo.