Nimeamka nikiwa na furaha sana baada ya kusikia kumbe tunatembea na bidhaa bila kujijua. Ni wachache ambao walikuwa wanajua kwamba Kiswahili ni fedha, hasa ni wale wenzetu ambao wanatumia mitandao ya kuzunguka duniani wakiwa wamekaa katika viti vyao, sisi huku Kipatimo ni kama tunashangaa, unawezaje kuuza lugha yako unayoitumia? Utabakiwa na nini?
Kuna mtu anatangaza hapa Kipatimo kuwa walimu wa Kiswahili wamepata ‘shavu’ la kwenda kufundisha Kiswahili nje ya nchi, inaweza ikawa Afrika Kusini, Sudan Kusini, Rwanda, Congo ya Mobutu Sese Seko Kuku wa Zabanga na kwingine, ikipendeza basi watapaa zaidi hadi nje ya Afrika. Walimu wanaonekana kufurahia taaluma yao kwa kuwa wengi wako nje ya ajira na sasa ajira zimekuwa bwerere.
Sisi huku Kipatimo, naamini na sehemu zingine za nchi hii – huko Chekeleni bado hawaelewi nini maana ya kuuza lugha. Kabla sijazungumzia maana, leo niwakumbushe kizazi hiki kipya na hata mbumbumbu wenzangu juu ya umuhimu wa lugha yetu. Hii lugha ndiyo iliyotufanya tukawa wamoja miaka ile ya kutafuta uhuru, ilitumika nguvu ya ziada sana kutufanya tuzungumze wote na tuache hivi vijikabila vyetu japo vina umuhimu sana na hatuwezi kuviacha.
Baada ya kuona tunazungumza lugha moja tukajiona wamoja na ndugu katika mapigano ya kudai uhuru, hii ndiyo ilikuwa nguzo ya kupata uhuru kwa amani bila kumwaga damu. Tuliongea lugha moja, Tanzania ilijulikana kwa kuwa na kabila moja kubwa la Waswahili. Baadhi waliamua kuiga ili nao wapate nguvu ya pamoja lakini ukabila kwao halikuwa jambo dogo kuliacha, bado walipopata uhuru waliendelea kumeguka na kuchinjana wao kwa wao.
Wapo waliopitia hapa kwetu na kujifunza mambo mengi ya kutafuta uhuru, wakiwemo wenzetu wa Afrika Kusini ambao wengi walikuwa huko Morogoro na mikoa mingine. Walipata mafunzo ya kijeshi na umoja, walipata nafasi ya kutangaza mipango yao ya kudai uhuru kupitia redio zetu za Idhaa ya Nje (External Service) wakati huo kuwahamasisha katika mataifa yao kwa lugha mbalimbali lakini si lugha moja, ndio ukawa mwanzo wa kupata uhuru kwa mataifa hayo.
Hii ni historia kubwa sana kwa taifa letu, ni jambo tunalojivunia mpaka leo bila kujali malipo kutoka katika mataifa hayo ambayo kimsingi yalitumia ardhi yetu kufanya mambo mengi kwa manufaa ya mataifa yao. Lazima wajue historia na ikiwezekana wakumbushwe walichokifanya katika nchi yetu. Nadhani hatuhitaji fadhila ya malipo bali tunahitaji heshima. Tulichohitaji wakati huo ilikuwa ni amani Kusini mwa Jangwa la Sahara ili nasi tuwe salama na tufanye maendeleo.
Wiki iliyopita mwanzoni, kupitia televisheni ya jirani yangu, nimemuona rais wetu akizungumza na Rais mpya wa Afrika Kusini, alizungumzia kuhusu kuwafundisha Kiswahili na kwamba nchi hiyo imeomba walimu wa kwenda kufundisha Kiswahili. Hii ni dhahiri kuwa wamejua umuhimu wa lugha moja na ambayo inaweza kuwaunganisha. Kiswahili si lugha ya kubeza na si lugha ya kukurupuka ukasema unaweza kufundisha, hasa lugha mwanana, wapo waliojinadi kuwa wameingia mkataba na hao tunawajua kuwa ni wepesi wa kudandia meli.
Nilifurahia kauli ya rais kwa sababu kubwa chache. Mosi, atakuwa ametengeneza ajira za kutosha kwa vijana wetu ambao ni mahiri katika lugha hii kwenda kufanya kazi huko, hao watalipwa lakini pia watakuwa wameweza kuuza lugha kwa njia ya machapisho na kusomesha.
Pili, bila kuumauma maneno atakuwa amekata kilimilimi cha wale jamaa ambao siku zote hujinadi kwa vitu ambavyo si vyao kwa maana ya kuwahi fursa. Ni jambo jema kwa kuwa limetamkwa na mamlaka ya juu kabisa, naamini vijana hawatapata taabu kabisa katika kupata fursa hizo kutokana na baadhi kuwa na ukiritimba wa wivu.
Nichukue fursa hii kumshukuru kiongozi wetu, lakini nitoe rai kwa mamlaka zinazohusika, fursa hizi ni kwa ajili ya wanyonge wa Tanzania, naamini walimu wa Kiswahili waliopo hapa Kipatimo wakipopoa vidaka pia watapata nafasi.
Lugha ni bidhaa kama ambavyo tuliuziwa Kiingereza kwa muda mrefu na kutuletea tabia zake, sasa tuuze Kiswahili na tabia zake tuone ambavyo ustaarabu wa Mswahili utakavyotutoa kimasomaso.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.