Nianze waraka wangu kwa kuwapongeza viongozi wote ambao wanafanya kazi kwa msukumo wa kuleta mabadiliko ya kweli katika maendeleo ya taifa hili, mabadiliko ambayo lengo kuu ni kumuinua Mtanzania huyu maskini kwa kipindi kirefu awe na ahueni  ya maisha. Zamani  kilimo kilikuwa ni salamu ya Watanzania.

Nchi yetu imepata bahati ya kuwa na wataalamu wengi wa mipango. Kuna mipango mingine ambayo tuliona kama ni zima moto, lakini miaka kadhaa iliyopita tulipata kuwa na mipango ya kutumia nguvu kazi iliyokuwepo kwa kuagizwa kila mwananchi mwenye miaka kumi na minane ni lazima awe na shamba la mazao ya chakula na biashara. Kwa hiyo mipango ya sasa ni lazima pia iendane na mahitaji ya kitaifa.

Katika hotuba za Rais wetu inaonesha tumelenga kufufua viwanda. Viwanda hivi ni lazima viendeshwe na malighafi kutoka katika mashamba yetu. Turejee Tanzania ya miaka ya 70 kabla ya kuamua kubinafsisha viwanda vyetu vingi siku za hivi karibuni ambavyo sasa ni mabohari ya kuhifadhi bidhaa kutoka nje ya nchi baada ya sisi kujisusa katika uzalishaji.

Niseme kuwa tutakapoimarisha kilimo kwa vijana wetu ambao ndio nguvu kazi kubwa tunayoitegemea, ni dhahiri kuwa tunaweza kufufua viwanda vingi vya kutengeneza bidhaa mbalimbali na ikiwezekana kuongeza viwanda vya mbolea ili kuwawezesha kupata mazao mengi.

Wakati wetu wa ujana  kulikuwa na kilimo cha kufa na kupona, lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha kilimo ndio unakuwa uti wa mgongo. Kilimo kinapaswa kuwa kipaumbele cha maisha yetu na kwamba biashara ni sehemu ya kilimo. Tofauti yetu na sasa kilimo ni sehemu ya biashara.

Wakati wetu pembejeo na vifaa vya kilimo vilikuwa kipaumbele zaidi ya vitu vingine. Tulianzisha viwanda kwa ajili ya utengenezaji wa vifaa vya kilimo na viwanda vya kutengeneza pembejeo, hatukuagiza kutoka nje, na havikuwa na kodi kumfanya mkulima awe na uwezo wa kununua.

Haya yote yaliwezekana kwa kupanga mipango madhubuti ya kuendesha siasa ya nchi yetu. Tulijua kwamba kilimo ni siasa na uongozi ni siasa, tulipanga muda wa siasa na muda wa kilimo. Tulipanga muda wa biashara na muda wa kushinda shambani, hivyo tulipunguza muda wa  siasa za majukwaa japokuwa tulikuwa na mfumo wa chama kimoja.

Iwapo tutafanya tena kilimo kuwa uti wa mgongo basi tutapunguza matatizo ya chakula na tutakuwa na akiba ya chakula cha kuuza nje na kujipatia fedha za kigeni. Tukipata fedha za kigeni tunaweza kufungua viwanda vingi na kuzalisha zaidi kwa ajili ya kuuza ndani zaidi na kununua kidogo kutoka nje. Tukifanya hivyo hali yetu ya uchumi itakuwa juu kuliko kutegemea kununua zaidi kutoka nje.

Tupunguze athari za utamaduni wa nje, bado tunaimani kwamba vitu vya nje vina ubora zaidi kuliko vyetu. Tumesahau viatu vyetu, nguo zetu, matairi yetu, ngozi yetu, mapanga na majembe yetu, vyakula vyetu na kila kinachoagizwa na kuingizwa nchi. Tutukuza hata visivyotukuzika na ambavyo vinatufedhehesha kama taifa.

Haya yote yanatakiwa kutazamwa na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwawezesha wananchi kukabiliana na umuhimu wa kilimo ili tufanye kilimo kuwa cha kufa na kupona na kilimo kuwa uti wa mgongo.

Tukiweza kugeuza fikra za biashara kuwa kilimo ni dhahiri tutakuwa tunaondokana na adui njaa na umasikini, na pia utumwa wa kulazimishwa chakula kutoka nje.

 

Wasaalam ,

Mzee Zuzu,

Kipatimo