Kuna wakati nilipata kuwa monita wa darasa langu miaka hiyo ya zamani, uongozi ule nilidumu nao kwa muda wa wiki moja hivi kabla sijatumbuliwa na mwalimu mkuu mbele ya wanafunzi wenzangu asubuhi ya paredi, niliahidiwa kupewa kazi nyingine na baada ya wiki kadhaa nikapewa kuwa mtunza muda.
Ukweli ni kwamba sikuelewa madhara ya kutumbuliwa kwangu kuwa monita yataniathiri sana katika maisha yangu ya uongozi hapo shuleni, na hata katika maisha ya kawaida huku uzeeni, mpaka leo wale niliosoma nao tukikutana tunakumbushana jinsi nilivyotumbuliwa madaraka yangu enzi zile, huwa najisikia vibaya hata kama naonekana nacheka.
Kutoaminika kwa walimu na mwalimu mkuu kiasi cha kutoswa madaraka makubwa ya kuongoza darasa zima hadi kupewa saa na kengele, ni ishara kwamba nilionekana sifai kuwa kiongozi kwa makosa ambayo niliyafanya – iwe kwa kushindwa kusimamia au kurubuniwa na wahuni wenzangu – kufanya mambo ya kutoaminika.
Nakumbuka kabla sijafutwa kazi, niliitwa mbele ya jopo la walimu na kuulizwa makosa kadhaa ambayo niliyafanya, kwa akili ya kitoto nilijibu uongo wa kutukuka kwa kujiamini nikidhani kwamba akili za walimu zinakaribiana na zangu.
Nilikuwa na makosa ya wazi kabisa, kwanza utoro wa kwenda kuvua samaki muda wa masomo bila kuzingatia madaraka makubwa niliyokabidhiwa na uongozi wa shule, pili kusingizia wanafunzi wanaopiga kelele wakati ukweli ni kwamba wapiga kelele walikuwa marafiki zangu ambao wengi wao walikuwa mabwege darasani.
Dhima ya uongozi niliyopata ilikuwa kuwatumikia wanafunzi wa darasa langu kwa ukweli na uaminifu, mimi nilizembea na kutotekeleza ahadi ambayo niliaminiwa na uongozi wa shule, wapo wanafunzi wenzangu ambao walikuwa na akili wananichukia mpaka leo kwa makosa ya kuwasingizia, wapo mabwege wenzangu ambao mpaka leo wanaamini niliwabeba sana darasani lakini katika maisha wanapambana peke yao.
Leo, nimekumbuka hadithi hii na kuamua kuwaandikia barua hii kuwaelezea madhara ya matumizi mabaya ya madaraka na jinsi ambavyo unaowabeba bila sababu wanavyoweza kukuharibia kazi yako, wale mabwege wenzangu ndiyo waliofikisha taarifa kwa walimu kuwa mimi ni mvuvi mashuhuri mtoni, ndiyo haohao walionigeuka na kusema kuwa naandika majina ya wapiga kelele ambao siyo wenyewe.
Nadharia hii haiishii shuleni tu katika uongozi, inaendelea hadi katika ngazi za uongozi wa jamii kubwa na Serikali. Siku za hivi karibuni tumesikia tuhuma nyingi za watu kutumbuliwa katika ngazi mbalimbali, wanaotumbuliwa baadhi yao wanaponzwa na marafiki ambao si watu wazuri katika maisha ya kawaida, wanapata faida ukiwa kiongozi na baada ya faida wanakuharibia ili kujiosha kwa watawala wengine wakiamini wataaminika wao kuliko wewe.
Wengi wetu tunasahau msemo huu wa ‘kikulacho ki nguoni mwako’, wengi wa waliotumbuliwa nyuma, yao kuna watu ambao wanahusika moja kwa moja na kashfa ambazo zimesababisha kutumbuliwa kwa kiongozi, wengi wetu tumeponzwa na marafiki ambao si waaminifu, marafiki ambao wametushauri tuwaumize watu waadilifu kwa kisingizio cha madaraka.
Hili ni somo kwa wengine ambao bado hamjatumbuliwa na kuyajua makosa yenu baada ya kutumbuliwa, wajibu wetu kama viongozi ni kuhakikisha tunawatumikia watu wote kwa haki bila kujali na kuweka mbele urafiki ambao unawaathiri watu wengine. Wengi wetu tumeendeleza urafiki katika madaraka ambayo ni dhamana tu tukiamini vyeo vyetu vya kudumu na kufanya mambo ambayo yana athari na kuathiri jamii tunayoiongoza, tunapoambiwa makosa yetu tunajaribu kutoa sababu ambazo kimsingi haziingii akilini kwa watu wenye akili.
Hivi; matumizi mabaya ya fedha za umma yana utetezi gani? Hivi; matumizi mabaya ya madaraka yana utetezi gani? Hivi; kufanya kazi binafsi muda wa Serikali kuna utetezi gani? Hivi; kuwaonea wananchi au kutotekeleza ahadi za Serikali kuna utetezi gani?
Wapo watakaopewa nafasi ya kuwa ‘time keeper’ kama mimi, naamini itakuwa bahati, mimi nilipata kwa kuwa nilikuwa najua kusoma saa enzi hizo, je, nyie wa leo kwa dunia ya watu kujua mambo, mnadhani kuna sababu ya kuwajaribu tena?
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.