Thamani ya binadamu yeyote inabebwa na dhana ya utu alionao, na utu wa muungwana yeyote ni kufanya kazi kama kipimo cha utu wake. Wapo wanaofanya kazi zisizo rasmi lakini zinawaingizia kipato na wapo wanaofanya kazi rasmi na haiwaingizii kipato, thamani na utu wa mtu utaendelea kuwapo hata kama matokeo ya kazi anayofanya ni tofauti na matarajio yake.

Katika barua zangu zote huwa najaribu kukumbuka mambo ya miaka kadhaa iliyopita ikiwa ni kigezo cha kujua thamani ya mambo baada ya muda kupita, nimewahi kukumbuka mambo ya siasa, michezo, uongozi na kadhalika, leo nimeona niwashirikishe nikumbuke utu wa kazi kwa Mtanzania niliyemfahamu mimi miaka ile ya mwanzoni kabisa tunaanzisha gurudumu la maendeleo ya nchi hii.

Kazi ni utu, hii ni kaulimbiu iliyokuwa ikituchoma sana ujanani, wakati huo thamani ya mtu inajulikana kutokana na majukumu yake katika familia na Taifa kwa ujumla, thamani yake inaonekana kwa vitendo, kazi yake inathaminiwa kwa matokeo chanya ya kuona aliposimama katika utendaji kazi.

Inawezekana kabisa maendeleo yakawa na tija kubwa kwa vijana na Taifa. Maendeleo ni kitu kizuri sana kwa dhana ya kuondoa maendeleo ya kiujima na kuleta maendeleo ya kisasa, unayoweza usielewe kipimo dhahiri cha maendeleo hadi utakapokokotolewa na wataalamu wa maendeleo ya kisasa.

Siku za hivi karibuni, nilikuwa najiuliza maswali mengi sana ambayo – labda kutokana na ushamba wangu – nashindwa kujijibu mwenyewe. Ni kama kuuliza maendeleo ni kuwa na maisha bora au kufanana maisha na mtu mwingine tunayedhani kafanikiwa?

Kuna maswali mengi ya msingi sana, maswali ambayo mjima yeyote anaweza akajiuliza kwa nafasi yake, kwangu mimi na ujima wangu naweza nikajiuliza hivi teknolojia ni kigezo cha kuonesha mafanikio ya mtu? Teknolojia ni kigezo cha heshima na utu wa mtu?

Zamani wakati tukiita kazi ni utu tulimaanisha mtu kuonekana na kuonesha alichofanya ni kigezo muhimu cha maendeleo ya mtu kwa jamii inayomzunguka, tuliutumia utu huo kama shamba darasa kwa wengine ili wajue thamani ya binadamu, tulitumia kama kigezo cha kijamii katika mambo mengi yakiwamo uongozi na ushauri katika jamii yetu.

Zamani mtu asiye na kazi alionekana hana utu. Huyu mtu asiye na kazi alitafsiriwa kama mtu mvivu katika jamii si kwa sababu hajaajiriwa na kwa sababu hajaamua kuonesha watu utu wake wa kuwajibika kwa kazi za kujiajiri mwenyewe, suala la ajira binafsi lilikuwa la mwanzo kabisa kabla ya kufikiria kuajiriwa na kulipwa mshahara.

Zamani utu ulitukuzwa kwa kuionesha jamii inayokuzunguka kwa kufanya kazi. Kazi ilikuwa kulima mazao yote ya chakula na biashara, ilikuwa kufanya kazi zinazogusa jamii na zenye muashirio wa mafunzo kwa wengine, zamani kulikuwa hakuna kazi za kufikirika.

Nimewiwa na jambo hili la kuchanganya aina za kazi na utu – hivi uigizaji ni kazi ya utamaduni wetu au imeingiliwa na utamaduni wa wengine? Hivi udalali ni utamaduni wetu wa kweli tuliokuwa nao tangu enzi na enzi?  

Najiuliza nafasi ya biashara wakati wetu na sasa ikoje? Ni kweli kwamba teknolojia inapaswa kupewa kipaumbele kwa jamii yetu sasa kwa maendeleo tuliyonayo dhana nzima ya utamaduni wetu? Hatuoni kama tunabinafsisha uhalisia wetu?

Hivi yale mataifa mengine ambayo yameamua kuuenzi utamaduni wao katika maendeleo wako wapi katika dhana ya kazi ni utu wa binadamu katika nchi zao? Ni maswali ya kijinga ninayojiuliza na nina imani mwenye akili za kisasa anaweza kuniona mjinga lakini kinachoniponza ni uzamani. 

Ushauri wangu wa bure; ni vema tukayatazama maendeleo kwa mukhtadha wa maisha yetu na utamaduni wetu jinsi ulivyo, tusijifananishe na utamaduni wa wengine kwa maendeleo yao kwetu, ni dhahiri kuwa wao ni wao na kwao na sisi ni sisi na kwetu.

Kimsingi maendeleo yao yanaweza yakahuishwa na utamaduni wao, utamaduni ambao hauna nafasi katika kuchangia maendeleo yetu kwa uhalisia wetu, tuwaone wao kama changamoto yetu kupigania maendeleo yetu kwa utamaduni wetu kabla hatujauza uhalisia wetu.  

 

Wasaalam 

Mzee Zuzu

Kipatimo.