Mwaka 1974 katika rekodi ya vijiji bora Tanzania kwa kilimo, ufugaji  na maendeleo ambavyo Julius alivipatia zawadi, ni pamoja na Kijiji cha Lwanzali kilichopo mkoani Njombe. Kijiji hiki kilipewa tangi kubwa la maji tena la chuma na mabomba yake ili kuunganisha maji kwa kila mwanakijiji.

Sifa mojawapo kubwa ambayo kijiji hiki kilifanikiwa kuingia katika mchakato wa mashindano ya vijiji ni utunzaji wa mazingira, hasa upandaji miti katika mpango mzuri wa kufanya kijiji kipendeze pamoja na ujanishaji pembezoni mwa kijiji chenyewe na kufanya mtiririko wa maji kuwa wa kuvutia.

 

Nakumbuka wakati huo kulikuwa hakuna wizara ya mazingira, kama ambavyo leo imepachikwa mahali chini ya ofisi ya mtu mkubwa sana kwa maana ya kupewa kipaumbele, miaka hiyo tulikuwa hatuna tatizo la maji wala mito, tulikuwa hatuna tatizo la mvua wala mkanganyiko wa hali ya hewa.

Kwa ufupi tuliweza kuwa na ratiba binafsi ya kujua mvua za vuli zitaanza kunyesha lini, hatukuhitaji wasomi ambao walikuwa wanabashiri mvua kama ilivyo leo, kwamba mvua na manyunyu na ngurumo za hapa na pale zitakuwapo na matokeo yake jua la utosi linatuandama.

 

Haya yote yalitokana na utunzaji wa mazingira ambayo tuliweza kufanya kutokana na ratiba nzuri na uongozi bora wa viongozi wetu wa kata, tarafa na wilaya ambao kimsingi elimu yao ilikuwa ndogo sana, walitumia nyongeza ya uzalendo zaidi katika kukabiliana na changamoto za kimaendeleo.

Tanzania ya leo si ile ya miaka ya 1970, Tanzania iliyokuwa na viongozi wasio wasomi, Tanzania ambayo ilikuwa haina wizara maalum ya mazingira kama kumbukumbu zangu zipo sahihi, naikumbuka Wizara ya Aridhi, Makazi na Nyumba, labda ndiyo iliyopewa dhima hiyo.

Kwanini nimeamua kuandika barua hii leo kwenu kizazi cha dotcom? Nina sababu nyingi sana; ya kwanza nataka nichukue fursa hii adhimu kuwalaani ninyi dotcom pamoja na viongozi wenu ambao mmeshindwa kuendeleza ule utamaduni wetu wa utunzaji wa mazingira.

Pili, pamoja na usomi wenu mmeshindwa kujua dhahiri kuwa bila utunzaji wa mazingira hamtakuwa na ratiba nzuri ya kujua misimu ya mwaka inakwendaje, mmekuwa wasomi na wajanja msio na macho ya kuona kuwa sasa mnakosa maji kutokana na kuharibu kwa makusudi vyanzo vya maji.

Kwa akili ya haraka ya dotcom na usomi wa kisasa,  mnadhani ni busara kuanza kukinga maji kutoka katika maziwa na bahari ili muweze kuyatumia katika matumizi ya kawaida, uchapushaji wa maji kwa kutumia misitu na utunzaji wa mito ni hadithi kwa kizazi chenu, kila mtu amefikiria tumbo lake kujineemesha kwa kuangamiza kizazi kijacho, uzalendo wetu umewashinda.

Natazama ramani ya Tanzania na sifa ya mito iliyokuwa ikitiririsha maji sehemu mbalimbali, natamani kulia.Natazama misitu iliyokuwa ikiifanya Tanzania kuwa nchi nzuri inayopendeza kwa misitu asili naona uchungu.

 

Leo kuna mabonde yaliyokuwa yakipitisha maji, leo kuna majangwa yaliyokuwa misitu, haya yote yamefanyika katika kipindi ambacho Tanzania imejaaliwa kuwa na hao wanaoitwa wasomi wabobezi, wasomi wanaozijua sera za maendeleo.

Inawezekana kusoma hatujui lakini kuna usemi kwamba hata kama hatujui kusoma ni kweli kuwa hatuwezi kugundua kitu kwa picha? Hivi ni kweli viongozi wetu mnaoshinda angani na kwenda kutua kwenye nchi za wenzetu hamuoni jinsi kulivyo na mandhari za kuvutia katikati ya mji?

Hebu nendeni Washington mkaangalie mji ulivyo na mandhari nzuri na kupambwa kwa miti mikubwa mikubwa ya asili katikati ya mji, nendeni Vatican, Paris, Stockholm, Brussels haya hata hapo Goma, Kongo kwenye vita kila siku bado wanatushinda. Kulikoni wale viongozi kama wa Kijiji cha Lwanzali huko Lupembe, Njombe wako wapi leo?

Tunategemea nini kama tunashindwa kutunza miti ambayo haitugharimu kitu chochote zaidi ya faida kubwa ambayo tutapata kutoka katika miti hiyo, udhibiti wa hali ya hewa, mvua, vyanzo vya maji, usafi wa mazingira, mandhari nzuri ya miji na vijiji, akili yetu ya dotcom na usomi wetu uko wapi, tunadhani tunaweza kubadili hali hiyo kwa semina na makongamano ya posho kila siku?

Ile kaulimbiu yetu ya ufukara wa elimu miaka ile ya kuwa na ekari moja ya miti kwa kila mwananchi mwenye umri wa miaka 18 mmeona ni ujinga kwa maisha ya sasa ya dotcom? Mmeona ni fahari kuwa na nchi ambayo ni jangwa, mnadhani tunaweza kuwa na mandhari nzuri kwa maua na miti ya Kichina? Mnadhani biashara ya mbao na magogo ni muhimu zaidi kuliko mazingira yetu?

Tazameni hapo mjini kwenu Dar es Salaam mnapowapokea wageni wenu wanaokuja kutoka katika mataifa yaliyoendelea na jinsi, ambavyo wanapaona palivyo jangwa na majanga, hakuna miti kutoka uwanja wa ndege hadi ikulu na vijiti vidogo vilivyopo bado mnakataa sababu ya msingi hakuna, mnakwenda wapi? Usomi wenu unasema nini juu ya mimea na afya za viumbe?

Nendeni mikoani kote na sasa hadi Kijiji chetu Bora cha Lwanzali ni majanga ya jangwa na wasomi mpo, viongozi mpo, wananchi msio wazalendo mpo, siasa za majukwaani zitawafikisha wapi? Kazi kwanza na siasa ni kilimo si maneno.     

 

Mzee Zuzu 
Kipatimo.