Watu wengi wanasifu kasi ya kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘hapa kazi tu’, na kweli inaonekana kuna kazi inafanyika, matokeo chanya yanaonekana dhahiri bila shayiri na kwamba kwa kasi hii baada ya miaka mitano kutakuwa na kitu cha kuwaonesha Watanzania kutokana na utendaji wake.
Ni dhahiri kuwa mema mengi yataonekana na kuyaziba machache yaliyofanywa kwa bahati mbaya kutokana na kasi tuliyonayo.
Leo naandika barua hii nikiwa najua baadhi ya mambo ambayo awali nilidhani kuwa hayawezekaniki katika nchi yetu, lakini kumbe ni jambo la muda na uongozi tu kuwa tiba kwa Taifa letu ambalo lilifika mahali pasipowezekanika kwa jeuri ya Watanzania.
Hii ndiyo Tanzania ya ukiritimba huko bandarini kiasi cha baadhi ya watu kuchukia kuwa na mizigo au hata kutuma mizigo. Kulikuwa na miungu-watu ambao kila ukiwaona inakuwa kama unamuona kiumbe wa sayari nyingine, kuna watu waliofikia kujiona ndiyo wenye uamuzi wa mwisho hapa duniani kupitia bandari ya Tanzania japokuwa tuliwapa dhamana tu ya madaraka.
Utumishi wa umma ulikuwa ni jambo la kujitolea na siyo kuitendea haki taaluma uliyoajiriwa nayo. Kiufupi, lilikuwa eneo la kuchuma, lilikuwa shamba la kupewa na wananchi kwa ridhaa yao na kugeuka kuwa chifu na kurithisha familia, hali ilikuwa mbaya maeneo mengi na sasa tumeanza kuona mabadiliko makubwa kwa kasi ya ‘hapa kazi tu’.
Suala la rushwa japokuwa halijaisha kabisa lakini nadhani kwa asilimia nyingi kuna upungufu wa kudai ‘cha mbele’. Sasa hivi imekuwa mtoa rushwa anasoma alama za nyakati kutoa na mpokea rushwa anasoma alama za nyakati kupokea. Kwa kasi hii naamini itafika wakati ambapo hata nyakati hazitasomwa kwa kuogopa kutoa au kupokea.
Masuala ya afya yameboreshwa sana, huduma imekuwa ikipatikana japokuwa kuna uduni wa huduma za dawa na vifaatiba, taratibu tutafika. Kuna upungufu wa matabibu lakini hakuna ubosi wa matabibu kama zamani, kunapotokea upungufu kuna sababu ya msingi nyuma ya kushindwa kutekeleza majukumu. Haya ndiyo yaliyokuwa matarajio ya Watanzania wengi kabla ya kuamua nani ashike mpini wa awamu ya tano.
Shuleni mambo ni shwari japokuwa hatuwezi kuwa na mabadiliko ya haraka kwa ukubwa wa tasnia yenyewe, itachukua muda kidogo kupata mabadiliko ya asilimia kubwa, ukiangalia tulikokuwa miaka miwili tu iliyopita na tulipo sasa ni kama mazingaombwe. Inasemwa kuwa kwa sasa hakuna mwanafunzi anayekaa chini na kwamba shule nyingi michango imesitishwa, ni jambo la kupongezana kwa ufanisi huu.
Hali ya ufanyaji kazi imebadilika, watu wanafanya kazi kuliko zamani ambapo watu walikuwa wakiamka na kushinda vijiweni wakisogoa huku wakipata fedha za dili kwa maana ya kuiibia Serikali, au watu wengine ule ujanja wa kuishi kwa dili umeanza kupotea kabisa. Kwa ufupi mpiga dili hana dili na mpigwa dili kashtuka sasa kaulimbiu ya kilimo kwanza inaweza kusawiri baada ya watu wengi kuonekana wakiuliziaulizia namna ya kulima na upatikanaji wa mashamba.
Kiufupi, kilimo kinazungumzwa sana na vijana katika kipindi hiki cha awamu ya tano. Ufugaji ni kama umeshavamiwa sana na akinamama waliopo mjini na kuokoa maisha ya wapiga dili wengi ambao ndiyo waliokuwa akinababa – viongozi wa familia.
Matumizi ya ponda starehe hayapo tena, baa nyingi zimekuwa wazi hazina wateja kutokana na majukumu ya kile watu wanachokipata. Kwa ufupi, familia nyingi zinaishi kwa bajeti halisi ya kile kinachopatikana, bajeti zinasomwa kila mwezi ndani ya familia na wanaangalia vipaumbele na kupitishwa, atakayetumia vibaya anawekwa kilingeni ili ajieleze imekuwaje ametumia bila kuzingatia bajeti iliyopitishwa na familia.
Nidhamu ya kuishi kifamilia imerudi, baadhi ya ndoa zimetengemaa na baadhi ya michepuko imesalimu amri na kurejea kutwanga jembe kijijini, saluni za kusingana sasa zinasinga zaidi maharusi na siyo wasichana wa mjini kama ilivyokuwa zamani. Hii ndiyo kasi ya awamu ya tano.
Rai yangu kwa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuomba iende taratibu maana waumiaji ni wengi, hasa katika kipindi hiki ambacho mabadiliko yanakuja kwa kasi vilevile.
Wasaalam
Mzee Zuzu
Kipatimo.