Nakumbuka sana kuhusu andiko langu la kitabu ambalo liko toleo la mbali kidogo, lakini nitakuwa sina fadhila iwapo siku hizi za mwisho wa mwaka na sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo nitajitoa fahamu ya kusahau umuhimu wa kumaliza mwaka na kutakiana heri ya Mwaka Mpya na kuombeana mambo mema mapya kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Kwanza, niwape pongezi nyingi sana kwa kusherehekea Sikukuu ya Krisimasi na makanisa yote yalihubiri upendo na utengamano, hiyo ndiyo kazi kubwa ya viongozi wa dini duniani. Jukumu letu kama wananchi na waumini ni kuchagua njia nyoofu kwa faida ya amani na upendo kwetu sisi wenyewe.

Mwaka huu unakwisha kama ambavyo miaka mingine imekwisha, hakuna jambo jipya zaidi ya kubadilika kwa namba ya mwaka. Yale malengo ya muda mfupi na muda mrefu tuliyojiwekea baadhi yamekamilika na mengine yamepata mkwamo ama wa kiuchumi na pengine kutokana na uvivu.

Najua kuna watu wengi walikuwa na mipango mingi kwa mwaka huu ambao wataalamu wa mambo ya nyota walisema ni mwaka witiri. Mwaka witiri ni mwaka ambao watu hufanya maajabu ya kimaendeleo, lakini wapo ambao mpaka mwaka unakwisha wapo kama sisi wengine ambao kimsingi mambo yalikuwa si mambo, kila kitu kilikwama kwa sababu mbalimbali.

Kwangu mimi sikuwa na matarajio makubwa sana ambayo nilijipangia. Kwanza, nilipanga kusajili namba yangu ya simu kwa alama za vidole, jambo ambalo kimsingi nimelikamilisha kwa asilimia zote mia. 

Jambo la pili lilikuwa kuandikisha shamba langu la mikorosho ili nipate hati ya kimila, nalo limefanikiwa kwa kiwango kizuri sana. Sikuwa na mipango mikubwa kama kumiliki maghorofa na kununua magari ya kifahari kama vijana wengi walivyojipangia.

Najua vijana wana mipango mingi huku wakijua dhahiri kwamba kila mpango mkubwa unahitaji fedha nyingi, lakini wao wakiwa na matumaini bila kufanya kazi, najua matumaini ya wanasiasa kufikia malengo yao japo baadhi ya watu wakifanya vikwazo vyao kuwa kipaumbele, najua matumaini ya viongozi wa dini na jinsi ambavyo waumini wanakuwa vigeugeu kwa madhehebu yao.

Haya ndiyo matokeo ya kila mwaka kuuona kama mwaka wa mkosi kwa kila mtu, mambo ya msingi ya kiimani yanazidi kuporomoka kutokana na watu kuamini zaidi mambo ya giza huku wakiwa washirika wazuri wa neno la Mungu. Tukiamua kubadilika na kushika moja, tena moja lenye tija, hakuna litakaloshindikana.

Najua jitihada za kimamlaka na siasa kwa mataifa yote duniani na jinsi ambavyo kuna siasa za kushindana na kuharibiana kwa kiwango kikubwa. Haya ni matokeo ya  kushindana katika boksi la kura na mbadala wa sera mbalimbali, tukikubaliana kutokukubaliana na kushikamana kwa pamoja basi miaka hii witiri ingekuwa inatutoa katika shimo na kutupeleka katika mitungi ya asali na maziwa.

Kundi la vijana ambalo linataka mafanikio ni moja kati ya makundi ambayo huwa yanamaliza mwaka vibaya sana, hasa pale wanapoona hawajafikia malengo yao. Wapo walioingia katika imani za kishirikina ili wafanikiwe lakini wameishia katika mikono ya dhambi. 

Wapo waliotumia nguvu za ziada nao wameishia katika mikono ya watu wenye hasira. Hapa kuna kitu cha kujifunza kwa vijana kwamba ni lazima wawe na mipango ya muda mrefu, hasa kutokana na umri wao.

Lakini tukiachana na yote, tunapoanza mwaka mpya, mwaka ambao hauna tofauti yoyote na miaka mingine bali ni tarehe tu za mwaka, tunapaswa kujua kuwa jitihada zetu zinamilikiwa na nguvu ya uwekezaji wa kweli bila kuvunja sheria. 

Na sisi ambao ni wanasiasa tunatakiwa kuwa na sera za uhakika kwa ajili ya manufaa ya jamii tunayoiongoza katika kipindi cha muda mrefu na hali kadhalika walimu wa dini waendelee kufundisha neno jema kwetu ili turudi katika mkondo mwema.

Nina mengi ya kusema lakini itoshe kusema, heri ya Mwaka Mpya na hakuna tofauti ya miaka bali tuwekeze kwenye mikakati ya muda mrefu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.