Wanangu, hongereni kwa kuvuka mwaka uliopita na kuukaribisha mwaka mpya na mambo yaleyale ya mwaka jana kwa tofauti ya tarehe na mwaka, nawapa kongole kwa sababu baadhi yetu tukiingia mwaka mwingine tunajitengenezea malengo ambayo lazima yatekelezeke.
Furaha ya kuukaribisha mwaka mpya kwangu ilipotea miaka mingi baada ya kuona hakuna tofauti ya mwaka ninaouaga na unaofuata, hakuna malengo yanayotimizwa kwangu au kwa nchi yangu, naona ni kama utamaduni wa ulimbukeni kutoka Magharibi ambao wanajua wanafanya nini katika kipindi fulani.
Wanangu, kwa kipindi kirefu kidogo nimekuwa nikiomba kazi mbalimbali serikalini kutoka kwa mwajiri mkuu, yaani mkuu wa nchi. Ajira pekee ambayo naipenda ni kuwa waziri mtendaji na siyo waziri mwanasiasa, lengo langu ni kutaka kutoka hapa tulipo kwenda japo hatua chache mbele za kimaendeleo.
Nimeomba nafasi nyingi mpaka leo lakini sijapata hata moja, labda inawezekana sijafiti kutokana na sera zangu lakini rai yangu ni moja kwamba mawaziri walioko katika sehemu hizo basi wajaribu kuchukua mawazo yangu na kuyafanyia kazi.
Wanangu, lengo langu la kuomba kazi ni kutaka kujaribishwa kama ninaweza ama la, lakini katika barua zangu nilimwambia mwajiri kwamba atakaponiteua nitaomba niongee naye faragha kumwomba radhi ya hatua madhubuti ambazo naweza nikazichukua kisheria, na tukumbuke kuwa sheria inauma na kukata, wapo watakaopiga kelele za maumivu na wapo watakaoona ahueni ya maisha. Watakaopiga kelele za maumivu ni wale ambao kwao kuvunja sheria ni jambo la kawaida.
Namshukuru Mungu kwa kuwa hadi sasa kwa umri wangu sijawahi kufungwa na kesi yoyote mahakamani ya Tanzania huru, kosa moja tu ambalo nilifungwa ni la wakati wa mkoloni lilihusu kuendesha na kutembea na baiskeli ambayo nilikuwa sijailipia ushuru wa barabarani, wakati ule risiti za kulipia zilikuwa zikibandikwa katika nanga.
Nakumbuka nilitumikia jela kwa miezi sita kule Ulanga Morogoro japokuwa sikuweza kuendelea kuilipia baiskeli hivyo nikaiuza ili nisiwe mkwepa kodi kwa serikali ya mkoloni iliyokuwa ikitutawala.
Leo baada ya miongo kadhaa bado nakumbuka kadhia hiyo ya kwenda jela kwa kosa la kutolipa kodi, nilitengenezwa kiimani kwamba kodi ni kitu muhimu kwa taifa lolote ili liweze kuendelea katika kutoa huduma kwa wananchi. Tanzania ni taifa kama yalivyo mataifa mengine ambayo yanakusanya kodi na kutusaidia sisi wenye baiskeli nyingi barabarani na hatulipi kodi kwa baiskeli zetu.
Wanangu, siku kadhaa wakati wa sherehe za wafanyakazi duniani nilipata kumsikia mtu akilalamika kwamba nchi hii ya Tanzania walipakodi wa kweli ni watumishi wa serikali, wao hawawezi kukwepa kulipa kodi kwa sababu kodi zao zinakatwa moja kwa moja na mlipaji (serikali).
Wanangu, leo naenda mbele ya rais tena kuomba kazi ya kuwa waziri wa kodi kwa kuwa mianya mingi ya kukwepa kodi naiona, nawaona wachache wanavyonufaika na wengi wanavyoumia kwa kutolipa kodi stahiki serikalini.
Wanangu, kuna mambo ambayo mtu wa kawaida hawezi kuyafanya hadi atakapokula kiapo cha kutanguliza kifo, kwamba nitalitumikia taifa hili kwa tone langu la damu kuhakikisha kile ninachokifanya kinatekelezeka bila kuleta mizengwe ya kisiasa, upendeleo kwa hasara ya taifa, bila kumuogopa mtu kwa madaraka yake na historia yake ya nyuma.
Wanangu, nasikitika malezi tuliyonayo, kwa maana ya kuogopa kulipa kodi kana kwamba ni adhabu badala ya kuwa tunu na jambo la kujisifia mbele za wenzako. Unaona ufahari na ujanja kutolipa kodi kwa taifa ambalo unaishi na kuhitaji huduma zake za kijamii na kwamba tuko mbele kudai serikali haifanyi maendeleo yoyote ilhali hujalipa kodi tangu uzaliwe.
Wanangu, sijapata bahati ya kutembea nchi mbalimbali zilizoendelea lakini taarifa nilizonazo ni kwamba wenzetu kulipa kodi ni jambo la kifahari, si hiyari wala kulazimishana kama ilivyo kwa Tanzania yetu, imefikia mahali kodi yao baada ya kutimiza yale ya msingi yaliyoko kwao sasa wanaweza kutusaidia hata sisi wakwepa kodi tunaoona fahari.
Sasa leo kwa heshima na taadhima naomba rais wangu nipe ajira ya kuwa waziri wa kodi uone jinsi ambavyo nitatumia sheria ikate watu waumie na waone TRA ni mahali pekee pa kukimbilia kukwepa matatizo yanayoweza kuwapata, nisingependa kuwa waziri mwanasiasa ambaye nategemea kura za walipakodi, ningelipenda kuwa waziri mtendaji, niwatendee Watanzania hawa na kuipenda nchi yao kwa kulipa kodi bila kusukumwa au kupewa elimu ya kulipa kodi.
Naangalia mianya ya kawaida tu ambayo ningeweza kuisimamia vizuri kama madini, maduka, kampuni, biashara za udalali, baiskeli, pikipiki, maguta, kodi ya mazao, viwanja vya starehe, majengo, kampuni za simu, uvuvi, usafiri, wamachinga, kitimoto, gereji, mashamba na kuona ufahari wa kodi ambayo ningeikusanya. Huwezi kuwa na taifa lenye vitu vyote hivi halafu wasilipe kodi.
Mimi nilifungwa miezi sita Ulanga mwaka 1958 kwa kosa la kuendesha baiskeli ambayo haikulipiwa kodi ya mwaka, iweje leo mtu amiliki kiwanda halafu akwepe kodi halafu achekewe? Mheshimiwa Rais kama unataka tuendelee hatuna budi kupageuza TRA kuwa kimbilio la wanachi kulipa kodi na ili iwe hivyo nipe kazi ya kuwa waziri wa kodi uone na ili nisidanganyike sitahama Kipatimo.
Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo – kidumu chama changu cha TANU.