Nawapa hongera wale wote tuliotoa michango yetu ya hali na mali mwaka 1978 hadi 1980 wakati wa vita ya kumtoa yule jamaa wa Uganda aliyekuwa na mbwembwe nyingi za maneno na vitendo. Kuna wakati, kwa akili yake ya kuvukia barabara, alitaka wakutane na Julius ulingoni wachapane makonde, hiyo ndiyo akili ndogo katika kichwa kikubwa.
Wakati ule hatukuwa na jeshi hasa la vita. Tulikuwa na jeshi dogo lenye wazalendo wengi na likiwa limezungukwa na vijana wengi waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na wazee wachache wenye kutoa mawazo ya ukweli katika kukabiliana na janga la Taifa, mawazo ambayo walijua fika kuwa hayana manufaa yoyote kimapato kwao bali kwa Taifa lao.
Julius pamoja na Moringe kwa kauli moja wakatangaza vita ya kumtoa adui katika eneo letu kule Kagera huku wakijua fika kwamba jeshi letu ni dogo na duni kwa vifaa, lakini wanaume wakatangulia bila chakula wakaanza kazi na chakula kikafuata.
Hili ndilo lililokuwa jeshi. Jeshi la vita. Watanzania wengi tulikuwa tukipata ripoti ya vita kupitia RTD ya ukweli ya wakati ule, na mtangazaji aliyekuwa mstari wa mbele aliitwa Hamisi Kikoroma almaarufu Ben Kiko.
Nakumbuka vita ile sana kwa sababu iliniathiri hadi leo. Tumefunga mkanda baada ya ushindi, wengine wakafungua, tumetoa michango yetu ya hali na mali wengine leo wanaitumbua bila kujua sisi tulitoa kwa uzalendo ndani ya kiza kikubwa cha umaskini, tuliwapokea vijana wetu Kagera wakitokea Arua, wengine hawakurudi lakini kama Taifa la wazalendo tuliwaona ni mashujaa.
Nimeamua kuandika waraka huu kwa sababu kubwa mbili. Mosi, nchi yetu kwa sasa ina jeshi kubwa ambalo limefikia mahali tunaligawa na kuwapa wenzetu walioelemewa kimapigano. Pili, sioni haja ya kuwa na jeshi kubwa katika kipindi hiki ambacho hatuna viongozi sampuli ya yule jamaa wa Uganda, ambaye anaanzisha sokomoko wakati wowote.
Kwa maoni yangu ya kizee japokuwa si lazima yatiliwe mkazo na umuhimu, nilidhani jeshi letu la magwanda tulibadilishe liingie katika vita nyingine ambazo zipo na waanzishaji wapo na wanatakiwa wapate mvua za rasharasha kama zile za Uganda.
Wakati tukipata Uhuru, tulisema kuwa nchi yetu ina maadui watatu wakubwa, ambao ni ujinga, maradhi na umaskini. Hatukumtaja Idi Amin katika orodha ya maadui zetu. Nchi yetu kwa sasa imeongeza maadui zaidi ya hao tena ni hatari zaidi.
Sasa hivi tuna maadui hatari kama wala rushwa tulioshindwa kuwadhibiti kisheria, wanahitaji vita ya kijeshi kuwatokomeza, tuliowapa dhamana ni kama wanasiasa ambao wakichanganya na sheria mtuhumiwa anakuwa hana hatia na anaongezewa madaraka. Tuna wauza dawa za kulevya ambao bila kuumauma maneno Serikali imeshindwa kuwabana na kuwamaliza na matokeo yake watoto wetu wanamalizwa. Kazi hii kwanini wasipewe JWTZ hata kwa siku tano muone matokeo yake?
Maadui wanaoangamiza Taifa ni wengi kuliko tunavyodhani vichwani mwetu. Tuna wakandarasi ambao kazi yao kubwa ni kuchakachua majengo, barabara na kadhalika, na wanatazamwa kama wafalme huku wakiwa wamevuruga shughuli nzima na kuangamiza uchumi wetu.
Hii ni baadhi ya mifano. Katika waraka huu nilitaka kutoa ushauri kuwa jeshi letu libadilishiwe majukumu ikiwa ni pamoja na kuongezewa maadui ili wapigane nao, na ikitokea kukubaliana na hilo basi ule uzalendo wa kuchangia kwa hali na mali kama tulivyofanya mwaka 1978 na kuendelea, tutaufanya tena sababu ipo kwa kuwa ushindi utapatikana katika vita hizo.
Sekta zote zenye ubabaishaji wapewe vijana wetu wa JWTZ kama ujenzi wa shule, zahanati, barabara, ulindaji wanyamapori, uvuvi, viwanda, sayansi na teknolojia, utabibu, usalama barabarani, usalama wa nchi, ukusanyaji mapato, Mahakama na sheria kwa ujumla nchi iwe kama inaongozwa kijeshi lakini chini ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia.
Sioni haja ya kuwa na viongozi ambao muda mwingi wanatumia majukwaa kupiga kelele ya kisiasa na kutoa tahadhari badala ya kuchukua hatua kama ambavyo wanajeshi wanafanya, sioni haja ya kuwa na watawala ambao wanaona mambo yanaharibika kwa kiwango cha juu kabisa lakini wanashindwa kupata mahala pa kuanzia tu kwa sababu kuna sheria ambayo inawabana kuchukua hatua.
Tukiendelea kuliachia jeshi letu kubwa lisiwe na majukumu, matokeo yake ni mabaya na makubwa ikiwa ni pamoja na watumishi hao kulipwa bila kufanya kazi. Jeshi linatakiwa lifanye kazi, jeshi linatakiwa lipigane na umaskini pia lisiwe jeshi la kuvunja sheria, kubeba dawa za kulevya, nyara za Serikali, ugomvi na raia na usharobaro mitaani. Tutakuwa hatujawatendea haki.
Nakumbuka jeshi la uzalendo, uchapakazi, kujituma, kujitolea na vazi lao la heshima, hebu tuwape kazi tuone kama watashindwa kuifanya, kazi ambayo sisi tumeonesha wazi kwamba hatuiwezi na hatuhitaji kuwapa muda wa kujipanga kwa kuwa mfano waliuonesha mwaka ule walipoamrishwa na Julius na Moringe.
Aluta continua, mapambano yaanze sasa.
Wasalaam,
Mzee Zuzu
Kipatimo.