Wanangu mu hali gani, siku zote nawaandikia barua lakini siwaulizi hali zenu, mara zote huwaeleza siha yangu bila kujua siha zenu. Nimeona sitendi haki kwa kuwa kujua hali zenu ni jambo bora zaidi kuliko kuwafikishia ujumbe wangu, maana naweza kuwa nafikisha ujumbe katika uwanja wa makaburi ambako mmelazwa kutokana na ugumu wa maisha.

Niwape kongole wale wote wanaosoma waraka wangu na kunitumia ujumbe mfupi wa simu – iwe kunikosoa au kunipongeza – japokuwa wakosoaji wanaongeza maneno mazito sana katika waraka. Mimi niwaombe kuwa na subira katika maisha yote na maneno makali sana si suluhisho la jambo lolote, na ndiyo maana nimeamua kuwa mwanasiasa.


Wanangu, baada ya kutaka vyeo vyote, jana nimefikiria kuwa mbunge lakini nikagundua kuwa vigezo na masharti vinaweza vikanizuia kupata ubunge huo, na hata kama nikipendelewa kwa viti maalumu kutokana na kuwa kibogoyo, nitaishia kuchangia kwa maadishi ambayo hayasomwi kwa jamii na sitakuwa nimefikisha ujumbe kwa jamii bali kwa mhusika na jambo hilo (waziri).


Nimefikiria kuwa mbunge ili nisiwe mwanafamilia, mwanamtandao, mnafiki ili niwasaidie walionichagua, niwawakilishe kwa niaba yao, niyatafute maisha bora kwa walionichagua na si mimi niliyechaguliwa na nijijengee heshima ya siasa katika jamii.


Napenda kuwa mbunge huru ambaye sijatoka katika chama chochote ambacho naweza kuonekana mhuni, mwanamtandao, mkimbia hoja. Naweza nikaonekana mtetea hoja, mbunge wa watu, lengo langu litakuwa kuwaweka sawa wananchi wanaosikiliza maelezo yangu bungeni kutokana na ufinyu na udogo wa akili zao.


Nitapenda niwe mbunge ambaye sitataka niitwe mheshimiwa kwa lazima, ila nipewe jina la mheshimiwa na wale walionichagua  kutokana na heshima yangu kwao kwa kuwafanyia vizuri kazi niliyotumwa na jimbo langu.


Nitajisikia fahari sana kila nikishuka kwenye gari la kibunge na kupokewa na wananchi kwa jina la mheshimiwa, na mwisho nitakuwa mbunge pale ninapohudhuria vikao vyote vya bunge bila kukosa, isipokuwa tu maadhura yatakapokuwa yanahusisha maradhi.


Wanangu, leo nimeamua kusema naupenda ubunge ili niisimamie serikali ambayo ni taasisi kubwa sana inayohitaji usaidizi wa karibu kutoka katika chombo hiki. Sitapenda kuwa mbunge ninayelala au kuacha kuhudhuria vikao huku nikijua kuwa nina mtoto anayesimama dede na anahitaji jicho langu kwa usalama wake.


Naijua nchi yetu na mtindo wa siasa ambao upo baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi, mfumo ambao umetuaminisha kwamba kuwa nje ya chama kingine ni kuwa mpinzani na hupaswi  kuikosoa serikali ambayo nyote mnapaswa kuisimamia utekelezaji wake.


Wanangu, napenda kuwa mbunge ambaye sitakuwa mnafiki na nitamwogopa Mungu kwa kiapo ambacho nitaapa kusema kweli kwa faida ya wananchi. Serikali ni chombo kama vyombo vingine duniani ambavyo vinafanya makosa – yawe ya makusudi au bahati mbaya – na kwamba mkombozi mkubwa wa serikali yoyote ni bunge.


Kwa sasa nimefika mahali nimeridhia kuingia bungeni, kwenda kuisimamia serikali na kuwawakilisha wanajimbo kwa kusema kweli daima na uongo uwe mwiko kwangu, na kwamba tofauti ya vyama isimeze hoja ya msingi ya mbunge mwenzangu kwa manufaa ya taifa. Sitajisikia fahari kuona nakubaliana na kitu au jambo kutokana na mkumbo wa wengi wape.


Najua uzee ni kikwazo kikubwa kwangu kupata ubunge, lakini najua kuwa uzee ni dawa na hoja hujibiwa kwa hoja na si wengi wape, na matokeo ya kutotumia hoja tumeona katika mabunge mengi na hata maarufu ya mataifa yaliyoendelea kwa demokrasia, huamua kutumia nguvu na wakati mwingine hupageuza bungeni kuwa ulingo wa ndondi na si siasa.


Mwalimu wangu wa siasa wakati wa mkoloni ambaye alikuwa mzungu, aliwahi kunifundisha akisema maana ya siasa hasa ni ujanja wa kuwashawishi watu waweze kuishi kwa amani, kuwashawishi wakusikilize, wakuamini na kuwafanyia unalolitaka wewe.

Wanangu, napenda kuwa mbunge lakini sitaki kukubaliana na mwalimu wangu wa ukoloni. Nataka niheshimiwe kiukweli.

Mzee Zuzu,

Kipatimo.