Niwape pole wale wote waliopata maswahibu mabaya huko Kusini mwa Tanzania kwa sababu ya matatizo ya gesi, kama ni kweli, lakini nadhani hiyo ni propaganda ya watu wajanja katika kuhitimisha fikra zao za kujinufaisha zaidi badala ya utu kwanza.

Zamani tulikuwa tuna neno  linaitwa utu, neno au msamiati huo ulitafsiriwa vizuri sana katika kijitabu cha Azimio la Arusha kizamani, tofauti kabisa na maana ambayo leo naweza kusema inachukua maana nyingine ya kisasa kutokana na maendeleo.

 

Maneno mengi sana yanazidi kubadilika maana kama ilivyo kwa neno utu, yapo maneno kama unyonyaji, ubepari, utajiri, usawa, haki, ushirika, umoja, kujitegemea na mengine mengi sana, ukimuuliza rafiki yeyote wa Mzee Zuzu, atakuwa na maana tofauti kutokana na mtindo wa siasa na maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa.

 

Maneno haya pamoja na mengine yalikuwa na maana sana katika awamu yetu, awamu yetu ya kizamani, awamu yetu ya ujamaa na kujitegemea, awamu ya chetu sote na awamu ambayo ilikuwa ina mlengo wa kuleta maendeleo ya watu na nchi na siyo watu bila nchi.

 

Napata wakati mgumu sana kutaka kukubaliana na kile ambacho nakiona leo katika vyombo vya habari juu ya mvurugano wa amani ambao unatokana na rasilimali ya Watanzania wa Tanzania ambayo mipaka yake iliwekwa na mkoloni bila kujua kuwa analitenga eneo maalumu ambalo lingekuwa kisiwa cha amani.

 

Katika ukanda huu, enzi za ujana wetu ndilo lilikuwa eneo linaloheshimika kwa amani na kila aliyetaka amani alikuja hapa akajenga kambi ya mafunzo akajengewa uwezo wa kutafuta amani na akarudi kwao akiwa na misingi thabiti ya amani.

 

Waliochota hekima wamefanikiwa na leo wanaishi kwa amani hata kama hawakufuata utaratibu wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na vikorombwezo vyake vya Azimio la Arusha na utu wake. Wamefuata siasa za kimagharibi, utandawazi na uchumi huria.

 

Pamoja na mambo mengi ambayo yangeweza kudhibitiwa na utu tuliokuwa nao enzi hizo, utu uliokuwa katika Azimio la Arusha kwamba tuheshimiane katika misingi ya imani, siasa na ukabila, kwamba Tanzania ni moja na sisi ni wamoja, kulichopo Kaskazini ni cha Magharibi na kilichopo Mashariki ni cha Kusini.

 

Kwamba kwa utu wetu tuligawa rasilimali za nchi nzima kwa watu wake bila kujali ukanda, kabila, dini, jinsia na siasa na matokeo yake ni kuwa na huduma muhimu kwa jamii kwa kiwango cha juu kwa wakati huo kutokana na maendeleo tuliyokuwa nayo, elimu tulifanikiwa kwa utu, hali kadhalika suala la afya na miundombinu.

 

Tulikuwa na viwanda vingi vilivyotapakaa nchi nzima kabla ya utu wa uwekezaji kuvamia katika nchi yetu, tulikuwa na uongozi ambao ulikuwa unazingatia utu katika maamuzi yake, na wananchi tulikuwa na utu katika maamuzi yetu kwanza kabla ya kuchukua hatua ambayo haina utu.

 

Ni muda mrefu sasa mambo ya vurugu za kikanda, kikabila, kidini, kisiasa zinaendelea, na suala la utu limepewa kisogo ili tuone madhara ya kutokuwa na amani ambayo tumeijenga kwa miaka mingi na nguvu kubwa, jambo la msingi ni kukumbuka kuwa gharama tuliyotumia kuitafuta amani ni kubwa sana, ilitokana na utu tuliokuwa nao.

 

Kwa utu tuliokuwa nao, tulibatizwa na kupewa heshima kubwa eti Tanzania ni kisiwa cha amani pamoja na kwamba hatukuzungukwa na maji bali tulizungukwa na utu, mataifa yaliyokuwa na uvunjifu wa amani yalikimbilia Tanzania kuja kupata suluhisho la migogoro yao, leo utu ule umekwisha ukitaka kukosa amani basi uje Tanzania. Tanzania si kisiwa tena bali ni uwanja wa mapambano.

 

Napenda mabadiliko, hata yaje kwa kasi gani bora yawe mabadiliko ya kimaendeleo yenye utu, yazingatie maadili ya Mtanzania Yule wa kweli, Mtanzania mwenye uchungu na taifa lake, Mtanzania ambaye si kwa jina bali kwa vitendo, Mtanzania anayejua utu na kwamba kila mtu ni ndugu na tuishi kwa upendo.

 

Bila kuwa na utu, wazalendo wenye utu, viongozi wanaojua utu, na kuzingatia utu katika kila jambo, utu ule tuliokuwa tunausema wakati wa Azimio la Arusha, tutaimba nyimbo na kutoa hotuba zote lakini vurugu ipo palepale na cha moto tutakiona.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.