Nianze kwa kusali Kikristo: Baba yetu uliye mbinguni jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe kama yanavyotimizwa huko mbinguni, utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wanaotukosea, usitutie majaribuni…… ameni.

Mimi nilibatizwa kwa maji yaliyokuwa katika bakuli kubwa na kubarikiwa na kiongozi wa dini kama maji ya Baraka. Mtumishi aliyenibatiza nadhani aliitwa Kinyamagoha. Ilikuwa miaka ile ambapo ulikuwa ukisikia kanisa unaliogopa hata kudanganya mbele ya eneo hilo.

 

Namkumbuka kiongozi yule wa dini kwa sura na jina, na ilikuwa nikimuona barabarani nahisi kutubu dhambi zangu. Ni kama vile mitume walipokuwa wakikutana na Bwana Yesu na akawakazia macho, unahisi umeufungua moyo wako na kuziona dhambi zako zote.

 

Hii ilitokana na imani kubwa tuliokuwa nayo waumini wa dini mbalimbali duniani. Naamini bila dini duniani kusingekuwa na amani hata kidogo kwani ni kitu kinachotufanya tuishi kwa hofu ya Mungu. Hii ni kwa dini zote, dini kuu, matawi yake na sasa michepuo mipya ya dini inayotokea, yote bado inaamini juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu.

 

Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza wimbi kubwa la dini za watu wachache wenye ushawishi mkubwa katika jamii na kuwavuta waumini katika makanisa yenye msingi wa siku nyingi na kuwaaminisha kuwa huko ni kubaya. Uzuri wa dini hizi hazisemi kuwa Mungu hayupo bali zinamzungumzia Mungu katika sura nyingine mpya ya mapokeo.

 

Mimi nimezipokea dini hizi kwa kuwa zinatumia kitabu kile kile kikuu cha Mungu, na upande mwingine nazipenda kwa kuwa muda mwingi huzungumzia amani miongoni mwa wanadamu; amani na upendo ambao Mwenyezi Mungu aliutaka katika zile amri zake kumi alizomkabidhi mmoja wa mitume wake.

 

Maisha ni mitihani, hii ni lugha ya kiraia zaidi. Katika dini yoyote tunasema maisha ni majaribu na tunatakiwa kusimama katika imani na maombi ili tuweze kupishana na majaribu. Lakini katika maisha ya kiraia, mitihani haihitaji kusimama katika imani ila inataka kupigana na ugumu wa maisha  – iwe katika kufanya kazi ama kuongeza juhudi, na yote hayo katika uraia hayazungumzii amani na upendo, inaweza ikawa juhudi ya wizi au utapeli na kadhalika.

 

Leo nimeamua kuzungumzia katika dini moja tu ya Kikristo, ambayo imenifanya nisononeke kuona ina matawi mengi madogo, ambayo kimsingi yananipa hofu kubwa ya kuenea kwake sasa na siku zijazo kwa waumini kuaminishwa na sababu ndogondogo kutoka katika makanisa yao.

 

Nimeshuhudia makanisa ambayo sasa waumini wanasali katika makundi ya watu 10 au 20 na likiwa ndiyo tawi pekee duniani ambalo linajitegemea kwa katiba yake ya usajili kama kanisa. Nimeshuhudia waumini wakiaminishwa mambo ambayo hata katika historia ya dini ya Kikristo hayako, waumini kutakiwa kuleta watoto wao waombewe ili wafaulu mitihani yawezekana bila kusoma, kukamatwa, kukamatwa kwa wachawi, na ufufuo wa siku ya mwisho unaoweza kufanywa sasa bila Yesu Kristo kurudi kwa mara ya pili.

 

Ugumu wa maisha umewafanya waumini washindwe kuingia katika maombi ya kupishana na majaribu, sasa wanaweza kuaminishwa kwamba mtu fulani anaweza kumaliza matatizo yao kwa kukaa sebuleni na kufanya maombi makubwa ya muda mrefu na hatimaye matatizo yaishe.

 

Waumini wengi waliopotea wanakaa katika maombi huku wakiwa wamezitelekeza familia zao, wakiacha kufanya kazi na kuamini katika maombi ya kutatua matatizo waliyonayo bila kujua kuwa hayo ni majaribu yaliyopo. Wengi wanavunja ndoa, wanakosa kuwapa malezi watoto wao, wanakosa chakula, na kila wanachokipata wanakipeleka kwa kiongozi wao anayewafanyia maombi.

 

Viongozi wa makanisa ya Kikristo wamebaki kimya kwa sababu ya kushindwa kuingilia imani ya mtu, hata kama tunaona kabisa kondoo wa Mungu wanapotelea kondeni kwa imani haba. Nadhani sasa umefika wakati ambapo badala ya kuliombea amani taifa iwe kuwaombea walioingia katika mkondo wa imani haba kwa kuwa bila kuwatoa hao tunaweza kuliingiza taifa katika dhambi kubwa zaidi.

 

Mwenyezi Mungu ana vitu halisia, hana vitu vya kufikirika. Mwenyezi Mungu anawataka waumini wake wafanye kazi ndipo wale, wasikae wakitegemea kupewa chakula bila kufanya kazi. Mwenyezi Mungu alisema ikumbukeni siku ya bwana kuitakasa, hakusema siku zote msifanye kazi badala yake mkae mkizitakasa siku zangu. Alisema mtakula kwa jasho lenu na kila nafsi itaonja mauti, hakusema kuwa nafsi iliyoonja mauti itarejea kabla ya baragumu ya siku ya mwisho.

 

Wito wangu kama kweli viongozi wa dini ya Kikristo mnaweza mkachukua hatua dhidi ya Wakristo wanaorubuniwa na hao viongozi wapya wenye makanisa majumbani kwao, na kuwageuza waumini kuwa na imani ya kusali muda wote hata ule wa kufanya kazi, kuwa na familia, kulea watoto, kuamini katika utawala wa duniani, kuna kila sababu ya hili la makanisa kuangaliwa upya na mfumko wake ili ukemewe kwa nia nzuri ya amani.

 

Sisi Wakristo wa zamani bado tumesimama katika imani, naomba mtusaidie tusije tukaaminishwa kuwa hakuna kifo, kuna utajiri makanisani, kuna kurudisha mapenzi ya ndoa kwa maombi bila kufuata misingi ya ndoa za Kikristo, kuna ufufuo kabla ya Yesu, kuna kula kama bustani Eden bila kufanya kazi na kadhalika.


Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.