Mwisho wa makala iliyopita, nilisema nawafahamu waganga wa jadi ambao tukitaka kugangwa inatubidi tuwafuate. Kwa bahati mbaya yawezekana wakawa wametangulia mbele ya haki lakini bado kuna dawa walizoandika ama kuongea juu ya maradhi yetu, hebu tuige kabla hatujawa machizi wa kushinda jalalani.
Kuna shujaa mmoja wa zamani aliyesema: “Mtu mwenye busara anaweza kujifunza mengi kutokana na swali la kipumbavu kuliko mpumbavu anavyoweza kujifunza kutokana na jibu la busara.” Nahisi kuuliza maendeleo haya kwa swali la kipumbavu, wenye akili wanaweza kupata faida zaidi kuliko sisi walewale wapumbavu kwa majibu yao ya busara.
Leo naangalia tena maendeleo ambayo tunayataka kwa faida ya kizazi hiki na kijacho, kwamba kuwa katika mfumo wa vyama vingi ni maendeleo pia, na kuwa katika Bunge lenye mchanganyiko wa hoja zitokanazo na mfumo wa vyama vingi, ni kama kuleta ubishani wa kushikiliwa.
Maendeleo kwamba tunakuza misemo na methali za kunangana badala ya kufikiria maisha ya huyu Mtanzania anayeishi maisha ya kufikirika kila siku, kwamba hajui hata kesho yake itamkuta wapi, pengine katika moja ya majengo mawili ya bure ya Serikali ama mochwari au gerezani, haya ndiyo maendeleo tunayotaka!
Najua kuwa maendeleo yanakuja na maumivu yake kama kutumia akili sana, kuwa ‘busy’ sana, kwenda na wakati na mengineyo mengi sana, lakini swali la kipumbavu ni kwamba tunahitaji uwekezaji katika akili, u-busy, kwenda na wakati ama tunahitaji kujipanga upya?
Kuna wakati najiuliza maswali ya kipumbavu sana kuhusu viwanda vyetu vilivyokufa ilhali malighafi ipo hapa hapa nchini, na kwamba hiyo malighafi sasa tunaiuza nje tena kwa kupangiwa bei na hao wanaoitwa matajiri, ni nani aliyeturoga tukaamua kutambuka akili na kutua katika upumbavu?
Huwa najiuliza inakuwaje tunatumia fedha nyingi sana katika kampeni za uchaguzi ambazo haziwiani na hali yetu ya kiuchumi, badala ya kumteua mshindi wa pili katika uchaguzi uliopita na fedha hizo zikaenda katika shughuli za kijamii kama hospitali, shuleni na usafiri? Lakini ni maswali ya kipumbavu tu wala hayana umuhimu wowote kwa jamii yenye akili.
Pengine naweza nikajiuliza maswali mengine ya kipumbavu zaidi kwamba kwanini tuna jeshi kubwa katika nchi yenye amani kama Tanzania, kwamba umoja wetu tuliojenga kwa zaidi ya miaka 20 baada ya Uhuru sasa umekuwa uadui, tumeshindwa kuudumisha hadi tufikie mahali tunahitaji kuwekeza katika Jeshi la Polisi na kuilinda mipaka yetu?
Nahisi ni maswali ya kipumbavu kwa sababu wanaoiona tija wanakubaliana na wengi katika matumizi ya fedha katika Taifa hili changa kiuchumi baada ya miaka 50 ya kujitawala, na kujitafutia maendeleo na matokeo yake ni haya.
Sijui kwa dhati ya moyo wangu, nasema tena sijui labda malengo yao wale waliotafuta Uhuru ni tofauti na yetu watawala wa leo, watawala tunaoiona siasa kama kimbilio la wengi badala ya wataalamu, tunaoiona Tanzania katika kuchuma zaidi badala ya kuilinda na kuipenda, nchi yenye wenye moyo safi wenye hatihati, haya ni maswali yangu machache ya kipumbavu kwa wenye akili.
Naipenda Tanzania iliyokuwa na wataalamu wachache kabla ya Uhuru, ambao walifanya kazi kwa moyo wa kizalendo sana hadi tulipokuwa na wasomi wengi wenye hoja zinazokinzana kila siku na kuleta ukiritimba unaochelewesha na kuviza uchumi wetu, naipenda Tanzania iliyokuwa na amani, Tanzania isiyopandikizwa uadui, Tanzania ya chetu sote na Tanzania iliyokuwa na maendeleo ya kasi kabla ya hayo mambo yenu ya utandawazi.
Kama wako akina Mzee Zuzu wengine kama mimi, natushike mikono ya mshikamano tuseme inatosha kwa kizazi kipya kutuletea ukoloni mamboleo kwa sababu za kutaka maisha ya haraka na ya mkato. Kukopa si suluhisho, suluhisho ni kuzalisha kwa wingi na kuuza, kuwa na viwanda na kuajiri wazalendo, kuwasaidia wakulima na kuwa na soko imara, kutoa elimu bora kwa kila mwanafunzi na elimu ya kujitegemea na si ya kuajiriwa, huo ndiyo uliokuwa mpango kazi wa Mao Tsetung na Julius katika vita yao ya maeendeleo.
Kidumu chama chetu,
TANU oyeeee!
Mzee Zuzu,
Kipatimo.
Simu: 0759 784583