Kama lingekuwa ni genge halafu lipo mahali fulani mbali huko tungesema kuna ‘chuma ulete’ katika vichwa vyetu, yaani leo tunalala na hili ambalo halijaisha na kesho tunaamka na jambo jipya ambalo limebuniwa kututoa katika reli ya mambo ya jana, sisi ndio sisi.
Ukipata bahati ya kutembelea nchi zingine utasimuliwa juu ya raha ya kuishi hapa Tanzania, utaambiwa mambo mengi matamu ya nchi hii ambayo hata wewe labda huyajui, utaambiwa upole wa Watanzania na utaratibu walio nao, utaambiwa namna tunavyojua kushukuru hata pale tunapokosewa, kwa ufupi sisi tuna lugha tamu, ya upole na upendo.
Watanzania wanapenda kusikiliza hoja, hata kama hoja yenyewe ni mfu, Watanzania wanajua kusikiliza maneno kutoka kwa mtu na wakamwacha aongee mpaka amalize hata kama wanajua kwamba wanadanganywa, hii ndiyo sifa yetu katika macho ya mataifa mengine yaliyoshindikana, sifa ya kutozua tafrani kama wao inapotokea mambo yakakorogeka.
Watanzania tuna upendo uliopitiliza na hili halina mjadala kwamba lilipandwa kwa vizazi vingi japo upendo wa sasa ni haibridi, si ule tuliopanda sisi kwa maana ya uzalendo wa kweli. Uzalendo wa sasa unatia shaka kidogo kwa vile upo kwa sababu ya mapato, si uzalendo wa kufia nchi bila malipo.
Leo nimekumbuka mengi na kwa kweli mtaniwia radhi kwa kuanza kufikiria akili hii tunaitoa wapi? Akili ya kutofikiria jambo muhimu ambalo watu wengine katika mataifa mengine wanatoana ngeu kwa jambo hilohilo, hatujawahi kuwa siriasi kwa mambo ya msingi kabisa.
Siku kadhaa zilizopita tumepokea chanjo ya UVIKO – 19, wakati tukipokea chanjo hiyo ambayo kimsingi serikali italipa kwa namna moja ama nyingine, kuna watu wanakusanya watu mahali popote pale iwe kijiwe cha kahawa au darasani wanaanza kuwapigisha stori ambazo zinakinzana na juhudi za chanjo.
Watanzania wanaweza wakawa wanajua kabisa kwamba kuna corona na inaua watu na serikali imetoa tamko la kina juu ya chanjo na ushauri wa kitaalamu lakini Watanzania hawahawa wanatoa nafasi na masikio yao kwa mtu aliyeshindwa kufanya jambo lolote la maana katika jamii au aliyesema mambo mengi yaliyoshindwa kutekelezeka katika ngazi ya mtaa tu.
Wanakaa na kumsikiliza mtu ambaye hajui kwamba hajui na anaowasimulia hayo asiyoyajua nao hawajui kwamba hawajui kuwa hajui, wanaamini na kuaminishana kwa ushahidi wa papo kwa hapo, wanajisahaulisha mambo mengi nyuma ya corona kisa kuna kaulimbiu ambayo wameipenda.
Hili ni jambo moja tu kati ya mambo mengi ambayo kama sisi hutujawahi kuamua kufikiria kwa kina, serikali inaweza ikatoa fursa ya michango ya mawazo kwa wananchi lakini kila mmoja anakuwa na jambo lake nje ya angalizo tulilopewa, inapotokea kukawa na jambo limetokea katika jamii pamoja na maelezo yaliyokuwapo kabla tunaanza kulaani na kisha kusahau.
Mara nyingi sisi huwa hatupendi kusikiliza taarifa ya hali ya uchumi ambayo kimsingi ndiyo dira ya bajeti ya serikali, lakini sisi ndio wa kwanza kulaani bajeti iliyosomwa na hatukuisikia bali tumesimuliwa, sisi ndio wale wa kuamini katika kusikia na kuanza kulalamika kidogo kisha tunasahau.
Hebu tujiulize, ni mambo mangapi muhimu kwa mustakabali wa taifa na familia zetu tumewahi kuhoji, tujiulize tumehoji juu ya afya zetu?
Tumefuatilia masuala yahusuyo elimu kwa watoto wetu? Ni kweli kwamba tunajua jinsi maendeleo yanavyoletwa na kodi zetu au hatujui chochote? Tumechukua hatua gani?
Najua sijui lakini pia ninajua hamjui kwamba tunasimuliwa na wasiojua, tunajazwa akili na watu kwa masilahi yao, kama ingekuwa nchi nyingine labda mtu angeshitakiwa kwa makosa ya udanganyifu. Lakini katika muda tulionao naamini mambo mengi yatarudi katika vichwa vyetu na kuachana na ‘chuma ulete’ wa ubongo.
Tupunguze muda wetu kuambatana na wanafiki na waongo, tuongeze muda wa kuanza kuwasikiliza wataalamu wa kilimo kama kweli wapo, wataalamu wa uchumi kuhusu hali yetu na hali kadhalika katika masuala nyeti kama ya UVIKO-19 kwa mustakabali wa taifa na afya zetu.
Endeleeni lakini siku mambo yakifika ukingoni ndipo mtajua hamjui.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.