Wanangu, naamini mu bukheri wa afya na mnaendelea kufanya kazi kwa bidii kama tulivyokuwa tukifaya sisi wakati wa ujana na afya zetu.

Naamini hivyo kwa sababu taifa linahitaji nguvu yenu ili tuweze kutoka hapa tulipo na kuelekea kule ambako wenzetu wale tulioanza nao safari wameshafika, wakiwa na furaha tele ya matumaini waliyokuwanayo.

 

Nina furaha kwa sababu nyingi. Kwanza, katika kipindi hiki cha mgogoro wa serikali na madaktari mizimu yangu imenilinda sijapata kusikia dalili za homa wala kuhara damu, kama ilivyokuwa katika mgomo ule wa awali ambao alimanusra nipoteze maisha kwa kipindupindu. Najua mnajua kuwa mimi sina uwezo wa kununua maji safi ya kunywa na vyanzo vya maji safi vyote vina vimelea vya maradhi kwa sababu hamtunzi mazingira vizuri.

 

Kwa umri wangu sasa siwezi kupigana na kazi ambazo leo hii zinaleta kipato kwa mwanaume. Siwezi kupiga debe, kuuza bigijii, kuuza mitumba, kuokota makopo ya plastiki, kuwa dalali, kuuza vocha za simu, kuwa wakala wa fedha za simu, kuosha magari, kuwa mgambo wa city (jiji), kufanya dili, kuwa kuli tena bandarini, kuanzisha chama cha siasa na kazi nyingine ambazo hatukufundishwa katika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

 

Naweza kutoa ushauri tena nikiwa katika kigoda changu pembeni mwa kibanda cha mbavu za mbwa ambacho siku kikipambana tena na misukosuko ya mabomu au upepo mkali, lazima safari hii kikubali kushindwa kuhimili zahama kwa mara ya pili baada ya ile ya mabomu ya Mbagala na kisha ya Gongo la Mboto na mwisho upepo mkali na mvua kubwa ambayo kwa mara ya mwisho ilinyesha mwaka 1954.

 

Wanangu, kwa sasa ni mzima wa afya njema isipokuwa ulemavu wangu ni uzee, ambao kwa hakika hakuna anayeweza kuukana ulemavu huu kama hajaufikia kwa umri; ni ulemavu ambao kila mwenye kupata baraka ya Mwenyezi Mungu ya maisha marefu kama yangu akumbane na ulemavu huu tarajiwa.

 

Ubaya wa ulemavu huu ni kwamba huwezi kulazimisha kufanya jambo lolote linalohusu nguvu au akili ya kizazi cha dot.com kuweza kuhimili kuwa sawasawa kiuchumi kama walivyo watu wengine kwa umri wenu, ni ulemavu ambao serikali haitoi pensheni wala kujali tulichokifanya enzi zetu kwa manufaa ya kizazi hiki.

 

Leo najitahidi kuokota mbatata katika mashamba ya watu yaliyovunwa, lakini kwa kibali maalumu kutoka kwa mwenye shamba. Naokota mboga zilizotupwa kutoka kwa wauzaji ili niweze kupata kitoweo cha uhakika kwa siku. Navizia taarifa za msingi za taifa langu kupitia redio yangu ya 277 ambayo aghalabu wakati wa miziki ya kizazi chenu nazima ili niweze kutumia betri zangu za Kichina kwa muda mrefu kidogo.

 

Haya ndiyo maisha halisi ninayoishi hapa Kipatimo. Sina hofu wala shaka. Ninachojali kwa wakati huu ni kuona jinsi wanangu mnavyoweza kufikia umri wangu mkiwa mmeondokana na maradhi ya umasikini na mnafikiria kizazi kijacho kama ambavyo sisi tuliwafikiria ninyi na wanenu.

 

Jana jioni, kabla sijawaandikia barua hii leo asubuhi, kulipita kaupepo kidogo mbele ya nyumba yangu, naamini kilikuwa kitu kama kimbunga kidogo ambacho kilisafirisha kipande cha gazeti ambacho nadhani kilifungiwa vyakula kutokana na harufu yake. Kwa tamaa yangu ya kutopitwa na maandishi nilikiokota na kukisoma.

 

Sina hakika ni gazeti gani, lakini niliokota ukurasa ambao nadhani ni wa barua za wasomaji. Nilitulia kigodani ili nisome yanayowasibu wengine. Kwa hakika barua ya kwanza tu ilinifanya nisisimke kwa mshangao wa hao wanaoitwa viongozi kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika.

 

Nilijiuliza maswali mengi. Hii inatokana na udot.com au ni kuchoka kwa hao wanaoitwa watumishi wa umma wenu? Katika ukurasa huo kulikuwa na barua kumi zilizoandikwa kwa ufupi, lakini kwa nia ya dhati inayokera kwao.

 

Barua zote zilinigusa, lakini niliona ni vema nikagusia barua ya wafanyakazi wa hoteli moja huko jijini Dar es Salaam wanaodai kunyanyaswa na mwajiri ambaye ni mgeni katika taifa hili. Nilijiuliza maswali machache, la kwanza ni kwamba hivi ule Uhuru tulioutafuta tumeshauzika au tumeshaubinafsisha?

 

Hili limekuwa ni tatizo kila kukicha katika vyombo vyetu vya habari na utendaji mdogo wa kuchukua hatua wa dot.com. Nchi tuliyowakabidhi tulikuwa tukipinga sana suala la ubaguzi, kila aliyebagua mtu kwa rangi yake, kabila lake, ukanda wake, dini yake na mengine mengi tulimuona ni kaburu.

 

Kaburu hatukumkubali katika taifa letu kwa matendo yake. Tulijua ni mbaguzi wa watu wetu; watu ambao tumewalea katika hali ya kujivunia utaifa wao na haki ya msingi ya kumiliki sheria na wajibu kwa taifa lake. Tuliheshimu suala la uraia na sifa zake na tulidhani kila Mtanzania ana haki ya kuishi kwa amani katika taifa hili.

 

Malalamiko yaliyotolewa na wafanyakazi wa hoteli hiyo, yalitolewa kwa  niaba ya wafanyakazi wa hoteli nyingi, migodi na kampuni ambazo zinamilikiwa na wageni katika ardhi ya Tanzania, lakini kukiwa na tatizo kubwa la kubaguliwa kwa Watanzania wenyewe.

 

Matatizo haya yanafanyika kila siku na msimamizi mkuu wa kuweza kudhibiti haya ni serikali kupitia vyombo vyake vya dola vyenye mamlaka ya kisheria kujua kila yanayotokea kwa hao wanaoitwa wawekezaji. Haiwezekani Mtanzania abaguliwe kwa rangi yake ndani ya taifa lake.

 

Nimesoma barua hiyo nikaanza kujiuliza hivi hawa wageni wanaokuja kufanya kazi hapa nchini, vibali wanapata wapi? Huko wanakotoa vibali wanajua masharti na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa na hao waombaji kazi kutoka nje? Wanaujua utamaduni wa Mtanzania katika kuheshimiana, na wanajua vigezo vya kuwapa vibali vya kazi?

 

Lakini swali jingine najiuliza, vyama vya wafanyakazi viko wapi katika kutetea haki za wafanyakazi na ni kazi gani tunazohitaji kuwa na mtu maalumu kutoka nje ya nchi ambayo hatuna Mtanzania anayeweza kuifanya? Hatuna manyapara wa Kitanzania, hatuna wauzaji wa bidhaa za kawaida hapa Tanzania?

 

Tulipotaka Uhuru tulimaanisha kujitegemea na kuweza kufanya kazi zote. Hatukumaanisha uhuru wa bendera, umefika wakati ambako mimi nikiwa kama mzee mbashiri naona madhara mengine yanayokuja mbele kutokana na vyombo vyetu vinavyohusika kuacha mwanya katika kuzingatia vigezo vya ajira za kigeni.

 

Nina wasiwasi kuwa iko siku Watanzania watasema sasa inatosha, na kupandikiza uadui na mataifa ya nje ambayo kwa namna moja au nyingine, ndiyo wafadhili wetu wakubwa wa masuala ya kimaendeleo. Tufike mahali tuseme inatosha hawa Watanzania wanaolalamika kunyanyaswa wanasikilizwa kwa kina kabla hawajachukua hatua mikononi.

 

Vyombo vinavyohusika viwasikilize, vinginevyo ule wimbo wa “kaburu matata chinja” utafanywa kwa vitendo. Tanzania ninayoijua mimi tuliwakataa sana makaburu, sina hakika Tanzania yenu kama mmeamua kuwakumbatia na kama ndivyo, basi nguvu ya maji inakuja – tengeni mabeseni kuzuia mafuriko mnayoyatafuta kwa gharama nafuu.

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu- Kidumu chama cha TANU,

Kipatimo.