Nashukuru kwa kuwa Bunge letu sisi lilikuwa pale Dar es Salaam, Karimjee na pia hakuna vikinga hatari kama vilivyopo katika Bunge lenu la pale Dodoma, na wakati ule idadi ya wabunge ilikuwa ndogo, kiasi cha 72 tu, waliochaguliwa kwa jembe na nyumba.
Sina hakika, lakini vijana wa dotcom wanaliita Bunge lile kama ni la ‘ndiyo mzee’ kwa mujibu wa hiyo inayoitwa demokrasia wakati huu wa utandawazi. Wabunge wetu walikuwa wanawakilisha nchi na majimbo yao, kulikuwa hakuna wabunge wanaowakilisha majimbo na vyama vya siasa wakasahau nchi.
Nayapenda maendeleo, tena napenda yaje kwa haraka sana, lakini sipendi maendeleo yanayobadilisha utamaduni wetu na kuendeleza utamaduni mpya kwa kizazi kijacho, ambacho hatujui Bunge lao litakuwa wapi na maadili ya wabunge yatakuwa vipi.
Mimi ni mzee sasa, lakini sitaki kumlaumu yeyote kati ya hao waheshimiwa. Tatizo langu ni moja ambalo kimsingi nilidhani ni busara ndiyo inayotakiwa kumaliza mzozo, ambao kimsingi si wa wabunge peke yao isipokuwa ni mzozo kati ya wabunge, wananchi, nchi yetu, Serikali yetu na kizazi kijacho.
Ni Bunge letu ndilo lililokubaliana kuwa na mfumo wa vyama vingi, lilikubali kuwa na hao wanaoitwa wabunge wapinzani na si wabunge wa vyama vingine vya siasa kama wanavyojulikana katika nchi nyingine. Uamuzi wa kuwa na vyama vingi mimi sikuupenda sana kwa sababu moja kubwa ya mazoea ya chama kimoja cha TANU.
Vikaanzishwa vyama utitiri vya siasa, vingine vikafia njiani, tukawa na wenyeviti wengi wa vyama sanjari na mwenyekiti wa chama chetu tawala, nao wakawa na mbwembwe kama za viongozi wa kitaifa. Kwa dhana hiyo chama tawala kikawachukia na kuwaona ni wapinzani kutokana na kosa dogo la wachache kulewa madaraka ya uenyekiti wa vyama vyao.
Baadhi ya vyama vikapata wabunge kutoka katika majimbo kadhaa nao wakaonekana kama wakorofi kwa kupinga kila kitu kinachoendelea bungeni, kwa hoja kwamba wanawatetea wananchi. Zipo hoja zilizokubalika na zipo zilizokataliwa kulingana na uzito wake.
Bunge limeendelea na awamu zikaongezeka na idadi ya wabunge wa upinzani ikaongezeka, wengine wakiwa wamemeguka kutoka katika chama tawala. Hoja zikawa zinajengwa na baadhi zikawa zinakubaliwa na nyingine zinakataliwa, hatukudhani kwamba hoja zitakuwa zikihusisha nguvu ya mwili, nilidhani hoja zitajengwa kwa mujibu wa taratibu na kusikilizwa.
Kanuni za Bunge lenu sizijui, lakini kama mwananchi tena mzee naweza nikashauri kwamba ziwe zinatoa fursa ya kumsikiliza mbunge ambaye anasimama na kuzungumza. Kuzomea hakumaanishi anayetoa hoja ni mjinga, la hasha. Wananchi tunawapima wabunge wetu kwa hoja zao.
Zipo hoja zilizotolewa, mathalani hoja ya maji katika mji mkubwa kama Dar es Salaam, hoja ya mtaala wa elimu Tanzania, hoja ya mikataba ya madini — zote hizi ni hoja ambazo kimsingi ni za kitaifa na wala hazimnufaishi mwanachama wa chama chochote cha siasa isipokuwa Taifa la Tanzania.
Mlolongo wa matukio yaliyopo katika jengo hilo la Bunge Dodoma usichukuliwe kama utovu wa nidhamu, uchukuliwe kama kutoelewana katika hoja. Siuoni ujinga wa mbunge yeyote, ambaye alipenda hoja yake isikilizwe lakini haijapata mashiko kutoka kwa waheshimiwa wengine.
Nguvu iliyotumika ya Jeshi la Polisi na picha zilizoonekana mitaani ni kashfa kwa Bunge letu. Na ili kupunguza idadi ya wabunge wakorofi kwa mujibu wa ajenda yenu mpya ya upinzani, nilidhani ni vyema mkawaacha waseme hicho mnachokiita pumba zao ili sisi tuwachekeche katika uchaguzi ujao kwa pumba zao.
Sisi wapigakura tumegeuka kuwa vichaa maana wawakilishi wetu kuna wakati hawasikilizwi na badala yake wanaambiwa wakae chini, hatujui wanataka kuzungumza nini, inawezekana ni jambo la kijinga, hilo kwetu sisi litatusaidia kujua kama mbunge wetu anastahili kupewa kura tena kipindi kijacho.
Kanuni na sheria za Bunge sisi hatuzijui, tunachokijua ni jinsi gani mbunge anatakiwa kudai kutoka serikalini, kile ambacho tulimwagiza kutokana na kupungukiwa katika eneo letu. Jinsi gani anawasilisha kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za Bunge kwetu sisi ni kitu kigeni tusichokijua. Wengi wetu tunaona kama wanaonewa baadhi ya wabunge wa upinzani na hata baadhi ya wale wa chama tawala.
Kuna lawama nyingi zinapelekwa katika kiti cha mkuu wa Bunge, lakini mzazi ningeshauri kila mtu anayetaka kuzungumza apewe nafasi azungumze — iwe ni pumba sisi tutamchekecha na kuamua kipindi kijacho tumpe nani nafasi hiyo.
Kwa hali ilivyo sasa hivi, ningeshauri Bunge lenu liendelee kuoneshwa ‘live’ katika televisheni na kusikika katika redio ili sisi tuendelee kujua nani anafanya nini kwa faida ya nani, na nani anamkataza nani kwa faida ya nani, na nani anazungumza pumba kwa faida ya Taifa letu.
Mwisho ningesema hivi, wabunge kutoka vyama vingine vya siasa si wapinzani wa kugombana nao, na wabunge wa chama tawala si wafalme wa kuwaona wenzao ni makaburu. Hali kadhalika, wabunge wa vyama vingine vya siasa wasiwachukulie wabunge wenzao kama hawawakilishi wananchi, tunachohitaji ni hoja za msingi na si kuambiwa kaa chini.
Chonde tukumbuke Bunge la Karimjee lilikuwaje, na hili likoje na lijalo litakuwaje? Nachelea kusema kuna siku mtu ataingia bungeni na kisu au helmet kwa ajili ya kujihami, tusifikie hapo wanangu, huu ni wosia wangu.
Mzee Zuzu
Kipatimo.