Kama wiki moja hivi imepita tangu nipitiwe na usingizi mzito kama ule wa kutolewa ubavu mmoja ili kumuumba mwanadamu mwenzangu uliponikumba katika mazingira ya ajabu, ningeweza kujiita majina ya ajabu ambayo wengine wamejibatiza huku wakijua hawakupata nafasi ya kuota kama mimi bali wao ni usingizi wa maruweruwe tu ndio wameugeuza kuwa njozi za neema kwa wakosaji na watenda dhambi.
Niliota ndoto ya kupokea barua kutoka kuzimu, sikumbuki niliichukua wapi, lakini ninakumbuka nilikuwa nayo mkononi nikiisoma kuanzia aya ya kwanza mpaka ya mwisho. Barua hiyo haikuwa na huruma na mimi, niliona ni kama ninahukumiwa moja kwa moja kuwaletea ujumbe ule wasomaji wetu. Ninaweza kusema jinsi ambavyo iliandikwa, lakini ningependa ninukuu zaidi kama nilivyoipokea.
Naanza kunukuu kama ifuatavyo: “Habari za leo Mtanganyika mwenzetu uliyebaki huko, sisi tuko huku na wenzetu waliokuja zamani na siku za hivi karibuni. Tunawaangalia kwa macho yote lakini tunajitahidi kupiga kelele mtusikie. Naona kama sauti haifiki, nimeamua kuandika barua kwa niaba ya wenzangu wote tulioko huku pamoja na Julius. Ipokee, isome kisha fikisha ujumbe wetu kwa Watanganyika wenzako.
Mimi si Julius, lakini mawazo yangu na yake yanaweza kushabihiana japo namna ya kuwasilisha tunaweza kutofautiana. Yapo mambo tunayapenda sana, waambie wenzako kama kuna jambo linatufurahisha, basi ni umoja na mshikamano ambao mnao mpaka leo.
Kuna wenzetu huku wa mataifa mengine wanalia sana jinsi wanavyowaona vijana wao waliowaacha wanavyofanya. Mandela analia sana, kila siku tunamfuta machozi, tunamuuliza kuna nini huko kwake? Anatujibu kwa ufupi tu kwamba: “Watu wangu hawana shukurani, wanatafunana na Waafrika wenzao.”
Sisi tunaona mambo mengine, haya ya kuumizana tunayaona japo ni mabaya lakini hayatokani na ubaguzi, ni tabia tu za wenzenu wachache ambao wamekosa mafunzo ya uzalendo ambayo mlifuta wakati mkiondoa mafunzo ya JKT mkidhani mmeamua jambo jema.
Waambie wenzako kwamba hilo ni kosa kubwa, jipimeni na kuona faida na hasara ya mafunzo yale kwa maana ya uzalendo na ajira binafsi. Kuna mahali mnakwama, hamjajitambua kuwa ni kuondoa mafunzo ya JKT.
Tupo huku tunawaona kwa hisia zenu kwamba kila mtu ana jambo lake hata kama ni la kimaendeleo, lakini kwa kuwa sisi tunawaona ndani ya mioyo yenu, tunagundua hila na nia mbaya ya kujinufaisha mtu mmoja mmoja badala ya taifa, tunawaona wanafiki wote na jinsi wanavyokaa vikao vyao vya kudhulumu taifa katika mipango ya mikataba.
Tunawaona wanaotoa rushwa kununua haki na wanaotoa rushwa kupotosha haki, waambie wenzio haki ni jambo muhimu sana, haiuzwi wala kununuliwa. Wanaosimamia suala la kidhibiti rushwa waangalie sana wasiwe miongoni ili waweze kudhibiti.
Wape salamu walimu wote, hasa wale wa ngazi ya awali. Waambie tunawakumbuka sana, juhudi zao ndizo zinazozaa wataalamu wa kila nyanja. Kupitia wao mnapata wanataaluma wa ngazi zote hadi wahudumu wa chini.
Ni kazi ngumu lakini wengi wao ukifunua mioyo yao ni kazi ya wito kuliko mnavyodhani. Wakumbushe wenzio msiwasahau walimu wanaowafundisha kusoma na kuandika, mnajiongezea laana msiyoijua.
Hii barua itakuchosha lakini tafadhali soma yote na fikisha ujumbe kama ulivyoandikwa ili siku moja barua yetu ikumbukwe. Waambie viongozi kuwa uongozi ni karama. Pia kiongozi yuko nyuma ya wananchi.
Tunawaona viongozi walio mbele na wananchi walio nyuma. Huu haukuwa utaratibu wetu wakati tukipata uhuru. Waulize viongozi wa mifano, mbona ni wachache sana? Na kwanini wengi wao wakiteuliwa wanasahau ni kwa ajili gani waliteuliwa?
Waambie wenzio maendeleo hayaletwi kwa wingi wa maneno, yanaletwa kwa kufanya kazi. Sasa kwanini wafanyakazi ni wachache sana na wanasiasa ni wengi? Kwani ule utamaduni tulioacha wa siasa ni kazi siku hizi mmeufanya nini mpaka uongozi umekuwa kazi? Tunaona wanavyosherehekea wanapoteuliwa ni kama vile wamepata machimbo ya dhahabu, wakemee.
Wafikishie taarifa kwamba, taifa letu lilitakiwa kuwa taifa tajiri zaidi Afrika lakini kutokana na tamaa zao wanazidi kuliangusha taifa hata kama mnaishi kwa amani kuliko huko kwa mwenzetu Mandela anayelia kila uchao.” Kwa leo mwisho wa kunukuu.
Nitaendelea sehemu ya pili.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.