Nimefarijika kusikia bajeti ikisomwa na waziri wa Wizara ya Fedha anayesifika kwa misimamo ya uzalendo. Ni bajeti ya kwanza kabisa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoakisi utendaji kazi wa awamu ya tano kwa kaulimbiu ya ‘hapa kazi tu’ ya Mheshimiwa Rais JPM.

Matarajio ya wengi katika bajeti hiyo yalikuwa tofauti sana na tulivyosikia. Kuna sababu nyingi za kuelewa tofauti, kwanza siye akina Zuzu tulitarajia kusikia kupanda kwa gharama za vitu kwa majina, tulitarajia kusikia kodi ikiongezwa katika vitu vinavyotajwa hadharani. Imekuwa kinyume, imesomwa kisomi kiasi cha kutuvuruga tusijue nini kilichozungumzwa lakini tunawaona wasomi wakijaribu kudadavua wanavyoelewa.

Akina Zuzu tunajua mifuko ya Rambo imepigwa marufuku, haitatumika tena, mafuta hayajapanda bei kwa hiyo nauli haitaongezeka kwa mwaka ujao, yapo tunayoyajua kidogo kama ilivyoamuliwa kuwa mapato yote sasa ya Serikali yanatakiwa yaende Hazina ndipo yaombwe tena kwa matumizi. Haya yote yako vizuri, tatizo langu ni uwahishaji wa mafungu hayo ambayo kimsingi yanadhibitiwa kwa manufaa yetu.

Jambo jingine tulilolisikia ambalo halijatajwa kisomi ni uanzishwaji wa Mahakama ya mafisadi, tumeshangilia japokuwa inawezekana mchakato ukachukua muda mrefu na kutufanya tusahau ile dhana ya kuwashughukia mafisadi, ambayo tumekuwa nayo kichwani tangu wakati wa kampeni ya mheshimiwa.

Tukasikia pia kuwa yale magari ya watu maarufu ambayo yalikuwa yakiandikwa majina yao badala ya namba kuongezewa tozo kwa mwaka, nalikubali japokuwa hofu yangu kwa hali ilivyo sasa nachelea kusema wengi wao watarudia kwenye namba za kawaida, ule ujanja wa kupata bila jasho naona umefikia ukomo, hapo pato la Serikali litatoka wapi?

Akili zetu akina Zuzu zilituama pale tuliposikia waziri akisema kuna kodi ambazo zinapaswa kuingia au kuongezeka, ikiwamo ya mikopo ya benki, ushuru wa gesi na mahamisho ya miamala ya fedha katika simu zetu. Sasa itabidi tuchape mwendo kupelekeana fedha mambo ya simu ni mwiba mwingine.

Haya ni baadhi ya maono ya akina Zuzu katika bajeti ambayo ilisomwa kisomi na kutuacha wengi wetu tusijue kinachomaanishwa labda mpaka mwezi wa saba tutaanza kuona mabadiliko na kuelewa kilichokuwa kikizungumzwa.

Pamoja na kutokuwa na usomi unaoweza kutufanya tusielewe mambo kwa undani, kuna taarifa ambazo hatukuzisikia kama masuala ya madini yanayochimbwa hapa nchini, hatukusikia suala la kodi ya madini labda kama lilitamkwa kisayansi zaidi, macho yetu yalikuwa katika machimbo makubwa ambayo yanatufanya tuone ni Taifa linalopunjwa kila siku. 

Tulitarajia kusikia kodi na mipango thabiti ya kusimamia madini yetu, upitiwaji mpya wa mikataba ya uchimbaji na usafirishaji, masuala ya utalii na vitalu ili kuongeza tija na wateja katika mbuga zetu, gesi na misamaha ya kodi kwa matumizi ya ndani ili kupunguza matumizi ya kuni huku vijijini kwetu na kutufanya kuwa Taifa la kulinda misitu.

Tulitarajia kusikia mipango mikubwa kwa watumishi wa umma baada ya kupunguza wale watumishi hewa na majipu, kwamba katika bajeti ijayo kuanzia mwezi wa saba basi kungekuwapo na afua ya ugatuaji malipo mazuri kwa watumishi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Tulitarajia katika bajeti hii kusikia huduma za jamii zikiimarishwa sana kwa kuwa ni kilio cha muda wote kwa wananchi wa kawaida, huduma za afya, huduma za elimu, huduma za mawasiliano, huduma za maji, umeme na bidhaa maalumu muhimu.

Tulitarajia kusikia suala la rushwa likiwa ni ajenda pekee katika miaka mitano ijayo siyo kwa kuongeza bajeti yao bali kwa kuboresha utendaji kazi wa kudhibiti na kuipoteza rushwa, ifike mahali kusiwepo harufu na hata dalili za kuombwa rushwa. 

Hii ni hotuba ya mwanzo kati ya hotuba tano za awamu hii ya ‘hapa kazi tu’, nina imani inaweza ikakidhi haja kwa siku zijazo kwa kuwa siyo rahisi kufanya kila kitu kwa mwaka mmoja tu. Hata hivyo, ninashauri kwa lile ambalo linakera na halijaweza kuwekwa katika hotuba ya bajeti haimuzuii waziri kufanya marekebisho wakati atakapoona inafaa. 

 

Wassalaam

Mzee Zuzu

Kipatimo