Wanangu, leo ni Jumanne nyingine ambayo kwa uhakika imenifanya nikumbuke mambo mengi sana. Mojawapo ni yale maneno yaliyozungumzwa na Mwenyekiti wa TANU pale Mwanza Oktoba 17, 1967. Alizungumzia utekelezaji wa Azimio la Arusha.
Naomba ninukuu sehemu ya hotuba yake. “Mambo mengi yametokea tangu tulipokutana katika mkutano uliopita. Kazi ya mkutano huu sasa ni kuyafikiria mambo hayo katika shabaha tulizojiwekea tulipolikubali Azimio la Arusha.
Maana tulipolikubali Azimio tulikuwa tunakubali kuweka misingi ya Ujamaa na Kujitegemea. Azimio lenyewe halikuleta Ujamaa wala Kujitegemea; tutafikia lengo hilo la Ujamaa na Kujitegemea kama tutatumia busara yetu na kufanya kazi kwa juhudi. Ni jambo muhimu kuelewa barabara jambo hilo.
Azimio la Arusha halikuleta miujiza. Halikutuongezea watu wala kuwafanya wawe na elimu zaidi. Halikubadilisha mawazo yetu tuliyolelewa nayo wala kutubadili hali yetu kwa muujiza.
“Kulikubali kwetu Azimio la Arusha ni sawa na kijana wa Kikristo kupata kipaimara, au kijana wa Kiislamu kusilimishwa. Ni ahadi ya dhamiri ya kuishi maisha ya namna fulani na kutenda vitendo vya aina fulani kwa sababu ya makusudio fulani. Hawi Mkristo mwema, au Mwislamu mwema, kwa sababu tu ameahidi kuwa mwema. Na sisi kadhalika.
Hatujawa nchi ya Ujamaa kwa sababu tu tumeazimia kuwa nchi ya Ujamaa. Kweli kuamua na kuahidi ni jambo la maana. Lakini jambo la maana zaidi ni vile vitendo vitakavyofuata baada ya ahadi ile. Kwa hiyo swali tunalojiuliza sasa ni kama tumeanza kufikiria mambo yafaayo, au kupanga mipango ifaayo, au kutenda vitendo ambavyo hatimaye vitajenga Ujamaa na Kujitegemea katika Tanzania.
“Kwanza tuanze na Kujitegemea, maana naamini kuwa wengi wamelielewa vibaya jambo hili, hasa sisi kuliko hata watu wengine. Baadhi ya watu wetu wameeleza, na kufanya vitendo, wakifikiri kwamba Kujitegemea tusemako maana yake ni kujitosheleza kwa wataalamu na mapesa. Hiyo siyo maana yake.
Tutakuwa wajinga sana tukifikiria kwamba Azimio la Arusha limetufanya ghafla tuwe na madaktari zaidi waliohitimu, au walimu zaidi, au mainjinia, au makatibu, au watumishi wa aina nyingine, hata shabaha ya Mpango wetu wa Miaka Mitano ya kujitosheleza kwa wataalamu wetu wenyewe mnamo mwaka 1980 ghafla ikaonekana haina maana.
Maana ya Kujitegemea siyo hiyo, maana Kujitegemea siyo kitu cha kipumbavu. Hebu sasa tufikiri barabara tunaratajia kupata nini, na siasa ya Kujitegemea ina maana gani katika miaka michache ijayo, na tafsiri gani ya siasa hiyo si sawa.
“Kwanza, kujitegemea maana yake ni kwamba hatuna budi kutumia kwa juhudi zetu zote rasilimali yetu tuliyo nayo. Tunataka raia wapewe nafasi katika kila kazi mara tu watakapomudu kufanya kazi hiyo barabara. Na hasa uamuzi juu ya mambo yote ya kuendesha nchi hii hauna budi kufanywa na Watanzania; nchi yetu haina budi kuendeshwa na Watanzania wenyewe. Lakini kwa sasa hilo si jambo kubwa, maana tumekwisha fikia hali hiyo. Swali la kujiuliza ni kama lazima tuwe na raia wa Tanzania watupu katika kila kazi ya kutimiza mipango ya wananchi, hata kama wananchi hao hawazimudu kazi hizo.
“Wakati tukitoa jibu la swali hilo hatuna budi kufikiria hali yetu ilivyo, kama kweli tunataka kutimiza shabaha zetu. Maana kweli yenyewe ni kwamba hatuna bado Watanzania wa kutosha wenye ujuzi unaotakiwa na kufanya kazi zote zitakiwazo kufanywa, kutimiza mipango ambayo sisi Watanzania tumeamua itimizwe.
“Sasa basi tujiulize kama tu radhi kuacha mipango yetu isubiri kwanza mpaka tumewaelimisha na kuwafunza Watanzania kufanya kila kazi itakiwayo kufanywa. Na toka zamani tumeamua kuwa kusubiri si lazima, na kwa kweli ni ujinga. Bwana Fedha ni Bwana Fedha tu, awe raia au si raia; kadhalika daktari ni daktari tu, na meneja ni meneja tu, ama anaiweza kazi yake ama haiwezi.
“Jambo kubwa tunalopaswa kufikiria juu ya watu hawa, wawe raia au si raia, ni kama wataweza, kwa utii na uhodari wao kutimiza mipango inayowekwa na serikali yetu na watu wetu.
“Kumwajiri mtu asiye hodari, kwa sababu tu ni Mtanzania, ambapo kazi yenyewe inayotakiwa kufanywa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, siyo Kujitegemea ni upumbavu. Kama wewe au watoto wako wakiugua, haja yetu ya kwanza ni kumpata daktari hodari, si lazima awe raia. Tunapoamua kujenga daraja, tuna haja ya injinia hodari, ambaye atahakikisha kwamba daraja hilo litakuwa salama na litafaa kwa kazi inayotakiwa.
“Maswali tunayopaswa kujiuliza ni kama haya. Kwanza: Je, kazi hii ni muhimu kwa mipango yetu? Pili: Je, tunaye Mtanzania mwenye ujuzi na mazoezi ya kutosha kufanya kazi hiyo? Na tatu: Kama hakuna Mtanzania mwenye ujuzi huo, tunaweza kumpata mtumishi mwenye ujuzi, japo asiyekuwa Mtanzania, ambaye tutamtarajia atufanyie kazi yetu kwa utii na uhodari? Na mwisho: Je, tuna mipango gani ya kuwafunza Watanzania ili hatimaye wafanye kazi hizi?
“Na hapo tutakapoamua kwamba kazi hiyo ni muhimu, na kuona kwamba hakuna Mtanzania anayeiweza, ila mtumishi asiye Mtanzania anaweza kupatikana, basi tumwajiri mtumishi huyo atufanyie kazi yetu ya kujenga daraja. Tukifanya hivi tutakuwa tumesonga mbele katika shabaha ya Kujitegemea. Kwa mfano kwa kujengwa daraja lile kijiji cha mbali kinaweza Kujitegemea kwa sababu sasa kinaweza kuuza mazao yake yaliyo mengi zaidi, na kuinua hali ya wananchi wa pale.
“Tungesema tungoje tusijenge daraja hilo, kwa sababu tu hakuna Mtanzania mwenye ufundi huo, basi kijiji hicho kitabaki katika hali ya chini, bila ya uwezekano wa kufikia hali ya Kujitegemea au maendeleo yoyote.
“Lakini katika nchi hii kuna jambo la pili tunalolipenda watumishi wetu wawe nalo. Kwa kweli tunataka watumishi wenye mawazo ya Ujamaa katika kila kazi. Kusema hivi maana yake si sawa siku zote na kusema tuna haja ya Mtanzania katika kila kazi, maana si Watanzania wote wenye mawazo ya Ujamaa.
Lakini kama daktari hodari pia ana mawazo ya Ujamaa, basi mtu huyo atatufaa sana sisi. Na kwa kweli ni kwamba jina la Tanzania katika nchi za nje ni kubwa mno hata watu wengi wenye mawazo ya Ki-ujamaa kutoka nchi za nje wanatamani sana kuja kufanya kazi nasi.
“Labda katika siku zijazo Watanzania wenye mawazo ya Ujamaa wataweza kusaidia wajamaa wa nchi nyingine kutimiza mipango yao. Lakini kwa sasa yatupasa tuwe tayari na radhi kuwakaribisha wasoshalisti wanaotoka nchi zingine walio tayari kutusaidia katika juhudi ya kufikia lengo letu.
Pia tukumbuke kwamba wasoshalisti wengi wanatoka katika nchi za kibepari; wakati mwingine wanakuwa na shauku kufanya kazi nasi kwa sababu hawawezi kuutumia usoshalisti wao katika nchi zao wenyewe”.
Mwisho wa kunukuu.
Wanangu, swali pekee ninalotaka kuwauliza ni kwamba hawa washoshalisti tulionao leo ni wale wajamaa wa kweli waliotoka katika nchi za kibepari? Na je, umuhimu wa kumpa kazi Mtanzania asiyeweza kazi hiyo, bali kwa sababu ni Mtanzania mnaonaje katika maisha yenu ya ki-dotcom?
Nawapa pole, lakini sisi tulikuwa na mawazo haya miaka hiyo ya 1960 na kuona kitakachotokea miaka hii ya dotcom.
Wasaalam,
Mzee Zuzu
Kipatimo