Leo hii ukimuuliza Mtanzania yeyote atakwambia anasoma namba ambayo haijui, dhana ya kusoma namba imekuja kipindi ambacho Rais wa awamu ya tano Tanzania alipoingia madarakani na kauli mbiu ya hapa kazi tu.

Leo hii nchini Marekani kuna waka moto, kuna timuatimua ya viongozi mbalimbali na raia ambao wanatiliwa mashaka ya uhalali wao, lakini pia kuna ujenzi wa ukuta mrefu sana ili kuzuia wananchi wa Mexico wasivuke ili kujipatia uhamiaji haramu.

Leo hii Tanzania moto na Marekani moto, imekuwa motomoto kote, Tanzania tunabadilika kwa mengi na tunapitia mambo mengi ambayo tulikuwa tukiyafanya kwa mazowea, leo tunajifunza kulipa kodi, leo tunajifunza kutumia bajeti na leo tunajifunza kufanya kazi.

Haya yanaweza kuwa mambo mabaya kuja ghafla kwa wananchi ambao walizowea kubweteka kutokana na mfumo wa maisha ambayo tulizowea kuishi, mambo huwa yanabadilika na mabadiliko huja na maumivu yake ambayo ni nadra kusema ni ya kawaida.

Kutokana na uzoefu wangu kwa awamu zote tano hakuna awamu ambayo watu walisema awamu hii ni bora kuliko awamu iliyopita, kila awamu huwa ngumu kuliko awamu iliyopita, hii inatokana na maono ya awamu mpya kuona mianya mibovu katika awamu iliyopita.

Kama ilivyo Tanzania ni kwa mataifa yote duniani na ndio maana awamu hii ya Trump inaonekana mwiba kwa wazamiaji na wajasiliamali wadogowadogo waliopo huko, wengi wao wakiwa ni wageni na ambao waliamua kutafuta maisha kwa njia ya mkato.

Hii ni hata hapa kwetu Tanzania, Tanzania iliyokuwa ya wakulima na wafanyakazi, sasa ikageuka kuwa Tanzania ya madalali na wafanyabiashara, wafanyakazi walisahauliwa na serikali na wakanunuliwa na wafanyabiashara, wakulima walisahauliwa na serikali wakawa yatima.

Awamu ya tano imekuja na kauli mbiu ya viwanda kwa maana ya wafanyakazi, imekuja na kaulimbiu ya hakuna njaa ili watu walime na wafanyabiashara wasiuze mazao yao kwa kigezo cha njaa, kilimo kinaswihi dhana ya hapa kazi tu, ni awamu ngumu na nyepesi kwa atakayeweza kujikubali kuwa sasa afanye kazi.

Awamu hii inataka kukubaliana na awamu ile kwa kujali utumishi uliotukuka, kujali maslahi ya taifa zaidi kuliko maslahi ya mtu mmojammoja, nasikia kawatumbua mabalozi wote, sielewi kwa sababu gani lakini ni lazima kwa lengo la kujali maslahi ya taifa kwa mtazamo wake kama rais.

Awamu yetu utumbuaji unaendelea kwa maslahi mapana ambayo labda utawala huu unayoona pasi na nguvu ya siasa zetu za mitaani. kila awamu ina lake jambo na tuone jambo la awamu hii na ile kwa maslahi ya taifa na maono ya viongozi wake.

Naamini kuwa awamu ya sita itakuwa ngumu kuliko awamu hii ya tano kutokana na maono ya viongozi wa awamu hiyo kwa makosa ambayo awamu hii hawajayaona au walishindwa kuyakabili kutokana na majukumu mengine.

Ni lazima tujue kuwa kuishi kwa mazowea kulishapitwa na wakati, kufanya mambo kienyeji na kuvunja sheria siyo utaratibu wa kawaida katika nchi yoyote yenye dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo wananchi wao.

Nchi yetu ni moja ya mataifa ambayo awali yalikuwa yakipindisha sheria kwa jeuri ya fedha za watu wachache, wapo waliokuwa Miungu watu wakifanya mambo mengi bila kufuata sheria, wapo walioshika mali za umma kama mali zao na familia zao.

Nchi yetu iligubikwa na rushwa, iligubikwa na utumishi usiotukuka kwa viongozi wa umma, ilitawaliwa na dhana ya pesa mbele kuliko utu, uongozi ulinunuliwa kwa pesa na siyo kura, fedha za umma zilitumiwa ovyo na watu wachache, sasa ni moto kwa wachache japokuwa wanaoumia ni wengi waliokuwa tegemezi na ndio wapiga miluzi kuwa utawala huu ni mbaya.

Nikuombe kiongozi wangu baada ya kuinyoosha nchi wakumbuke watumishi wa serikali yako ambao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana na kipato kidogo sana, naamini baada ya watumishi hewa na makusanyo ya kodi utafanya maajabu kwa watumishi wako ili nao watende yale unayotaka katika awamu yako.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.