Kama miaka 10 iliyopita, hawa wenzetu Wakenya walikuwa na kazi kubwa ya kusuluhisha mgogoro wa uchaguzi, uliosababisha baadhi ya Wakenya kupoteza maisha na wengine kuendelea kuwa walemavu hadi leo.
Wakenya hawa walikuwa wakitambuana kwa majimbo na makabila, hawakuwa kitu kimoja hadi pale akili ilipowajia na kujiuliza kuna nini ambacho kitatugharimu tukiwa wamoja, kwa kauli moja walivunja imani zao za ubaguzi wa ukabila na ujimbo na hatimaye wakaamua kuwa wamoja.
Umoja huo sasa umeleta faida zaidi, umeleta uzalendo, mshikamano na kuvunja itikadi za vyama, ukabila, ujimbo, ubaguzi wa rangi, elimu na matabaka ya walionacho na wasionacho. Lakini pia nimeambiwa kuwa hata vyama vya kiraia vimeungana, vyombo vya usalama kwa kushirikiana na vyombo vya habari vimefanya kazi bila kuwa na upendeleo. Ni Al-Shabaab ndiyo waliowafungua Wakenya kujua hali hiyo.
Mwaka fulani, Julius alikwenda Marekani, alikaribishwa chakula cha jioni na Gertrude Mongella. Wakati wa chakula, mama mmoja Mkenya alimwambia Julius kuwa Wakenya na Waganda walikuwa wakijuana kwa makabila, lakini Watanzania walikuwa hawajulikani kwa makabila.
Julius akamwambia ni wakati huo, lakini sasa Watanzania wanaona sifa kujuana kwa makabila. Alisema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wa kumchagua mgombea wa kiti cha urais mwaka 1995, Chimwaga mjini Dodoma.
Kama Julius angekuwa bado yupo hai angejua makubwa zaidi kwamba Tanzania ya sasa tumeshazoea kujuana kwa makabila na ajira kimakabila. Tumefika mbali kimaendeleo, udini sasa ndiyo umeshika kasi tunaheshimiana kwa udini, tunapeana kazi kwa udini, tunashirikiana shida kwa udini, tunaandamana kwa udini, tunaandaa Katiba kwa udini. Kwa ufupi tumeshaparaganyika.
Tusi kubwa la Watanzania kwa nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Jangwa la Sahara ni kuwaona wenzetu kama walioparaganyika, wao wakachukua nafasi hiyo kujifunza kutoka kwetu, sisi tukabweteka na kuwatazama wenzetu kama waliokosa kitu cha kujifunza na sisi tukaanza kujifunza kitu kipya cha kimaendeleo, kuvunja uzalendo tuliokuwa nao.
Tanzania ya kwetu tumefanya kazi kubwa ya kujenga utaifa na uzalendo, kujenga mshikamano na umoja, tumesaidia mataifa mengine kufanya kile ambacho sisi tunafanya, tumewatafutia Uhuru wa mataifa yao, mchango wetu ni mkubwa katika vyama vingi rafiki vinavyotawala dola katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tanzania ya kwenu inajitahidi kuongeza utandawazi ambao lengo kubwa ni kuwamilikisha kasumba na utamaduni wa mataifa ya Magharibi, utamaduni ambao wakati wetu kwa utamaduni wetu tuliona ni matusi makubwa kuwa tegemezi wakati tuna nguvu zetu, kusaidiwa kufikiri wakati tuna vichwa vyetu, kutubadilishia majukumu ya kila siku kwa mtindo wao na hatimaye tumekuwa ombaomba kutoka katika ardhi yenye kila kitu duniani.
Tanzania ya kwenu imegubikwa na dhana ya kwamba fedha ni kila kitu, fedha inahamisha uungwana na kupandikiza chuki miongoni mwenu, kazi rahisi yenye kuleta fedha haraka ni kaulimbiu yenu, mmeamua kuwa wasanii wa filamu badala ya kulima na kufuga, mmeamua kuwa wanamuziki badala ya kufanya kazi viwandani na mashambani na sasa mmeamu kuwa ma-Al shabaab ili mpate fedha za kujitoa maisha kiroho ama kitajiri, hiyo ndiyo Tanzania yenu!
Maombi yangu katika barua yangu ya saba niliwahi kusema natamani ifike siku ya hukumu, nione hukumu yenu na jinsi mtakavyokumbuka kazi kubwa tuliyoifanya sisi kuwatafutia amani hii mnayoichezea leo kwa hoja ya kwenda na wakati.
Yaliyotokea kwa wenzetu hapo Kenya ni fundisho kwetu kwa mambo mengi ambayo mimi nayakumbuka. Nawakumbusha, enzi zetu kulikuwa hakuna mgeni ambaye anaweza akaingia nchini na asijulikane anafanya nini na yuko wapi. Kitengo cha Usalama wa Taifa kilikuwa kina taarifa zote muhimu hadi ikafikia mahala wakawa wanataniwa kwamba waliweza kujua mtu kanywa bia chupa ngapi siku iliyopita.
Watu wa usalama walijua matukio na kuyachukulia hatua kabla hayajatokea. Mfano mzuri ni ule wa suala la mapinduzi ambalo Julius alitakiwa kupigwa risasi kanisani na nchi ichukuliwe na vijana wahuni ambao wote walikamatwa na mganga wao wa kienyeji. Huu ndiyo uliokuwa usalama wa nchi yetu.
Leo usalama wetu upo rehani, sijui kipi ni hatari kwa Taifa ambacho kinafanyiwa kazi mapema na wale mashahidi X na Y wa zamani. Tunasikia dawa za kulevya kilo kwa matani, twiga wanaswagwa na kupakiwa katika ndege hatuna habari. Wasomali wanavuka mipaka wanatembea usiku kucha wanakufa kwa kukosa hewa ndani ya Fuso ndiyo tunajua.
Ni Tanzania ambayo fedha zinaibwa mabilioni kwa mabilioni, lakini vyombo vyetu vya usalama vimefichwa na kulazimishwa kutosema kwa maslahi ya wachache, rushwa kubwa zinafanyika na kubadilishwa jina kuwa kamisheni au takrima na kuvifunga vyombo vya dola vyenye mamlaka ya kuhoji kushindwa kutokana na kubadilisha Azimio la Arusha.
Hii ndiyo Tanzania ninayoingojea kwa hamu kuona hukumu yetu ya kudharau kile ambacho kilijengwa kwa nia njema na watu wenye maadili ambao waliona fedha si msingi wa maendeleo.
Nangojea siku uzalendo utakapofika asilimia sifuri kwa Watanzania wakaamua kuwakaribisha maadui kwa rushwa, watakapoamua kuwa sehemu ya Al Qaeda, Al-Shabaab, Boko Haram na M23 labda baada ya hapo tutakaa mezani na kufikiri upya kwa akili ya kimapinduzi.
Al-Shabaab jaribu kuja Tanzania labda tutaanza kujenga uzalendo ambao tumeuona kwa Wakenya waliokuwa wameparaganyika, Wakenya ambao sasa wamesema wao ni wamoja na sisi tumekataa, labda tutaukumbuka uzalendo wa Taifa tuliokuwa nao na kuanza kuujenga upya na kuupa heshima.
Siwapendi wote kati ya hao, lakini kuna wakati tunatakiwa kujifunza kwa vitendo. Aluta Continua nimeandaa pagale langu Kipatimo kwa ajili ya kujificha wenyewe wakija kudai chao!
Wasalaam,
Mzee Zuzu
Kipatimo.