Kwa Mataifa ya Magharibi kila ifikapo Februari 14 wapendanao huitumia siku hii kutumiana jumbe zawadi na maua kuonyeshana hisia na namna kila mmoja anavyompenda mwenziye.

Katika siku hii ambayo chimbuko lake ni huko Roma ikihusishwa na askofu wa Kanisa Katoliki aliyefahamika kwa jina Valentine aliyefungwa kwa kukiuka amri ya Mfalme Claudius ll kwa kufungisha ndoa kwa siri.

Licha ya kwamba mataifa mengi ulimwenguni kote husherehekea sikukuu hii lakini kwa mataifa haya saba ni marufuku kwa raia wake kusherehekea siku hii kwa namna yoyote ile.

Malaysia

Huku asilimia 61 ya wakazi wa Malaysia wakiwa ni waumini wa dini ya Kiislamu,huchukuliwa siku ya Valentine kama kwenda kinyume na sheria za taifa hilo ambazo zina uhusiano mkubwa na Sheria za dini ya Kiislamu. Mnamo mwaka 2005 mamlaka ya kiislamu nchini humo iliunda sheria ya kuweka zuio la kuadhimisha siku hiyo.

Inaarifiwa kwamba 2011 takribani raia 80 walikamatwa na Polisi kwa kusherehekea sikukuu hiyo. Amri na ulinzi mkali hufanyika mijini katika hoteli na migahawa kubaini wanaoadhimisha siku hiyo.

Indonesia

Taifa hilo ambalo uchumi wake hutegemea sana shughuli za utalii, ikitembelewa na idadi kubwa ya watalii kutoka Australia ilipiga marufuku shughuli zozote zile zinahusika kwa namna moja ama nyingine kuadhimisha sikukuu ya wapendanao.

Mnamo Desemba 2022 Bunge la taifa hilo lilipitisha mswada wa kuharamisha ngono kabla ya ndoa jambo ambalo lilizua mijadala kwa raia na wanaharakati katika taifa hilo wakipinga sheria hiyo kuwa ni kukiuka haki za binaadamu.

Hata hivyo licha ya kuweka zuio la kuadhimisha siku hiyo,katika baadhi ya sehemu na miji maarufu ya taifa hilo kama vile Jakarta bado kuna watu huadhimisha kwa siri licha ya kuwa ni marufuku.

Iran

Kwa miaka ya hivi karibuni mamlaka nchini Iran ziliweka zuio la kuadhimisha siku ya wapendanao ikichukuliwa kama mila potofu za kimagharibi, vitisho vikali hutolewa kwa maduka na migahawa ambayo huuza au kutoa huduma zinazohusianishwa na siku hiyo.

Licha ya kuwepo kwa sheria hizo imeriptiwa kwamba katika mji wa Tehran maduka makubwa na migahawa huuza bidhaa kama vile midoli ya dubu chokoleti na maua mekundu ambayo kimsingi hutumiwa na watu kusherehekea siku hiyo.

India

Inaelezwa kwamba taifa la India tangu lijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni wao Uingereza mwaka 1947,Serikali iliweka jitihada ya kuhimiza raia wake kutokuhusudu mila za kimagharibi ikiwemo kusherehekea sikukuu ya wapendanao.

Mnamo mwaka 2015 kiongozi mmoja wa chama cha kisiasa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “Hatuko kinyume na kitu kinaitwa mapenzi, ila kama watu wapo katika uchumba na wanapendana basi itabidi waoane kwa ndoa na ikiwa hawana uhakika wa kuoana basi hawapaswi hata kutoka kwenda mahali pamoja kwa kigezo cha kusherehekea sikukuu ya wapendanao.”

India pia ni miongoni mwa mataifa yaliyoweka sheria inayozuia watu kushiriki ngono kabla ya ndoa.

Pakstan

Ni miongoni mwa nchi zenye msimamo mkali wa sheria ya dini ya kiislam na imewahi kukumbwa na ghasia nyingi kutokana na mabishano kuhusu kuadhimisha siku hiyo.

Mnamo 2014 zimewahi kuzuka ghasia baina ya wanafunzi wa vyuo kati ya chou kikuu cha Peshawar na Pakistan mabishano yao yakiwa ni juu ya itikadi za dini na sikukuu ya wapendanao inayochukuliwa kama kinyume cha sheria ya Kiislamu.

Inaipotiwa kwamba wanafunzi hao walirushiana mawe ambayo baadaye yalisababisha kurushiana risasi kutoka pande zote mbili na kuwajeruhi wanafunzi watatu.

Hata hivyo mnamo Februari 7 2018 Mahakama Kuu ya Islamabad ilipiga marufuku kusherehekea sikukuu ya wapendanao ikidai siku hiyo ni utamaduni wa kimagharibi ambao ni kinyume na mafundisho ya Uislamu.

Saud Arabia

Nchini Saudi Arabia, ni mwiko kuonyesha mapenzi hadharani ili dhana ya Siku ya Wapendanao isipatane na itikadi za nchi hii.

Wanaopatikana wakiadhimisha siku hii wanaweza kupata adhabu kali. Mwaka 2014,raia watano wa Saudia walihukumiwa kifungo cha miaka 39 jela na viboko 4,500 vya fimbo, baada ya kupatikana wakicheza na wanawake sita ambao hawakufunga nao ndoa katika siku ya wapendanao.

Ingawa unaweza kununua zawadi zenye mada ya upendo siku nyingine yoyote tofauti na Februari 14, Lakini maua mekundu na vitu vingine vinavyohusiana na mapenzi vimepigwa marufuku kabisa Siku ya Wapendanao, ikiwa ni pamoja na nguo nyekundu.

Urusi

Urusi husherehekea ya Siku ya Wapendanao kwa namna yake, ambayo ni toafuti na ilivyo katika mataifa mengine. Badala ya Februari 14, Warusi huadhimisha siku ya wapendanao Machi 8,ambayo ni siku ya kimataifa ya wanawake.

Siku hii hutumika kumuenzi na kumuonyesha mwanamke upendo ambapo hupeana maua na chokoleti ni jambo la kawaida sana katika siku hii, wanaume na wapenzi wanaotarajia kuonana huwaacha wanawake wawe huru na kupumzika siku nzima na hivyo husaidia shughuli za siku nzima kama vile kupika kufanya usafi hata kuhudumia.

Badala ya kusherehekea Siku ya Wapendanao kwa sababu ya mtakatifu Valentine kama ilivyozoeleka,Urusi huchagua kusherehekea upendo kwa wanawake wao, kutoa heshima kwa wanawake kote ulimwenguni kwa haki sawa.

Licha ya kwamba utamaduni huu umeenea na kukita mizizi ulimwengni kote ambapo katika baadhi ya mataifa ya Bara la Asia unapingwa vikali, kwa bara la Afrika hususani Tanzania watu husherehekea sikukuu hii, japokuwa haijathibitika waziwazi kuwepo taifa lolote linalopinga sikukuu hii.