Uamuzi wa Serikali, kupitia Bodi ya Filamu, kumfungia Wema Sepetu kujihusisha na masuala ya filamu kwa muda usiyojulikana kutokana na kuvuja kwa video yake ya ngono ni suala linalozua maswali.
Kwanza, nakubaliana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Godfrey Mngereza, anayeshuku unafiki wa Wema kuomba msamaha kwa kuvuja kwa video hiyo kwa sababu anasema si mara ya kwanza kwa video ya aina hii ya Wema kuonekana mitandaoni.
Inakubalika binadamu kujikwaa mara moja, au mara mbili, lakini ikianza kuonekana kuwa kila mara anajikwaa sehemu ile ile, si ajabu – kama Mngereza anayvosema – kudai ni bahati mbaya kutiliwa shaka.
Tabia ni suala moja, lakini inawezekana lipo tatizo limejengeka la imani kuwa mafanikio yanaweza kutafutwa kwa njia yoyote ile. Tunashuhudia kuwa Wema si pekee ambaye anakumbwa na kuvuja kwa video na picha za ngono. Inahitaji kuchunguza iwapo haraka ya mafanikio yanaziba uwezo wa mastaa hawa kutafakari jema na baya.
Inawezekana pia wanao uelewa makini kabisa wa jema na baya, lakini wakaamua kupima faida za baya na kuamua kuendelea na baya. Kukua kwa matumizi ya mitandao ya jamii na kupanuka kwa matumizi ya teknolojia kumechangia kuongezeka kwa mapato yanayotokana na umashuhuri wa mtu kwenye mtandao. Kwenye mtandao ubaya unalipa.
Tafiti nchini Marekani zimeonesha kuwa baadhi ya watu mashuhuri waliokumbwa na kashfa juu ya maisha yao binafsi wamejiongezea pia umashuhuri na kupanua uwezo wao wa kujiongezea kipato. Upo ukweli wa kiasi fulani kuwa ndani ya tasnia ya sanaa umashuhuri ni umashuhuri tu, iwe umeonekana umesahau kuvaa nguo au uwe Ninja.
Kuna neno la Kiingereza, infamy, ambalo halina neno linalofanana nalo kwa Kiswahili ambalo naamini linasaidia kueleza haya tunayoyashuhudia kwa wasanii wetu na watu mashuhuri kwa tasnia ya sanaa mbalimbali, lakini mahsusi filamu na muziki. Ni umashuhuri unaoletwa na suala ambalo si jema.
Kama kuna hoja moja naweza kuunga mkono kumtetea Wema na wenzake wanaosakamwa na Serikali sasa ni kuuliza sababu zao wao, kwa kiasi kikubwa, kuandamwa kwa suala ambalo limeenea sana kwenye mitandao ya kijamii.
Umaarufu una gharama yake. Akiyafanya mtu mwingine hatutayasikia, lakini kwa sababu ameyafanya Wema tutaendelea kuyasoma na kuyasikia kwa wiki kadhaa kuanzia sasa. Bangi inavutwa na watu wengi wasiojulikana na haileti mjadala, lakini anapovuta mtu mashuhuri wataalamu wanaandaa kongamano kujadili kukithiri kwa tatizo.
Inafahamika kuwa mitandaoni kumesheheni taarifa za watu wanaoweka picha na video za ngono kwa kukiuka Sheria ya Makosa ya Mtandao. Ilipoanza kutumika niliandika makala kusema kuwa ni sheria ambayo ina hitilafu kadhaa, lakini sikuona tatizo la sheria hiyo kwenye vipengele vinavyodhibiti matumizi ya picha na video za ngono.
Dhana ya sheria kuwa msumeno inakosa nguvu iwapo msumeno unamkata Wema na watu mashuhuri wenzake tu, lakini unawaacha wengine wengi ambao hawamulikwi na sheria zilizopo kwa sababu tu hawajulikani. Ingekuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya sehemu kubwa ya watu wanaonekana kukiuka sheria, sina shaka kuwa kila siku tungekuwa tunasoma taarifa za watuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Upo uwezekano kuwa Bunge lilipopitisha sheria hii ya Makosa ya Mtandao Serikali haikupima vyema mahitaji ya watu na gharama ya kusimamia utekelezwaji wake. Taarifa ya LinkedIn inabainisha kuwa watumiaji hai wa Facebook nchini Tanzania wanafika milioni 4.9 wakati watumiaji wa Instagram wanafika milioni 2.1. Hii ni takwimu nzuri kwa Facebook na Instagram, lakini itaumiza vichwa vya watu na mamlaka zenye jukumu la kufahamu ni nani leo kukiuka Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Serikali kote duniani zina uwezo mkubwa wa kudhibiti yanayojitokeza kwenye mitandao, lakini hayo yanawezekana tu kwa gharama kubwa. Lakini umuhimu wa watu wote kuonekana sawa mbele ya sheria unahitaji Serikali itumie gharama hiyo ili wale wanaoonekana kuachwa wakivunja sheria nao wadhibitiwe.
Ni kuachwa kutekelezwa kwa ukamilifu kwa sheria ndiyo kunatoa mwanya kwa baadhi ya watu kuendelea kukiuka sheria au kutofahamu kuwa wanakiuka sheria.
Mwaka mmoja kuanzia leo huenda tutayasahau au kuyapuuza haya ya Wema Sepetu na mastaa wenzake wanaokumbwa na tatizo la aina hii, lakini umashuhuri wao utabaki pale pale. Labda wao wanafahamu siri ya mafanikio ambayo wengine hatuifahamu: kulipa gharama kubwa sasa, na kupata malipo makubwa zaidi baadaye.
Kibano anachopata kinajibu na kukidhi kiu ya wale wanaotaka aadhibiwe na adhibitiwe. Lakini kinaleta swali lingine: ni lini wote ambao wanaanika picha na video kama yake watachukuliwa hatua?