MayweatherIlikuwa ni mkesha wa hiari kusubiri pambano la masumbwi kati ya Mmarekani Floyd Mayweather na Manny Pacquiao lililoacha gumzo kwenye ulingo mmoja maarufu pale Las Vegas, Marekani.
Wapo waliolala kwa mang’ang’amu kusubiri pambano hilo na wengine kukesha.
Kulikuwa na mabishano makubwa na timu ziliundwa kama kawaida. Wabongo kila jambo linaundiwa timu hata kama si la kihasimu. Kitu kilichoniacha hoi ni kule kusubiri kwa hamu pambano ambalo hatujui vigezo vyake katika kuamua mshindi hasa kama halitakuwa na ‘knockout’ (KO).
Kilichotokea siku ile nakifananisha na kile tunachokitumaini Watanzania kutoka pale TFF. Watanzania tuna matumaini na kupata tunachokitaka katika tuzo za TFF kwa waliofanya vizuri katika Ligi kwa maana ya kocha, mchezaji, kipa, mfungaji na mpuliza kipenga bora.
Watanzania wana matumaini na kuwa na timu bora za Taifa na pia wana matumaini kuwa na waamuzi bora wa kandanda. Matumaini haya hayana tofauti yoyote na kusubiri pambano la Mayweather na Pacquiao usiku ule, maana mshindi angekubalika na kueleweka endapo tu angeshinda kwa ‘knockout’ na si vinginevyo.


Si kama watu hawataki kukubali matokeo lakini hawaelewi vigezo vya kumpa ushindi huyu na kumnyima yule, na ili waelewe basi yule mstahilishaji anatakiwa kuelewesha wadau wa jambo husika.
Leo ukiuliza kuhusu tuzo zilizotolewa na TFF kwa washindi mbalimbali, wengi wao watakwambia hawana ugomvi na tuzo iliyotolewa kwa mfungaji bora kwa kuwa hapo ni kama ‘knockout’, ipo wazi na haina ubishi.
Ukiuliza kuhusu kocha bora, mchezaji bora, kipa bora na mengineyo, watu wataguna tu na wengine watachambua mpaka hutaona maana ya tuzo kama hizo.


Katika tuzo za kipa, kocha na mchezaji bora watu wanabishana na wataendelea kubishana maana haieleweki vigezo gani vilitumika kuamua ushindi wa tuzo hizo. Kama umeshiba na una hamu ya kutafuta njaa nenda kijiweni kaulize ni nani alistahili ushindi kati ya Mayweather na Pacquiao?
Hapo watu watabishana mpaka muuliza swali utajutia swali lako. Timu Pacquiao watakuambia refa, ulingo, mashabiki, na majaji wote ni Wamarekani isingewezekana mtu wao kupewa ushindi.
Timu Mayweather hawana maneno ya kubishana zaidi ya kutaja vigezo hafifu ambavyo havithibitishi ushindi wa mbabe huyo. Tatizo hilo lisingetokea kama mshindi angepatikana kwa ‘knockout’ kwa kuwa vigezo vyake vipo wazi kama kwa mfungaji bora. Utakuwa umetoroka wodi ya vichaa kama utasema Simon Happygod Msuva alipendelewa kupewa zawadi ya mfungaji bora.


Kinachoonekana hapa ni kukosekana kwa vigezo vya wazi vya kupata washindi wa hizo tuzo, mashabiki wa soka hawana ugomvi na Kado wala Makata ila hawajui vigezo gani vimetumika.
Kama vigezo vingejulikana sidhani kama kuna mtu angelalamika maana angekwenda kwenye vigezo na kupata majibu, na hata wao TFF wasingepata mzigo wa kujibu bali vigezo vingejibu vyenyewe.
Watu hawaelewi vigezo, hawajui jaji anatoka upande upi na ana sifa zipi mpaka amstahilishe huyu na kumnyima yule. Watu hawaelewi hata namna ya uteuzi wa hayo majina ya wanaowania tuzo hizo.
TFF wekeni mambo wazi kabla watu hawajakata tamaa kabisa na soka la nyumbani, wakawa wakimbizi wa kudumu wa soka la Ulaya na wakaukana utaifa wao milele.


Mashabiki wa soka popote duniani ni waelewa sana kama kanuni na taratibu zikiwa wazi, ndiyo maana hawashangai timu yao ikitolewa mashindanoni kwa kupata matokeo ya 0-0 ugenini na matokeo ya 1-1 nyumbani, ni kitu cha ajabu sana lakini kimekubalika kwa kuwa kanuni hiyo ipo wazi kwa kila mtu. TFF usiri katika utendaji wenu unaondoa ladha ya soka na kwa hapa karibuni mlianzia kwa Ajibu na kadi tatu za njano.
Mambo haya yanawachefua wadau wa soka na hata kuvutia wadhamini zaidi inakuwa ngumu. Wekeni vigezo wazi ili mambo kama haya yanapojiri watu waende ukutani kusoma na waridhike wenyewe kwa hoja za ukutani si za moyoni.
Soka ni mchezo wa wazi na ni vizuri uwazi ukaanzia kwenu TFF kisha ukashuka kwenda kwa waamuzi huko viwanjani. Watu wanataka kujua mipango ya wazi ya kuipa makali Taifa Stars, Twiga stars, Serengeti Boys ili hata kama tukifungwa tukatazame ukutani tujue kama nchi kuwa mpango wetu katika soka tujiridhishe.


Kurudisha au kuongeza imani ya watu katika jambo husika ni kuwa wawazi tu hakuna jingine. Watu wanataka kujua vigezo vilivyotumika kumtimua Poulsen na kumleta Mart Nooij na pia wanajiuliza ni jambo gani baya halikuvumilika kwa Poulsen ambalo leo linavumilika kwa Mart?
Watu wanauliza kama baada ya kelele nyingi Nooij amepewa mtihani wa kufuzu CHAN, kwanini Poulsen hakupigiwa kelele kama hizi lakini hakupewa hata jaribio ili kumpima?
Wapenda soka hawaelewi vigezo gani vinatumika kumpeleka uwanjani mchezaji ambaye timu yake inamuweka benchi? Hapa soka letu linaingia ukakasi mkubwa maana haieleweki kama tatizo ni la TFF au kocha maana hata ujio wa kocha mwenyewe haukuwa na baraka katika mioyo ya wapenda soka. Watu wanataka kuwekwa wazi na mambo mengi kuhusu soka letu.


Tusaidieni kujua kwanini Twiga Stars haina udhamini mnono kama Taifa Stars? Kwanini mlimuondoa Poulsen ambaye kama kocha alikuwa na mipango ya muda mrefu kwa kuwa na kikosi mchanganyiko?
Stars Maboresho mbona ilipigwa teke na Nooij na hamkusema chochote au mkataba mliompa hamkumuonesha mipango yenu? Vigezo gani mnatumia kupata wachezesha kandanda hapa nchini vijana kutoka mikoa yote wanataka kuingia hapo wafanye kazi?
Wekeni mambo wazi maana kutoweka mambo wazi hufanya watu waone kuna harufu ya “dili” hata kama hakuna hizo “figisu-figisu”. Nilipotoka kuangalia pambano la Mayweather na Pacquiao Mei 3, 2015 niliamini watu wamepiga “dili” kwa kuwa nilikosa kupata uwazi ambao ninatamani TFF wawe nao. Nikaingia katika ukurasa wangu wa facebook na kuandika haya ambayo sitamani watu wayaseme kuhusu uendeshaji wa mambo pale TFF.


Tulibishana, tuliwekeana dau, na saa hizi ndiyo tunarudi kulala kutoka katika mkesha wa Mayweather na Pacquiao. Watu wale wametengeneza pesa nyingi sana kupitia kile walichotuambia ni pambano la kihistoria na watu maarufu wa kihistoria walikuwapo, lakini hakukuwa na mpambano wa kihistoria kama yale ya kina Tyson, Evander, Mohamedi Ally na kadhalika. Kilichotokea watu walikaa wakawaza kupiga pesa za kihistoria na wakatengeneza jambo liitwe la kihistoria.


Pambano limekwsha majibu ya wazi ushindi umepatikanaje hayapo tumerudi tunabishana na tutazidi kubishana. Nafikiri ni wakati wa kufikiria mbinu ya kupiga pesa za kihistoria kwa kuandaa tukio halali la kihistoria na watu waone ni la kihistoria katika dakika 36 tu.
Pale hapakuwa na mtu aliyepanga kupiga ‘knockout’ na kama ulikuwa unaisubiri ulijidanganya, wale watu ni kama walijadili jinsi ya kupiga pesa na si ajabu walikubaliana nani apigane sana ila awe makini asimalize knockout na nani awe mshindi.”
Nikiwa najifunika shuka namkumbuka yule mkusanya kiingilio pale ‘kibanda umiza’ alivyokuwa anaruka juu kwa shangwe huku ameshika kitita cha ‘jero-jero’ zetu, naye namuona alijiandaa kufaidika na tukio la kihistoria, na mimi nalala nijipange kuandaa tukio la kihistoria.”
TFF fanyeni mambo kwa uwazi mtujengee imani tumsahau Mayweather katika soka letu maana hata Timu Mayweather hawana raha na ushindi wa masimango. Mambo yakiwa wazi hakuna atakayelalamikia ushindi wa ugenini au atakayebishana na knockout.
 
Baruapepe: [email protected] Simu: 0715 36 60 10