Kim Poulsen aliondolewa kazini bila kuwapo sababu zenye kuingia akilini. Alikuwa na mipango ya kuleta mabadiliko ya uchezaji wa Taifa Stars ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Waliomuondoa hawakulifahamu suala hilo, ingawa ni jambo muhimu lenye kutakiwa kupewa kipaumbele. Ufundishaji wa Poulsen uliwafaa wachezaji wetu, aina ya mfumo alioutumia uliendana na wachezaji wenye miili midogo tulionao.
Taifa Stars ya Poulsen iliyotumia mfumo wa 4-3-3, uliosisitiza umiliki wa mpira, ilitoa burudani kwa mashabiki uwanjani. Lakini kitendo cha uongozi wa TFF wakati huo chini ya Jamal Malinzi, kumuondoa kocha huyo kwa kigezo cha kutafuta kocha mwenye uzoefu zaidi na mazingira ya Afrika, kilikuwa ni mwanzo wa kuzivuruga juhudi zote zilizofanywa na Poulsen pamoja na wasaidizi wake.
Poulsen alikuwa amekwisha kuandaa mtiririko wa kurithisha nafasi za wachezaji wenye kueleweka. Kizazi cha kina Jonas Mkude kilikuwa kikiandaliwa kwa ajili ya kupewa nafasi ya kuichezea Taifa Stars. Wasaidizi wa Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na John Bocco, walishaanza kupewa mazoezi pale Uwanja wa Karume.
Uongozi mpya wa TFF ulipoingia madarakani wala haukujisumbua kutaka kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea kufanyiwa kazi kitaalamu. Kocha mkuu mwenye dira na ambaye alikuwa bado hajafanikisha mafanikio, japo nusu ya kile alichotarajia kukifanya, akajikuta anaondolewa kazini. TFF ikafanya kosa la kusikiliza baadhi tu ya maoni ya wadau na kuyafanya kuwa ndiyo dira yenye kuwaongoza.
Kwa hiyo lilikuwa kosa kubwa lililofanywa na TFF pale walipoamua kuachana na kocha ambaye tayari alikuwa katikati ya mipango ya kuleta maendeleo. Ni sawa na kocha mmoja mkubwa aifundishe timu ya Taifa ya Nigeria kwa mafanikio halafu eti ndicho kiwe kigezo cha kumpa nafasi ya kuifundisha Taifa Stars.
Mpango huo wa TFF wa kutaka Taifa Stars ifundishwe na kocha mwenye uzoefu wa soka la Afrika, ulitakiwa umsubiri Poulsen aache kitu fulani kwenye uchezaji wa Taifa Stars pamoja na utengenezaji wa mfumo bora wa urithishwaji wa namba za wachezaji uwanjani.
Tuje sasa! TFF, Simba mpaka Yanga ni baba mmoja – mama mmoja. Wote wanataka mafanikio ya haraka wakati hakuna msingi uliowekwa. Tuachane na ya TFF. Tuzitazame hizi timu za Kariakoo.
Yanga
Yanga nayo imemtimua Kocha wake, Mwinyi Zahera na timu imekabidhiwa kwa muda kwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’.
Kosa kubwa la Zahera ni kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho. Hakuwa na jipya na hata kikosi chake hakikucheza vizuri.
Mmoja wa wachezaji bora kupata kutokea Tanzania ambaye pia kwa sasa ni kocha, Abdalllah ‘King’ Kibadeni’, analikiri hili na kusema, Yanga haikuwa na uelewano unaostahili uwanjani.
“Yanga imefanikiwa kupata mtu anayejua tamaduni za klabu hiyo, simfahamu vizuri Zahera, lakini timu haikuwa na muunganiko,” amesema.
Dk. Mshindo Msolla
Ni mwenyekiti wa Yanga, aliye pia kocha mwenye taaluma ya juu ya ukocha. Ninamfahamu, lakini ukweli ilipaswa aende na upepo ili kuwaridhisha watu anaowaongoza.
“Tunataka kutoka hapa tulipo na timu inakwenda kwa Charles Boniface Mkwasa mpaka pale tutakapopata kocha wa kudumu,” amesema Dk. Msolla, lakini akakataa kwenda mbali zaidi.
Boniface Mkwasa
Charles Boniface Mkwasa ambaye amewahi kufundisha Stars akiwa pamoja na Dk. Msolla amekiri ana kazi ngumu na falsafa yake kubwa ni kusaka ushindi, hataki kingine chochote.
“Ninachotaka Yanga ifanye kweli na ifike mbali, kwangu ni ushindi tu na ndiyo falsafa ninayoongozwa nayo,” amesema.
Mwinyi Zahera ashangaa
Mwinyi Zahera amesema uongozi umefanya haraka kumtoa kwenye timu kwani hakufanya vibaya.
Amesema kila mtu alikuwa anajua Yanga isingeweza kuwatoa Pyramids ya Misri kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa sababu ni timu tajiri na ina wachezaji wazuri.
Amesema kwa upande wa ligi mpaka sasa halikuwa hajafanya vibaya, kwani alicheza michezo minne, ameshinda miwili, sare moja na kupoteza mmoja.
“Walitakiwa kusubiri angalau labda tumecheza mechi 10 tumefungwa ndipo waseme, lakini sasa ninaona sababu kubwa ya kunitoa si matokeo, kuna kitu nyuma yake,” amesema Zahera.
Kocha huyo amesema kama kutakuwa na timu yoyote inayomhitaji yupo tayari kufanya nayo kazi.
Ameongeza kuwa tayari kocha wa timu ya taifa ya Congo amemtafutia wakala ambaye anamhitaji kwa ajili ya kumpeleka kwenye timu ambayo hakutaka kuitaja.
Makosa yasawazishwe
Unapoanzisha mpango wa kutaka kutengeneza kikosi au timu ya taifa au klabu, tena kutoka timu za mitaani za Tanzania nzima, lazima uwe na kitu makini ulichofanya.
Hatuna vituo vya kukuza vipaji, lakini pia hatuzalishi makocha na kama kuna mahali tunakosea, hii fukuza fukuza ya makocha haitusaidii. Tusawazishe pale tulipokosea ili tutoke hapa tulipo.
Kama anavyosema Poulsen, angeachwa aendelee na mpango wake wa kuitengeneza Taifa Stars yenye kuweza kudumu kwa miaka mingi.
Poulsen alikwisha kutuelewa tunataka nini na alikwishaweza kutengeneza mikakati yenye kufanana na aina ya wachezaji tulionao, alichohitaji ni muda tu.
Hivyo, TFF, Yanga na hata Simba, wote ni wamoja, maana Wekundu wa Msimbazi nao wameshaanza kutaka kumtoa mtu kafara.