Na Mwandishi wetu

Kulikuwa kuna upuuzi wa aina mbili katika kesi ya Feisal; kuamini mawakili wa Morrison wangeshinda kesi ya Feisal kama walivyoshinda kesi ya Morrison na upuuzi wa pili na kuamini Feisal alistahili kudai haki yake. 

Kesi ya Morrison na Yanga ilikuwa ni kuangalia kama mkataba aliosaini na Yanga ulikuwa halali au sio halali baada ya mkataba wake wa awali kutamatika. Kesi ya Feisal na Yanga ilikuwa inafanishwa na ya Morrison wakati Feisal ana mkataba halali na Yanga tena mkataba wa miaka miwili. Huu ulikuwa ni upuuzi uliopewa uhalali na wachambuzi. 

Upuuzi mwingine ni ule wa kudhani eti Feisal alikuwa sahihi kudai haki yake. Haki ipi? Alikuwa halipwi mshahara waliokubaliana? Alikuwa hapati nafasi ya kucheza? Aliposaini mkataba alisaini akiwa amelewa au alilazimishwa kusaini mkataba? Kama halikuwepo moja kati ya hayo basi mkataba wa Feisal ulikuwa ni halali. 

Kuna hoja za eti Yanga walipaswa kumlipa zaidi Feisal baada ya kuona kiwango chake kimepanda. Hapa Kuna mambo mawili ya kujiuliza; kiwango cha Feisal Salumu kilipopanda hakukuwa na mchango wa Yanga katika kukuza kiwango hicho? Kwanini Yanga haifikiriwi namna ilivyowekeza kwa mchezaji huyo mpaka akafika hapo alipofika?

Yanga walimgharimia vitu vingi zikiwepo bonus na benchi bora la ufundi na kambi nzuri mpaka Feisal kuwa hivyo alivyo na ndio maana wachezaji waungawana hushukuru timu zao wakiwa katika ‘peak’ badala ya kufanya alichofanya Fei Toto. 

Swali la pili, ni wapi katika mkataba wa Fei Toto kuna kipengele cha kuongezewa mshahara ikiwa kiwango chake kitapanda? Yanga wana uhalali wa kumtumia Feisal bila kuboresha mshahara wake mpaka mkataba utakapoisha na hakuna dhambi yeyote ile. 

Yanga kutoboresha maslahi ya Feisal ili kumuongezea mkataba ni kwa hasara yao wenyewe kwa sababu mchezaji akimaliza mkataba ataondoka bure klabuni kwake lakini leo imekuwa kituko kwamba Yanga kutoboresha mkataba ni kosa. Sijui ni uchambuzi wa namna gani ulitumiwa na baadhi ya waeledi wa soka. 

Sadio Mane hakuboreshewa mkataba wake pale Liverpool na Mane hakuondoka Anfield bali alitulia na kuitendea mema klabu yake mpaka mkataba ulipokwisha akagoma kusaini mkataba mpya na akaondoka zake kwenda Bayern Munich. Haikuwa dhambi.