Kwenye hotuba aliyotoa ndani ya Bunge la Afrika Kusini baada ya
kuanguka kwa utawala wa kibaguzi wa nchi hiyo, Mwalimu Julius Nyerere
alilalamika jinsi ulimwengu unavyoiona Afrika, siyo kama bara
linalojumuisha nchi zaidi ya 50, ila kama nchi moja.
Ulimwengu, hasa wa nchi zilizoendelea umechagua kuliona Bara la Afrika
kama moja, na huzungumzia masuala ya Afrika kufanana kuanzia Misri
hadi Afrika Kusini, kuanzia Morocco hadi Djibouti. Kama zipo tofauti
hazionekani kuwa ni tofauti za msingi.
Alilalamika kwenye hotuba hiyo, lakini mwishowe akakubali uwezekano
kuwa si wazo baya kukubali nchi zaidi ya hamsini zilizo huru kuonekana
kama nchi moja. Tukifanya mapitio ya msimamo wa Mwalimu Nyerere juu ya
umuhimu wa umoja wa Waafrika tunapata jibu kwanini anaona si jambo
baya kukubali jina moja kuwakilisha nchi zaidi ya hamsini.
Ipo faida ya kujulikana kama wamoja, lakini zipo hasara pia za
kufahamika hivyo. Faida ni kuwa Bara la Afrika linaposifiwa sifa ni
yetu sote, lakini Afrika inaposemwa vibaya, basi wote tunasemwa bila
kujali ni nani chanzo cha kusemwa kwetu.
Tangu kuondoshwa kwa serikali ya kibaguzi nchini Afrika Kusini
matumaini makubwa yaliwekwa juu ya nchi hiyo na ikaonekana mfano bora
wa uongozi, demokrasia, na usimamiaji bora wa kukua kwa uchumi kwa
nchi za Afrika.
Nelson Mandela, kiongozi aliyekuwa kifungoni kwa miaka 27 na kuwa rais
wa kwanza wa nchi hiyo alitajwa kuwa mfano bora kabisa wa maridhiano
kati ya Waafrika wa nchi hiyo walioishi ndani ya mfumo wa kibaguzi kwa
miongo mingi dhidi ya wazungu ambao walinufaika na mfumo huo wa
kibaguzi kielimu, kijamii, kiuchumi na katika kila nyanja ya maisha.
Huu ndiyo mtazamo ambao ulionekana kwa wale ambao wako nje ya nchi
hiyo. Ndani, Nelson Mandela anakumbukwa kama kiongozi aliyeanza
uongozi wake wakati wazungu wanashikilia asilimia 30 ya ardhi,
akiahidi kuwezesha Waafrika weusi kumiliki ardhi zaidi, lakini
alipostaafu ni asilimia 3 ya ardhi ilihamia kwa kundi hilo.
Mandela atakumbukwa kama kiongozi aliyeleta utulivu wa kisiasa
ulioruhusu jitihada kufanyika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na
kijamii. Hata hivyo, yale mabadiliko makubwa na matumaini makubwa
ambayo yalisubiriwa na wananchi wa Afrika Kusini hayakupatikana chini
ya uongozi wake.
Ni hivyo hivyo pia kwa kiongozi aliyemrithi, Thabo Mbeki, ambaye
anasemwa na baadhi ya watu kuwa ni kiongozi ambaye alikuwa na mtindo
wa kulazimisha uamuzi na kutumia nguvu kubwa chini ya mamlaka ya
utawala na ushawishi wake wa kisiasa kuwaminya wapinzani wake ndani ya
chama chake cha siasa.
Julius Malema, wakati bado akiwa kiongozi wa chama cha vijana wa chama
cha African National Congress (ANC), alimtaja Mbeki kuwa ni dikteta.
Kilichomwondoa madarakani Mbeki ni tuhuma zilizoibuka ndani ya ANC za
kushinikiza mamlaka za kisheria kuchunguza tuhuma za rushwa dhidi ya
Jacob Zuma aliyekuwa mpinzani wake ndani ya chama. Rais Zuma
amelazimika kujiuzulu hivi karibuni. Kilichomwondoa madarakani Zuma ni
pamoja na tuhuma hizo hizo za matumizi mabaya ya madaraka na rushwa
dhidi yake.
Tuhuma za rushwa si nyepesi. Mwaka jana Mahakama ya Rufaa ya Afrika
Kusini ilitoa uamuzi kuwa Zuma anapaswa kujibu mashitaka 18 ya rushwa,
udanganyifu, utapeli, na utakatishaji wa fedha haramu kuhusiana na
ununuzi wa silaha uliyofanyika mwaka 1999.
Jina la wanafamilia ya Gupta limeibuka mara kwa mara kwenye tuhuma
zinazomwandama Zuma. Familia hiyo inasemwa kutumia uhusiano wake wa
karibu na Zuma kushinda mikataba ya thamani kubwa kutoka serikalini
pamoja na kushawishi uteuzi wa mawaziri. Wanafamilia hao wanakanusha
tuhuma hizo.
Waliomuunga mkono Zuma ndani ya ANC na kufanikiwa kumwondosha Mbeki
madarakani ni dhahiri, katika harakati zao za “kumpindua” Mbeki na
kumweka Zuma madarakani, walijipofusha na kushindwa kuona kuwa
walikuwa hawambebi Zuma peke yake, ila walikuwa wanabeba pia na tuhuma
zake za rushwa.
Na kama vile tuhuma alizokuwa nazo kabla hajawa rais zilikuwa
hazitoshi, tuhuma nyingine mpya za rushwa na matumizi mabaya ya
madaraka zikajitokeza aliposhika madaraka.
Mwaka 2016 Mahakama Kuu ya Afrika Kusini iliamua kuwa Zuma alivunja
katiba ya nchi aliposhindwa kurejesha pesa za serikali alizotumia
kufanyia ukarabati nyumba yake binafsi.
Kuna msemo wa Kiingereza kuwa hulka ya kuku ni kurudi kukaa kwenye
kiota chake ifikapo jioni. Matendo mabaya ambayo mtu aliyafanya zamani
huwa na tabia ya kumwandama baada ya muda. Inaweza kuchukua muda,
lakini mwishowe hujitokeza tu.
Kwa mfano huu wa uongozi wa Zuma tunaweza kuwa na uhakika kuwa wasiyo
Waafrika wakianza kutoa mifano ya mabaya ya yanayotokea Afrika, basi
uongozi wa Zuma utakuwa kipengele kimoja kutajwa juu ya mabaya ya
Afrika.
Mimi sikubaliani na hii hukumu ya jumla ya kwamba mfano mmoja mbaya wa
uongozi barani Afrika unahalalisha kuhukumu Afrika yote. Mimi ni
muumini mkubwa wa falsafa ya kila mtu kubeba mzigo wake, hasa kwenye
tuhuma zinazohusu ukiukwaji wa maadili ya uongozi. Lakini ukweli ni
kuwa tunachoamini siyo kinachotokea. Mzigo wa tuhuma alioubeba Zuma
kwa kipindi kirefu cha uongozi wake ni mzigo wetu wote, tutake
tusitake.
Kwenye pembe nyingine za ulimwengu kiongozi mbovu akijitokeza na
kuanza kujilimbikizia tuhuma ambazo zinaweka dosari kwenye uongozi
wake na kwenye chama chake cha siasa, wa kwanza kumshughulikia huwa ni
wanachama na viongozi wenzake wa chama chake cha siasa.
Mifano mingi ya Afrika inatufundisha kuwa wanachama na viongozi wa
vyama vya siasa huona kuwa wajibu wao wa kwanza ni kwa kiongozi
wanayemuunga mkono. Maslahi ya chama yanafuata, halafu mwisho kabisa
yanafuata maslahi ya Taifa.
Umefika wakati sasa kwa wanachama wa vyama vya siasa kupima vipaumbele
muhimu vya kuongoza uamuzi wao wa kisiasa na kutupunguzia aibu ambayo
tunaibeba kwa sababu ya uamuzi wao mbovu na unaoandamwa na ubinafsi.