Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Xavier Mrope Daudi, ametoa rai kwa watumishi wa umma kuzingatia maadili na kutumia lugha zenye staha wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha tija inayokusudiwa na Serikali.
Aidha, aliwasihi watumishi kuendana na wakati kwa kukumbatia teknolojia ili kuongeza ufahamu na kurahisisha utendaji kazi wao.
Xavier alitoa rai hiyo, Februari 21,2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Baraza la Nne la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), uliofanyika katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano, Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kwamfipa, Kibaha, Mkoani Pwani.

Pia, aliwaasa watumishi na watendaji wa mamlaka hiyo kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kuwa waadilifu.
Alisema, kupitia uzingatiaji wa misingi hii, fedha za walipa kodi zitatumika kwa manufaa ya umma na kuwa na thamani halisi ya fedha za serikali zinazotumika kwa umma.
Kwa mujibu wa Xavier, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuleta maendeleo kwa kasi kubwa, ikiwa ni pamoja na maboresho ya kiutendaji na kimifumo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ununuzi na udhibiti.

Aliitaka PPRA kuzijengea uwezo taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kwa mafunzo mbalimbali ili kuhakikisha wanapata uelewa wa matumizi sahihi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, kanuni zake, pamoja na matumizi ya mfumo wa kielektroniki (NEST).
“Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeanza kutumika tangu Juni 2024, Mfumo huu ni mzuri, endeleeni kuusimamia ili usaidie kuondoa changamoto zilizokuwepo awali,” alisisitiza Xavier.
Xavier aliipongeza Mamlaka kwa kupata hati safi na kuwa na mifumo unganishi inayosomana, ambapo NEST inasomana na mifumo mingine 20, ikiwemo mifumo ya malipo, ili kurahisisha ununuzi wa kidigitali.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Dennis Simba, alieleza kuwa, pamoja na mambo mengine, mkutano huo umejadili changamoto zinazowakabili ili kupendekeza njia za kuzitatua.

Alitaja changamoto inayowakabili kuwa ni upungufu wa watumishi, jambo ambalo Naibu Katibu Mkuu huyo aliahidi kulifikisha kwa Katibu Mkuu na litafanyiwa kazi.
Simba alieleza kuwa, licha ya changamoto hiyo, wamefanikiwa kusimamia udhibiti wa ununuzi wa umma chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024, ambazo zimetaka ununuzi kufanywa kwa njia ya mfumo wa kielektroniki.
Kadhalika, walikuwa wakisimamia maboresho ya sera, sheria, na kanuni za ununuzi wa umma, ambapo wameimarisha uwazi na uwajibikaji katika michakato ya ununuzi.
