Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia,Mtwara
Wananchi na asasi kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wametakiwa kupaza sauti za kuwalinda viumbe hai walio hatarini kutoweka katika maeneo yao.
Akizungumza katika mkutano wa wadau kutoka asasi mbalimbali na wananchi mkoani Mtwara ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF), Mwezeshaji kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI),Numan Amanzi, amesema suala la kupaza sauti kwa ajili ya uhifadhi wa viumbe hai ni muhimu kwa sababu ya tishio la kupotea.
Amanzi amesema kwa sasa duniani kuna zaidi ya viumbe hai 14,336 walio hatarini kutoweka huku Tanzania ikishika nafasi ya 15 kwa kuwa na viumbe 900, wakiwamo ndege, samaki, mimea na vyura wanaopatikana sehemu moja tu kutokana na mfumo wa ikolojia kutofautiana na nyingine.
Ofisa Ulaghabishi Sera wa Mradi wa Kupaza Sauti wa WWF, Nuhu Salasala, amesema lengo la shirika hilo ni kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufahamu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza viumbe hai ili kuisaidia nchi kupata faida zinazotokana na utalii na ulindaji wa nyara.
Nuhu amesema elimu hiyo itawawezesha jamii na wadau kushiriki moja kwa moja kusaidia kupaza sauti katika maeneo yao na kusababisha kuongezeka kwa utunzaji wa ikolojia isiharibiwe.
Amesema Tanzania ni moja ya nchi zilizoridhia kupaza sauti kwa ajili ya viumbe hai na ulianza kufanyiwa kazi na WWF mwaka 1996.
“Kuna miti ya asili ambayo ni muhimu na inatakiwa itunzwe na wananchi ndio watunzaji wakuu, kwa sababu hiyo tumewakusanya wadau wote kutoka asasi mbalimbali ili wajifunze kuhusu umuhimu wa kutunza viumbe hai.
“Tunao mradi unaongalia namna gani asasi na watu wanashirikishwa katika kuchangia utekelezaji wa huu mkataba wa bioanoai, wananchi wanatakiwa kujua umuhimu wa utunzaji ili wapate fursa ya kujua na kushiriki kwa sababu wao ndio inawazunguka.
“Miti ya asili ni muhimu kwa mazingira yetu lakini inaondoka, kwa hiyo ukizungumzia viumbe hai ni watu na wanyama pori wanaoizunguka jamii, baadhi yao wanatoweka labda kutokana na mazingira si rafiki au ukaribu wa nyumba zao,” amesema.
Amesema wananchi na wadau wanapaswa kujua baadhi ya mikataba ambayo nchi imeingia kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa ajili ya kutunza viumbe hai walio hatarini.
Ametolea mfano mwaka jana nchi 196 zilikutana kwa ajii ya kujadiliana masuala ya viumbe hai na wameafikiana kuwa na mpango wa kuyasimamia kwa mwaka 2020 hadi 2030, lakini ulichelewa kutekelezwa kwa sababu ya mlipuko wa Uviko-19.
“Kwa pamoja tushirikiane tuwe sehemu ya kushiriki kutekeleza mradi huu na tunapaswa kujua unavyotelekezwa kitaifa na kimataifa,” amesema.