Jumanne, Mei 7, mwaka huu maelfu ya Wana Dar es Salaam walikusanyika katika Ukumbi wa Karimjee kuaga mwili wa mpendwa wetu Dk. Reginald Mengi.

Runinga za ITV, Star TV, Channel 10, Clouds TV, televisheni za mitandao ya kijamii na redio mbalimbali zilionyesha na kutangaza shughuli ile mubashara.

Mmoja ya wazungumzaji siku ile alikuwa James Mbatia. Wakati anazungumza alisikika akitamka kuwa kati ya Januari na Machi mwaka huu amekutana na kufanya mazungumzo na Dk. Mengi mara tatu.

Katika fursa hizo tatu, safari ya tatu ilikuwa Machi 20, mwaka huu na katika mazungumzo yao siku ile hayati Dk. Mengi alitamka jambo moja kubwa.

Mbatia alitamka kwa mkazo kuwa siku ile na katika kikao kile Dk. Mengi alitamka: “Maisha yako kwenye ulimi wa binadamu.” Tamko lile mimi naliita ndiyo WOSIA wake wa mwisho alioutoa kwa Watanzania. Ni maneno mazito, yenye mzizi wake kutoka katika Biblia Takatifu. Inafaa kila Mtanzania atafakari na apokee kwa uzito sana wosia huu kama Mbatia alivyoeleza.

Katika Kitabu Kitakatifu – Biblia, tunasoma kutoka Waraka wa Yakobo Mtume, Sura ya Tatu maneno haya; nanukuu:

Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi ili watutii; hivyo twageuza mwili wao wote. Tena angalieni, merikebu ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, kokote anakoazimia kwenda nahodha. Vivyo hivyoULIMI nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto, ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwashwa moto na Jehanamu. Maana kila aina ya wanyama na ya ndege na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini vinafugika, navyo  vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ULIMI hakuna mwenye kuufuga, ni UOVU usiotulia, umejaa SUMU iletayo mauti.” (Yak. 3:3-8).

Ukiyasoma maneno hayo katika Biblia, unaweza kuona msingi wa hofu na wasiwasi aliokuwa nao hayati Dk. Mengi ndipo akaamua kumweleza mwanasiasa Mbatia, mbunge kwa imani na matumaini kuwa ataufikisha ujumbe ule kwa wanasiasa wenzake ili waufanyie kazi – au niseme ataufikisha mahali husika na panapostahili kufika.

Hayati Dk. Mengi amepatwa na wasiwasi hasa baada ya kuona namna baadhi ya wanasiasa wanavyotumia ulimi kuchochea vurugu na namna hata vurugu hizo zimeweza kuleta vifo kama kile cha mtoto Akwilina. Ndipo alimwomba Mbatia autamke WOSIA wake huu kwa nia ya kuepusha machafuko na mvunjiko wa amani hapa nchini, hasa katika uchaguzi ujao; ule Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Oktoba, mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kwa kutamka kwake pale katika Ukumbi wa Karimjee na kwa nafasi ile ni dhahiri Mbatia alitaka kuweka msisitizo wa namna ya kumuenzi Dk. Mengi kwa wanasiasa wote kujitathmini na kutafakari namna ya kuzitawala ndimi zao na matamko yao wakati wa kampeni za uchaguzi.

Ulimi unatoa sumu, ulimi unawasha cheche za moto, ulimi unatia najisi mwili mzima. Mbatia alimalizia kwa kuomba kuwepo maridhiano miongoni mwa wanasiasa. Waweke Tanzania kwanza na vionjo na maono yao baadaye.

Tujifunze kutoka kwa Dk. Mengi ule moyo wake wa unyenyekevu na wa kujali utu wa mwanadamu ndiyo maana alikuwa tayari kujitolea sana kusaidia wanyonge.

Kule Afrika Kusini tulielezwa na tumeona namna wazo la maridhiano alilotoa mzee Nelson Mandela lilivyojenga amani na maelewano ya kudumu. Kulikuwa na uhasama mkubwa sana kati ya wazawa weusi na wakuja weupe – Wazungu. Hali ile sasa imetoweka kwa kiasi fulani, raia wa Jamhuri ya Afrika Kusini wakati huu sisi tunapoomboleza kifo cha mpendwa wetu Dk. Mengi, wao kule ndio wamefanya uchaguzi wao kwa mara ya sita, tena kwa amani na utulivu mkubwa. Ni tunda la maridhiano.

Mbatia aliwasihi Watanzania kwa kusema kuwa namna bora na nzuri zaidi kwa wao kumuenzi mpendwa wetu Dk. Mengi; uwe ni huo moyo wa maridhiano miongoni mwetu na kutawala ndimi zetu.

Hamaki au mihemko kwa mwanadamu inafanya kutamka maneno ya ajabu na pengine yasiyofaa. Ulimi hapo nao unakoroga lugha. Kila mnyama amezaliwa na silka ya unafsi kujifikiria yeye tu. Waingereza wanaita silka hii kwa mwanadamu kuwa “EGOISM”. Lakini Mwenyezi Mungu ametutofautisha binadamu na wanyama wengine kwa kumzawadia mwanadamu kitu kinaitwa “UTASHI”, yaani uwezo wa kuchanganua mema na mabaya.

Hayati Dk. Mengi alijaliwa neema ya kuchagua kutenda mema kwa wenzake. Ndiyo maana alikuwa na unyenyekevu na moyo wa kufikiria wengine. Hii tunaita ni karama (virtue). Kuwa na karama mtu unaweza kuizuia au kutawala ulimi wako.

Hapo mtu unakuwa na tabia za usikivu, utulivu na kuwa tayari kukubali na kuamini kuwa huyu mwenzangu ni mtu kama mimi. Kule kusema “maisha yako kwenye ulimi wa binadamu” alikuwa na nia ya kukumbusha wanasiasa kutokutumia ndimi zao ovyo wasije wakahatarisha maisha ya Watanzania wenzao ambao ni wanadamu kwa wao.

Tujifunze katika somo lile la “Elementary Physics” – ile kanuni inayoitwa “Heat equation”, pale ndipo kumelala wazo la kutoa na kupokea (give and take principle). Kanuni ile inasema hivi kwa Kiingereza: “Heat lost by a hot substance is equal to heat gained by a cold substance.”

Hapo mimi ninaona ndipo ulipo msingi wa maridhiano – utayari wa kutoa na wa kupokea ndiyo utafanikisha maridhiano katika vikao vyovyote vile.

Chondechonde Watanzania, tupokee wosia ule kwa moyo wa uzalendo wa kuitanguliza nchi yetu mbele ya nafsi na vionjo vyetu. Tumuenzi Dk. Mengi kwa hilo. Tutawale ndimi zetu ili kuondokewa vurugu na machafuko ya aina yoyote hapa nchini Tanzania.

Dk. Reginald Mengi apumzike kwa amani.

(Requiescat in pace).