Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa na ya kihistoria ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake ni kuajiri wafanyakazi 186, jambo ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika ufanisi wa taasisi hiyo.

Kihulla ameeleza haya wakati akitoa ripoti ya mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Jijini Dodoma.

Amesema kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Wakala wa Vipimo, idadi ya watumishi imefikia kiwango kinachohitajika ili kuhakikisha utendaji kazi wa taasisi hiyo unafanyika kwa ufanisi wa juu.

Ameongeza kuwa, kati ya wafanyakazi hao, 150 tayari wamepata ajira kamili, huku 36 wakiwa bado wanahitajika katika hatua za usahili. Kihulla alifafanua kuwa, kabla ya kuajiriwa kwa watumishi hawa, Wakala wa Vipimo ulikuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa wafanyakazi, jambo lililokwamisha ufanisi wa kazi.

“Kwa miaka mingi, Idara ya Vipimo ilikuwa na changamoto ya kukosa wataalamu wa kutosha, hali ambayo iliathiri utendaji kazi. Hata hivyo, kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, hali hiyo imebadilika na sasa tuna nguvu kazi inayohitajika,” alisema Kihulla.

Aidha, Kihulla ametaja kuwa historia ya Idara ya Vipimo nchini Tanzania inaanza mwaka 1884 wakati wa utawala wa Kijerumani, ambapo ilianzishwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kuendeshwa na Kamishna wa Vipimo.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Wakala unahitaji nguvu kazi ya kutosha, na kuongeza kuwa, Wakala ya Vipimo inashukuru Serikali kwa juhudi zake za kuhakikisha ajira 186 za kada ya ukaguzi wa vipimo zinapatikana, ambazo zitasaidia kuongeza ufanisi katika uhakiki wa vipimo nchini.

Amefafanua mabadiliko ya idadi ya watumishi tangu mwaka 2021, ambapo kwa mwaka 2021/2022 walikuwa watumishi 2, mwaka 2022/2023 walikuwa 7, mwaka 2023/2024 walikuwa 17, na mwaka 2024/2025 watafikia 186. Hii ni ishara ya hatua kubwa ya maendeleo katika Wakala wa Vipimo.