Madini ya tanzanite yenye thamani ya mabilioni ya shilingi yanadaiwa kutoroshwa kutoka katika mgodi wa TanzaniteOne uliopo Mererani mkoani Manyara.
Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia na kampuni ya Sky Associates Limited na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Wakurugenzi wa Sky Associates Limited ni Faisal Shahbhai, Hussein Gonga, Halfan Hayeshi na Rizwan Ullah. Wamiliki wa TanzaniteOne wana maduka kadhaa yanayojihusisha na biashara ya tanzanite katika Jiji la Arusha. Miongoni mwa maduka hayo ni Prima Gems (T) Ltd, Tanzanite Forever (T) Ltd, na Maruti Gem Store.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la JAMHURI, umebaini, mpango wa kutoroshwa kwa madini hayo ulifanywa Juni 20 na kutekelezwa Juni 21, mwaka huu; huku wahusika wakuu wakitajwa kuwa ni wamiliki wa mgodi huo.
“Kinachofanywa na hawa wamiliki wa mgodi ni kuwa wao wenyewe ndio wanaotorosha madini,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:
“Siku hiyo (Juni 20) mgodini alifika Faisal akiwa na HR Manager (Meneja Rasilimali Watu) [jina tunalo] wakaingia kwenye sorting house (eneo maalum la kuchambua). Baadaye wakafanya kikao na maofisa wa STAMICO na wa TMAA. Inaelekea walikuwa wakipanga mipango ya kufanya siku inayofuata.”

Juni 21, baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa mgodi huo walifika mgodini hapo na kutekeleza mpango wa kuyaondoa madini hayo.
“Walichukua ndoo tano za udongo usiokuwa na madini, wakaingiza sorting house kama vile wanataka kupima kiwango cha madini. Baadaye wakafanya utaratibu wa kuyatoa. Lakini wakati wa kutoa, walitoa madumu sita badala ya tano yaliyoingizwa. Wakapeleka sehemu ya utawala.
“Dumu moja liliwekwa alama nyeusi. Hili ndilo lilijazwa madini yaliyokuwa safi, na ndilo lililotolewa mgodini na kupelekwa mjini Arusha,” kimesema chanzo chetu ndani ya mgodi.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba, aliyebeba dumu hilo na kuliingiza kwenye gari ni mfanyakazi wa TanzaniteOne aitwaye Innocent Solomon. Dumu hilo liliingizwa kwenye gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T710 BWT.

Gari hilo ambalo ni miongoni mwa magari ya kampuni ya TanzaniteOne, dereva wake siku hiyo alikuwa ni Yusuf Mhagama. Gari hilo lilisindikizwa na jingine lililokuwa likiendeshwa na Arafat ambaye ni mdogo wake na Faisal.
JAMHURI limegundua, gari hilo lilichukua shehena hiyo hadi Kituo cha Mafuta cha Panone kilichopo King’ori wilayani Arumeru. Hapo kituoni, dumu hilo lenye tanzanite lilishushwa na kuingizwa kwenye gari jingine aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T492 BSS, na hapo lile jingine lililokuwa limebeba mzigo (T710 BWT) likarejea mgodini Mererani.
Vyanzo vya habari vimelieleza JAMHURI kuwa, awali kabla ya madini hayo kuvushwa kwenye lango la mgodi wa TanzaniteOne, askari polisi aliyekuwa zamu [jina tunalo], alihoji kuhusu mazingira aliyoona hayaeleweki, lakini ghafla akaitwa sehemu nyingine na hivyo akawa ametoa mwanya wa kutoroshwa kwa madini hayo.
“Aliwauliza mbona kuna mzigo unatolewa bila kusindikizwa na askari kama ilivyo kawaida, akapelekwa nyuma ya jengo na ghafla gari likawa limeondoka. Huyu askari anaweza kusaidia kueleza kilichotokea,” kimesema chanzo chetu.

Kamishna Mkuu wa Madini, Benjamin Mchwampaka, ameulizwa kuhusu tukio hilo, lakini amesema hata taarifa zozote.
“Najua pale mgodini wapo TanzaniaOne na STAMICO wakimilikia asilimia 50 kwa 50, STAMICO wako pale (mgodini), mimi sina taarifa labda kama anazo Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini,” amesema Mchwapaka.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma, amezungumza na JAMHURI na kukiri kupata taarifa za utoroshaji wa madini hayo.
“Tulipofuatilia tulibaini kuwa ilikuwa hearsay (habari za kusadikika) tu. Kuna mambo mengi, kila mtu anasema lake. Pale kuna watu wetu wanaofuatilia kuanzia chini kabisa mgodini hadi nje. Watu wetu tulipowauliza kuhusu madai hayo wakatujibu kuwa si ya kweli,” amesema Juma.

Lakini baada ya kuwapo tuhuma hizo za utoshaji madini, Juma anathibitisha kuwa wafanyakazi saba wa madini waliokuwa eneo hilo waliondolewa.
Alipoulizwa kwanini waondolewe kama hawakuhusika na, ama uzembe, au ushirika kwenye utoroshaji shehena hiyo, akasema: “Tulifanya mabadiliko ya watumishi wetu wote pale kwa sababu walikuwa wamekaa muda mrefu eneo hilo. Tulibadili watu wote walioajiriwa kama njia ya mabadiliko ya kawaida.”
Ameongeza kuwa wakati tuhuma hizo zikisambaa, yeye na watendaji wenzake walikuwa bungeni Dodoma. “Kwa kweli kama kuna lolote kwa wakati huo wanaopaswa kuulizwa ni TMAA (Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania).” TMAA ilivunjwa hivi karibuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa TanzaniteOne, Hussein Gonga, ameulizwa na JAMHURI kuhusu utoroshaji madini unaodaiwa kufanywa na wamiliki wa mgodi, lakini hakuweza kukubali wala kukana tuhuma hizo.
“Haya ni masuala ya menejimenti, mimi sijafika mgodini siku nyingi, lakini ndugu yangu haya yote unayoyasikia ni vita…vita vyetu unavielewa. Kumefanyika uchunguzi na kila kitu kiko sawa.
“Siku nyingi sijafika mgodini, vitu vingi vipo. Kwa sasa nipo safarini, lakini nadhani menejimenti au Security Manager (Abuu) anaweza kuelezea suala hili,” amesema.
Kumekuwapo madai mazito kwamba wamiliki wa TanzaniteOne, wamekuwa wakishiriki kutorosha madini, wakitumia mwanya wa udhaifu wa usimamizi wa mamlaka za Serikali.
Inaelezwa kuwa licha ya kufungwa kwa kamera za CCTV, wamiliki wa mgodi huo mara kadhaa wamekuwa wakizizima, jambo linalotia shaka.
JAMHURI limeambiwa kuwa tanzanite nyingi inatoroshwa kupitia mpaka wa Namanga, na viwanja vya ndege vya kimataifa vya Kilimanjaro na Julius Nyerere.
Kenya inatajwa kuwa ndio msafirishaji mkuu wa tanzanite, ilhali madini hayo ulimwenguni kote yakiwa yanapatikana Tanzania pekee.
Taarifa ya Serikali kuhusu kuuzwa kwa mgodi wa TanzaniteOne

Mwaka 2015, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Mhandisi Edwin Ngonyani, alitoa taarifa kwa umma akieleza wamiliki wapya wa mgodi wa TanzaniteOne.
Januari 30, 2015, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alitoa ridhaa ya kuiwezesha kampuni ya Sky Associates Group Limited kuwa Kampuni Mama ya TanzaniteOne Mining Limited (TML) ambayo ni mmiliki mwenza na STAMICO wa leseni ya uchimbaji Na. ML 490/2013 katika mgodi wa tanzanite, ulioko Mererani.
Desemba 5, 2013 STAMICO na TanzaniteOne Mining Limited (TML) walitiliana saini mkataba wa ubia wa asilimia 50 kwa 50 katika umiliki wa leseni hiyo namba ML 490/2013 inayohusisha eneo la Kitalu C la Mererani.
Kifungu Namba 110 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kinamruhusu Waziri anayehusika na sekta ya madini kuridhia mabadiliko ya umiliki wa hisa katika kampuni yenye leseni za madini ikiwa mabadiliko husika yanampa anayeingia nguvu ya kutoa uamuzi (control) katika shughuli za kampuni.

Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited inamilikiwa kwa asilimia 100 na kampuni ya Afrika Kusini ya TanzaniteOne (SA) Proprietary Limited. Kampuni hiyo ya Afrika Kusini ilikuwa ikimilikiwa kwa asilimia 100 na kampuni ya Richland Resources iliyosajiliwa kwenye soko la hisa la Uingereza, kabla ya hisa zake zote kuuzwa kwa kampuni ya Sky Associates Group Limited.
Novemba 26, 2014, kampuni ya Richland Resources Ltd iliuza maslahi yake katika kampuni hiyo ya TML kwa kampuni ya Sky Associates Group Limited ‘’Sky Associates’’ kwa masharti ambayo ni upatikanaji wa idhini za mamlaka na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini.

Maombi ya kutaka ridhaa ya Waziri yaliwasilishwa na kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited ya Mererani, na kabla ya kukubaliwa Wizara ilitaka kujiridhisha na uhalali ikiwa ni pamoja na kampuni ya Richland Resources Ltd kuwasilisha uamuzi wa bodi yake ulioiruhusu kuuza asilimia 100 ya hisa zake kwa kampuni ya TanzaniteOne (SA) Proprietary Limited kwenda Sky Associates Group Limited.
Awali, katika taarifa yao, Richland Resources Ltd walieleza sababu za kujitoa ama kuuza hisa zao za kampuni mama ya TML inayoitwa TanzaniteOne SA ya Afrika Kusini ni pamoja na kwamba mgodi ulikuwa unaendeshwa kwa hasara kutokana na mazingira ya kuvamiwa na wachimbaji wadogo kutoka Vitalu B na D bila msaada wa ulinzi kutoka serikalini pamoja na wizi unaofanyika katika mgodi huo.
Baada ya mauziano hayo kufanyika, wanahisa wa Kampuni ya Sky Associates walifanya kikao na STAMICO Novemba, 2014 cha kujitambulisha kama wamiliki wapya watarajiwa wa TML na kuahidi kuboresha maeneo mbalimbali ya mgodi na kudhibiti wizi na uvamizi katika Kitalu C, ili kuhakikisha kwamba biashara ya tanzanite inanufaisha wabia na Taifa kwa ujumla.

Wakati wa kikao hicho cha Novemba, 2014 STAMICO ilipata fursa ya kufahamishwa kuwa uuzwaji huo unahusisha pia mali zote za TML zilizoko kwenye mgodi na pia kampuni ya Urafiki Gemstone EPZ.
Mauziano hayo yanahusu Richland Resources kulipwa US$ 5.1 milioni na kuchukuliwa madeni yote ya TML (Dola za Marekani 13.4 milioni) na TanzaniteOne (SA) Proprietary Limited (Dola za Marekani 3.6 milioni pamoja na riba Dola za Marekani 0.4 milioni) na Sky Associates pamoja na kurithishwa mkataba wa ubia kati ya STAMICO na TML.
Kampuni ya TML kama operator imekuwa ikiendelea na shughuli za uchimbaji kama kawaida pamoja na wafanyakazi wake.
STAMICO wanasema: “Kwa lugha rahisi, kampuni ya Richland Resources Limited imeiuza kampuni yake ya TanzaniteOne (SA) Proprietary Limited kwa kampuni ya Hongkong kwa bei ya jumla takriban US$ 22.5 milioni.” Hata hivyo, madai haya yanapingwa na wadau wengine.

Sehemu ya taarifa yao inasema, “kwa kuwa Waziri amesharidhia mabadiliko haya ya umiliki wa leseni ya Uchimbaji, STAMICO inatarajia kuanza majadiliano na mwanahisa mwenza mpya wa Kampuni ya Sky Associates, ili kuboresha mkataba wa ubia wa kumiliki Leseni ya Mererani kwa madhumuni ya kubainisha na kuongeza manufaa zaidi kwa STAMICO na kwa Watanzania kwa ujumla,”.
Katika maeneo yaliyokubalika kuboreshwa kwenye mkataba na mbia huyo mpya ni pamoja na:
a) Kuuza madini ya tanzanite kwa wazawa kwanza ili kukidhi soko la ndani.
b) Kulipa STAMICO kwa wakati ada ya usimamizi (management fees) ya asilimia 2.5 ya mauzo yote pamoja na kumaliza madeni yote ya nyuma.
c) Kuongeza uwazi katika mauzo kwa kuhusisha STAMICO kwa asilimia 100 katika hatua zote za uchambuzi (sorting) mpaka kuuza.
d) Kuongeza thamani ya madini ya tanzanite kabla ya kuuza ambayo inasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania.
e) Kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mgodi. Kutokana Kampuni kumilikiwa kwa sehemu kubwa na wawekezaji wazawa ambao wanajua njia zote zinazotumika katika kuhujumu mgodi huo ni dhahiri kwamba wanaingia katika mgodi huu wakiwa wamejidhatiti vya kutosha kudhibiti wizi huo. Wanalenga pia kutumia teknolojia mpya ya sensors na kufunga CCTV cameras chini ya mgodi.
f) Kusimamia utawala bora katika mgodi na kuheshimu makubaliano ya awali yaliyosainiwa kati ya STAMICO na TML.
g) Kuitangaza tanzanite duniani na kuonesha kuwa madini haya chimbuko lake ni Tanzania na hazina ya nchi hii.
h) Kutengeneza mazingira ya mgodi kuwa kivutio cha utalii na mafunzo.
i) Kuboresha maisha ya jamii inayozunguka mgodi kwa kujenga zahanati pamoja na kukarabati shule zilizopo eneo la mgodi na kuwa za kisasa.
j) Kupanda miti 1,400 katika maeneo ya mgodi ili kutunza mazingira.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa STAMICO itasimamia kwa uangalifu mkubwa hatua ya uboreshaji masharti ya mkataba na Kampuni hiyo ya Sky Associates, kama yalivyoainishwa hapo juu ili kuleta mabadiliko ambayo yataleta matokeo chanya katika udhibiti na uendelezaji wa mgodi na biashara nzima ya Tanzanite kwa manufaa ya Taifa.
“Hatua inayofuata kwa upande wa Sky Associates ni kulipa kodi za capital gain pamoja na stamp duty na kupata hati ya kutodaiwa kodi (Tax Clearance Certificate) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuipeleka Wizara ya Nishati na Madini, ili Wizara iweze kujiridhisha kuwa kampuni hiyo ni safi na haina madeni ya kodi,” inasomeka sehemu ya taarifa rasmi ya Serikali.
Kampuni hiyo ilitakiwa kulipa madeni iliyoyarithi ikiwa ni pamoja na deni la mrabaha kwa Serikali na pia itawajibika kuwasilisha Certificate of Compliance kwa Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) itakayoidhinisha uhalali wa kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini ikiwa itataka kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo.
Sehemu ya makubaliano mengine ilikuwa ni; katika kipindi hiki cha mpito, Kampuni ya Sky Associates ishirikiane na Chama cha Wachimbaji wa Wadogo wa Tanzanite Mererani (MAREMA) kuunda kamati ya kutatua migogoro mikubwa iliyokuwepo mwanzo kati ya TML na wachimbaji wadogo.

Hatua ya ushirikiano huo imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa wizi na uvamizi uliokuwa unafanywa na wachimbaji holela kutoka vitalu B na D waliokuwa wakiingia Kitalu C ambako ni nje ya mipaka ya maeneo waliyoruhusiwa kuchimba. Kitalu C kina jumla ya mashimo (shafts) saba (7) yaliyoandaliwa kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
“STAMICO itaendelea kusimamia kwa karibu maslahi yake katika ubia wa umiliki wa leseni na Kampuni ya TML. Pamoja na uboreshaji wa vifungu vya mkataba na mbia huyo mpya, STAMICO itaendelea kuweka wafanyakazi wake katika timu ya pamoja ya uangalizi na usimamizi (Monitoring and Evaluation Unit) wa mgodi huo ili kusimamia uzalishaji wa Tanzanite.
“Timu hii ina jukumu la kufuatilia mwenendo wa uzalishaji pamoja na utekelezaji wa masharti ya mkataba wa ubia. Utaratibu huu ni endelevu na tayari umeonesha mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa wizi wa ndani.
“Kwa niaba yangu binafsi, Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO, Menejimenti na Wafanyakazi, nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati Ofisi za Madini zaKanda ya Kaskazini, Polisi, kampuni ya ulinzi ya Nguvu Moja na wawakilishi wa STAMICO na TML kwa kufanikisha operesheni ya kudhibiti wachimbaji holela waliokuwa wakivamia katika kitalu C cha uzalishaji wa Tanzanite,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Serikali.
Taarifa zaidi zinaonesha kuwa, operesheni hiyo ambayo ni endelevu hadi kufikia Desemba 31, 2014 iliwezesha kukombolewa kwa asilimia 95 ya maeneo ya mashimo ya uchimbaji ya Investor, CT na Delta shafts yaliyokuwa yamevamiwa na wachimbaji wadogo.

Kazi kubwa iliyobaki ni kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyokombolewa ili kuzuia uvamizi kujirudia, na kuyakomboa maeneo yaliyobakia chini ya himaya ya wavamizi. Shirika hilo lilitakiwa kuhakikisha linadhibiti aina yoyote ya mianya ya wizi ya ndani inayoweza kufanywa na wafanyakazi na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na wizi katika Mgodi wa Tanzanite wa Mererani.
Mgodi umeendelea kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 600 na ajira hizo zinatarajiwa kuongezeka zaidi mara baada ya kufunguliwa kwa mashimo mengine ya uchimbaji. Idadi ya watanzania wanaoshikilia nafasi za juu za Menejimenti ya mgodi imeendelea kuongezeka na kufikia 11, wakati waajiriwa kutoka nje ya nchi kwa sasa ni wanne tu. Vijana 22 zaidi wameajiriwa katika Kitengo cha kuongeza thamani ya madini.
Pamoja na kwamba sio kawaida kuchambua undani wa kampuni ya Sky Associates Group Limited iliyosajiliwa katika nchi ya British Virgin Islands na kufanya kazi zake nchini Hongkong, nimeonelea niwafahamishe kuwa wamiliki wa kampuni hiyo kwa sasa ni Faisal Juma Shahbhai (asilimia 25 ya hisa zote) na Hussein Omarhajji Gonga (asilimia 35 ya hisa zote) ambao ni raia wa Tanzania wenye makazi yao jijini Arusha; pamoja na Bwana Rizwan Ullah (asilimia 40 ya hisa zote) ambaye ni raia wa India mwenye makazi yake jijini Hongkong.

>>ITAENDELEA…