Na Mwandishi Wetu, Helsinki, Finland

Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Misitu ya nchini Finland zinakamilisha mradi mpya wa kuboresha sekta ya misitu ili kuipa thamani sekta hiyo kuwa ya kibiashara zaidi kutokana na uzoefu wa Finland.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 7, 2024, jijini hapa wakati wa kikao cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, na pacha wake katika sekta ya Misitu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Misitu nchini Ufini (Finland), Bw. Pekka Pesonen.

Dkt. Abbasi amesema Sekta ya misitu imekuwa chanzo kikubwa cha ajira na Pato la Taifa la Finland ambapo kwa takwimu za mwaka 2022 sekta hiyo iliingiza jumla ya Euro Bilioni 20 katika uchumi wa Ufini hivyo Tanzania ina mengi ya kujifunza.

Ufini ambayo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kusaidia sekta ya misitu nchini Tanzania ukiwemo Mradi wa Forvac uliomalizika hivi karibuni uliochagiza ajira 500,000 katika sekta hiyo, sasa iko tayari kusaidia mradi mwingine mpya kuendeleza mageuzi hayo.

“Kutokana na uzoefu wa wenzetu katika biashara ya sekta ya misitu tayari tumekubaliana na tunakamilisha taratibu za kuanza mradi mwingine mpya ambapo Finland itaisaidia Tanzania Euro milioni 20 kuchagiza mageuzi zaidi kuifanya sekta ya misitu kuisaidia Tanzania,” alisema Dkt. Abbasi mara baada ya mkutano huo.

“Nimefurahia uzoefu mkubwa ambao tumejadiliana na kupeana leo. Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania na sisi pia kuchukua uzoefu wenu katika kusimamia misitu hasa ya serikali kwani hapa sisi uzoefu wetu mkubwa ni misitu ya sekta binafsi,” alisema Katibu Mkuu huyo wa Ufini.

Awali kabla ya kukutana na Katibu Mkuu huyo, Dkt. Abbasi na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Kusimamia Sheria za Misitu na pia Muungano wa Wazalishaji wa Kilimo na Wamiliki wa Misitu (MTK) wenye wanachama 600,000.

Dkt. Abbasi ameongoza ujumbe wa wataalamu ambao ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Deusdedit Bwoyo na Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Prof. Dos Santos Silayo.

Ufini ndio nchi inayoongoza Barani Ulaya kwa kuwa na eneo lenye misitu mingi, sehemu kubwa (asilimia 60) ikimilikiwa na sekta binafsi na asilimia kubwa inayobaki ikiwa chini ya umma ikisimamiwa na kampuni binafsi ya Serikali ya Forestry LTD.