Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kubuni mazao mapya ya Utalii ili kuwavutia watalii huku ikisisitiza kwamba inatamani watalii wanaotoka Zanzibar kwenda kutalii katika eneo la Mapango ya Amboni yaliyopo jijini Tanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ametoa wito huo leo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua mradi wa ujenzi wa lango la kuingilia katika eneo la Mapango.

Mhe. Mnzava aliongeza kuwa uboreshaji wa lango la kuingia katika eneo hilo uendane na kasi ya kuongeza mazao mengine ya Utalii katika eneo hilo.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Mnzava ameitaka Wizara hiyo kuja na mpango mkakati wa kuongeza mazao ya Utalii katika eneo hilo.

” Tanga ipo karibu na Unguja na Pemba na maeneo yale yanasifika kwa kuwa na vivutio vya Utalii, tunataka watalii wale wakitoka Zanzibar waje Tanga kisha waende kwenye maeneo mengine” amesisitiza Mhe. Mnzava.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea Miradi hiyo na kwamba Wizara yake itaenda kufanyia kazi mapendekezo ya kamati.

“Kamati imetushauri mambo mengi lakini kubwa ni kuongeza mazao ya Utalii katika Jiji letu la Tanga kama zip lining, campsite katika eneo la Amboni” alisema Mhe. Chana lakini utalii wa kutembelea msitu wa Mikoko katika eneo la Sahare”

Mhe. Chana alitumia fursa hiyo kuwaomba wawekezaji kuwekeza katika hifadhi za misitu kama ambavyo wanavyowekeza katika hifadhi za Wanyama.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ipo Jijini Tanga kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo leo imetembelea Mradi wa ujenzi wa Lango la kuingilia katika Mapango ya Amboni na Hifadhi ya Mikoko ambapo katika eneo Hilo Kuna Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Utalii.