Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewasilisha makadirio ya bajeti ya shilingi trilioni 1.77 kwa ajili ya utekelezaji vipaumbele tisa vyenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja, vivuko, mizani, ukamilishaji viwanja vikubwa vya ndege.
Amesema kati ya kiasi hicho cha fedha, sh. bilioni 81.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. Trilioni 1.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Hayo aliyasema bungeni jana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo alisema katika mwaka huo wa fedha, Wizara inatarajia kutekeleza Mpango na Bajeti kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Mpango Mkakati wa Wizara (2021/22 – 2025/26), Ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Bashungwa alisema Wizara imeandaa Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 kwa kuzingatia vipaumbele 9.