Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amebainisha vipaumbele nane vya Wizara ya Ujenzi itakavyotekeleza katika bajeti mwaka 2024/25.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara na taasisi zake kwa mwaka 2024/25, Bashungwa amesema bajeti itazingatia kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja iliyoharibiwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya.
Bashungwa amesema pia kuendelea na utekelezaji wa miradi inayoendelea ambayo ni pamoja ujenzi wa barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi na miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa kama vile Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma.
Ameeleza ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, zinazounganisha na nchi jirani kwa kiwango cha lami pamoja na barabara za ulinzi, usanifu wa barabara mpya hasa mijini, miradi ya kimkakati ikiwemo kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.
Amesema pia, mradi ya udhibiti wa uzito wa magari, ujenzi na ukarabati wa vivuko kupitia TEMESA na miradi ya nyumba na majengo ya Serikali kupitia TBA.
Bashungwa amesema kipaumbele kingine ni kuendelea na matengenezo ya barabara Kuu na za Mikoa kuhakikisha zinapitika majira yote ya mwaka na kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kwa lengo la kuongeza wataalam wabobezi wa ndani ili waweze kusimamia miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini.
Amesema pia kufanya mapitio ya Sera ya Ujenzi (2003) na Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani (2009) pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali inayohusiana na Sekta ya Ujenzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na tabianchi;
Pia kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi, kutumia teknolojia za gharama nafuu katika ujenzi wa barabara hususan katika maeneo korofi na kutekeleza Mkakati wa Uimarishaji wa Utendaji kazi wa TEMESA.