Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kufikisha gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia,kupeleka nishati vijijini, ikiwemo katika vitongoji; kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwemo mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG Project) na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP).
Hayo yamesemwa leo Aprili 24,2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Dkt.Biteko amesema kuwa wizara itaendelea kutekeleza na kusimamia shughuli za utafutaji na uendelezaji katika vitalu vya kimkakati na wawekezaji; usambazaji wa gesi asilia viwandani, katika taasisi na majumbani na kuimarisha matumizi ya CNG katika magari.
“Tutaendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking) nchini pamoja na upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini kupitia uanzishwaji wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo. “amesema Dkt.Biteko
Aidha amesema kuwa watahakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja na ufanisi katika kushughulikia upatikanaji wa bidhaa hizo; kuimarisha uwekezaji na ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Pia tutaendelea kuimarisha utoaji wa huduma, tija na ufanisi katika uendeshaji wa Taasisi/Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya TANESCO, TPDC, EWURA, PURA na PBPA pamoja na Kampuni Tanzu. Wizara pia itaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia pamoja na rasilimali watu ya Wizara ya Taasisi zake na upatikanaji wa vitendea kazi muhimu.
“Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2024/25 pamoja na mambo mengine, umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) 2021/22 – 2025/26, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Maagizo ya Viongozi wa Kitaifa katika Sekta ya Nishati, Mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2024/25 pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26). “amesema
Amesema kuwa miongozo mingine iliyozingatiwa ni Sera, Mikakati na Programu mbalimbali za Kisekta na Kitaifa pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya mwaka 2030 kuhusu masuala ya nishati.