πŸ“Œ Uzalishaji umeme waongezeka kwa asilimia 59.9

πŸ“Œ Misheni 300 kuongeza upatikanaji umeme kwa asilimia 100 ifikapo 2030.

πŸ“Œ Serikali yaokoa sh.i bilioni 58.4 kwa kuunganisha Kigoma na gridi ya Taifa.

πŸ“Œ Upatikanaji bidhaa za mafuta umeendelea kuwa wa uhakika

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametaja mafanikio yaliyopatikana katika Wizara kwa mwaka 2024/2025 mojawapo ikiwa ni kuimarika kwa uzalishaji wa umeme.

Akiwasilisha mafanikio hayo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Njshati na Madini, leo jijini Dodoma, Mhe. Kapinga amesema nchi inakidhi mahitaji ya umeme kwa ongezeko la megawati 3,796.71 mwezi Februari, 2025 ikilinganishwa na Megawati 2,372.96 zilizokuwepo mwezi Julai, 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 59.9 huku mahitaji yakiongezeka kwa asilinia 13.34.

β€œMheshimiwa Mwenyekiti kama nchi tunakidhi mahitaji ya upatikanaji wa umeme na tunaendelea kuimarisha sehemu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme huku Mradi wa Julius Nyerere ukifikia asilimia 99.8”. Amesema Mhe. Kapinga

Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu alisema kuwa katika mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa, megawati 2,481.27 sawa na asilimia 65.4 ni za maji.

β€œMegawati 1,198.82 sawa na asilimia 31.6 ni gesi asilia, megawati 101.12 sawa na asilimia 2.6 ni mafuta, megawati 5 sawa na asilimia 0.1 ni umeme wa jua na Megawati 10.5 sawa na asilimia 0.3 ni umeme utokanao na tungamotaka.” Aliongeza Lyatuu.

Amesema mahitaji ya umeme nchini yameendelea kuongezeka hadi megawati 1,908.15 zilizofikiwa Februari 20, 2025 kutoka megawati 1,683.57 zilizofikiwa
Julai 15, 2024 ambalo ni ongezeko la asilimia 13.34 ambalo linaonesha mahitaji ya juu ya umeme kuanzia mwezi Julai, 2024 hadi mwezi Februari, 2025.

Kuhusu mafanikio ya mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati (African Heads of State Energy Summit) uliofanyika Januari 27-28, 2025 jijini Dar es salaam Lyatuu amesema kupitia mkutano huo ulizinduliwa mpango ambao unalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kutoka cha sasa cha asilimia 78.4 hadi kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

Amesema mpango huo utasaidia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini kutoka asilimia 46 hadi kufikia asilimia 75 katika kipindi hicho.

Katika hatua nyingine amesema Serikali inaokoa takribani shilingi bilioni 58.4 kwa kuunganisha Mkoa wa Kigoma na gridi ya Taifa hivyo kuwawezesha wananchi wa mkoa huo kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wa umeme Vijijini amesema Serikali imeunganisha umeme katika Vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara na
vitongoji 33,657 kati ya 64,359 ambayo ni sawa na asilimia 52.3 vimeunganishiwa umeme.

Ameeleza kuwa, hatua za kupeleka umeme katika vituo vya afya, pampu za maji, maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini, viwanda na kilimo katika maeneo ya vijijini zinaendelea.

Amesema maeneo ya migodi yameendelea kufikishiwa umeme na mradi ulianza kutekelezwa mwezi Aprili 2023 kwa gharama ya shilingi bilioni 115.

Ameongeza kuwa, nchi imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli.

Ameeleza kuwa Serikali imetoa leseni ya uendelezaji wa Kitalu cha kuzalisha gesi asilia cha Ntorya kwa Kampuni ya ARA Petroleum. Kitalu hicho kina hazina ya gesi asilia ya futi za jazo Trilioni 1.64 na hivyo uzalishaji utakapoanza utaimarisha upatikanaji wa gesi asilia nchini kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha umeme, viwandani n.k