Serikali inaweka nguvu katika sekta ya maji ili kuhakikisha wananchi katika maeneo yote ya nchi wanapata huduma ya maji safi, salama, ya uhakika na yenye kutosheleza.

Wajibu huu wa serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kwa Watanzania wote, bila kubagua itikadi au eneo. Aidha, sera ya maji ya mwaka 2002 inaelekeza wananchi kupata huduma ya maji safi na salama ndani ya umbali wa mita 400.

Sera hii ya Serikali ya CCM katika sekta ya maji imenuia kumuondolea adha mwananchi kwenda umbali mrefu kutafuta maji, lakini pia kumfikishia huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza karibu na makazi yake kwa nia ya kumuwezesha kuwa na muda wa kutosha kushiriki shughuli nyingine za maendeleo na kutumia maji kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali katika kujenga uchumi wa nchi.
Hatua hizi zinazoendelea kuchukuliwa na zilizokamilika ni darasa tosha na jibu la kampeni za uchaguzi uliofanyika mwaka 2015, ambapo wananchi wengi waliipa dhamana CCM ya kuongoza nchi. Wakati wa kampeni hizo mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, ambaye pia alishinda kwa ushindi wa kutosha, Rais Dk. John Magufuli, alisisitiza jambo la msingi atakalozingatia ni umuhimu wa kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa kuahidi “Kumtua mama ndoo kichwani.”
Ni wazi kuwa serikali ipo kwa ajili ya wananchi na inawajali. Maji hayana mbadala, hivyo sekta ya maji ni moja kati ya masuala ambayo yamepewa kipaumbele katika kuwaondolea kero kina mama na wananchi wote, ambao wengi wao hutumia muda mrefu katika maeneo ya vijijini, pia mijini kuhakikisha maji kwa matumizi ya familia yanapatikana.

Kwa serikali kufikisha huduma ya maji karibu na makazi, hakika kina mama pamoja na wananchi wapenda maendeleo watajikita zaidi katika kazi nyingine, kwa kupata muda wa kutosha kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha.

Uwekezaji wa serikali katika sekta ya maji utaondosha adha zilizokuwa zikisababishwa na magonjwa mbalimbali yanayotokana na maji yasiyo salama na muda uliokuwa ukitumika kuhudumia mgonjwa.
Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa ambayo baadhi ya maeneo yake yana changamoto ya maji. Hili limesababishwa na baadhi ya vyanzo vya maji kukauka kutokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi.
Hali hii husababisha baadhi ya wananchi katika maeneo ambayo uharibifu umefanyika kutumia muda mrefu kutafuta maji kutokana na ukweli kuwa tayari kuna upungufu wa rasilimali maji.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, anasema serikali imejizatiti kupitia  Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili, kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 ya wakazi wa vijijini wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosheleza.
“Tumewekeza fedha nyingi sana katika miradi ya maji nchini, Mkoa wa Kagera ukiwa ni mmojawapo na mfano halisi ni mradi mkubwa wa maji wa Bukoba mjini wenye thamani ya takriban Sh bilioni 31, pamoja na miundombinu bora na ya kisasa. Mradi ambao una uwezo wa kuzalisha lita za maji milioni 18 kutoka katika kituo chake cha uzalishaji cha Bunena, wakati mahitaji halisi kwa wakazi wa Manispaa ya Mji wa Bukoba ni lita za maji milioni 13,” Naibu Waziri wa Maji, Aweso, anasema.

Waziri Aweso kutokana na hatua hii,  anaipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kwa usimamizi mzuri wa miradi na juhudi za kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.

Sambamba na hilo, anamtaka Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA, Mhandisi Allen Marwa, kuhakikisha mtandao wa maji safi unaongezwa kwa kupeleka maji safi katika maeneo yote ya manispaa ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.
Mhandisi Marwa akizungumzia mradi huo, anasema kuwa umefadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IFD), Kampuni ya TECHNOFAB ya nchini India pamoja na serikali. Hivi sasa mradi huu unazalisha lita za maji milioni 9.5 na unahudumia kata 10 kati ya 14 zilizopo katika Manispaa ya Mji wa Bukoba. Kata nne zilizobaki za Nyanga, Kahororo, Ijuganyondo na Buhembe ni miongoni mwa maeneo ambayo yatanufaika baada ya mtandao wa mradi kuongezwa.
Hata hivyo, Naibu Waziri Aweso ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya tathmini za kina na kutoa zabuni za kandarasi kwa miradi ya maji kwa wale wenye uwezo kifedha, rasilimali watu yenye sifa zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi ya sekta ya maji na vifaa. Hatua hii itawezesha kukamilishwa kwa miradi ya maji katika kiwango na kuepuka ubabaishaji.
Waziri Aweso anafafanua kuwa ni lazima halmashauri zifanye utafiti wa kutosha kuhusu makandarasi kabla ya kuwapa kazi na si kwa kujuana, ili kumaliza tatizo la kusuasua kwa miradi. Anaongeza kuwa hatua stahiki zichukuliwe kwa makandarasi wote wababaishaji, ikiwemo kutowapa kazi tena.

Kuhusu utunzaji wa miradi ya maji, akiwa katika mradi wa maji wa Kaisho – Isangiro, Naibu Waziri Aweso anasema wote wanaohujumu miradi ya maji lazima wakamatwe na hatua stahiki zichukuliwe kwa kuhujumu miradi iliyofanikishwa kwa fedha za wananchi. Ameongeza kuwa watendaji watoe elimu zaidi kwa wananchi kuhusu kulinda na kutunza vyanzo na miundombinu ya maji kote nchini ili miradi inayotekelezwa na serikali iwe na tija kwa kila mwananchi.

 

Weledi katika miradi ya maji

Kuhusu makandarasi, Aweso anasema baadhi yao wanashindwa kusimamia weledi na kuwa wababaishaji katika usimamizi wa miradi ya maji katika maeneo yao. Hali hii inasababisha baadhi ya miradi kukwama kutokana na uzembe. Anawataka wahandisi wa maji kote nchini waipende nchi, wapende kazi yao na watatue shida ya maji kwa wananchi, kwani elimu yao ni kwa faida ya wote.
Waziri Aweso anasema amekagua miradi ya maji ya Katoke, Nyakahura, Kaisho – Isingiro, hasa kwenye Wilaya ya Misenyi na amebaini mambo yasiyo sawa, weledi haujasimamiwa ipasavyo kwa wahandisi. Mfano, mradi wa maji Katoke, wilayani Muleba ambao unatekelezwa na mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Sagack Investment Co. Ltd aliyekwishalipwa shilingi milioni 404 kati ya milioni 476 lakini bado mradi haujaanza kutoa maji na kuagiza Mhandisi wa Maji wilayani Muleba, Boniface Lukoo, kukamatwa na kufikishwa polisi na mkandarasi kutafutwa ili ufanyike uchunguzi kuhusu kukwama kwa mradi huo.
Mwingine anayechukuliwa hatua kwa kusimamishwa kazi ni Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Biharamulo, Patrice Jerome, baada ya kubainika katika ukaguzi kuwa mradi wa maji wa Nyakahura uliogharimu takriban shilingi bilioni 30 hautoi maji, huku wananchi wakiendelea kusubiri.
Aidha, kwa kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Misenyi, Aweso alimtaka Mhandisi wa Maji wilayani hapo, Abdallah Gendaheka, aliye masomoni kufika ofisi za wizara, Dodoma, kutoa maelezo kuhusu mradi wa maji wa Bugango uliogharimu shilingi milioni 830, huku mkandarasi akiwa amekwisha kulipwa shilingi milioni 781 wakati mradi hautoi maji.
Aidha, akiwa wilayani Kyerwa alikutana na malalamiko kuhusu miradi ya Kaisho – Isingiro, Itera na Ruberwa kutoka kwa wananchi kutokana na ujenzi duni wa miradi hiyo kwa sababu ya uwezo mdogo wa mkandarasi.

Wakazi wa Kyerwa wapatao 321,026 ni asilimia 57 wanaopata huduma ya maji safi na salama.
“Haiwezekani serikali itumie fedha nyingi katika miradi ya maji bila kuwa na tija, jambo hili halikubaliki. Ni lazima tuchukue hatua kwa wataalamu wote wazembe ambao wanataka kutukwamisha lengo letu la kumaliza tatizo la maji nchini,” Naibu Waziri Aweso anasema na kutoa onyo kwa wataalamu wote katika sekta ya maji.
Katika ziara hiyo mkoani Kagera, Naibu Waziri Aweso, ametembelea miradi ya maji inayotekelezwa ya Ihungo, Ibwera, Kibirizi, Bulembo, Kayanga mjini, Kaisho – Isingiro, Rubwera, Muhweza – Murugarama, Nyakahura, Biharamulo mjini unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi ya mji mdogo wa Biharamulo (BILUWASA) na Katoke, pamoja na mradi mkubwa wa Bukoba mjini ulio chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Bukoba (BUWASA).

Waziri Aweso pia ametumia ziara ya kukagua miradi kwa kuzindua miradi mitatu ya maji ya Ibwera, Kibirizi na Bulembo, ambapo miradi ya Ibwera na Kibirizi ni miongoni mwa miradi ya vijiji 10 vilivyopewa kipaumbele na serikali inayotekelezwa chini ya Programu ya Maji Vijijini (RWSSP) iliyoanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2013/2014. Mradi wa Maji Kibirizi ukiwa umegharimu shilingi zaidi ya milioni 527, ukinufaisha wananchi 7,200.

Mradi wa Maji wa Bulembo, uliopo katika Kata ya Mshasha, wilayani Misenyi umefadhiliwa na Shirika la World Vision na  kugharimu shilingi zaidi ya milioni 158 na unahudumia kaya 270 katika vitongoji vinane.
Akitoa shukrani zake za dhati kwa Naibu Waziri wa Maji kwa niaba ya wananchi, Mweyekiti wa Kijiji cha Ibwera, Idd Mohamed, anasema mradi wa maji kijijini hapo umekuwa faraja kubwa kwa wananchi baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kwa kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Mhandisi wa Maji Mkoa wa Kagera, Avitus Exavery, anasema kulingana na takwimu za mkoa huo kwa sasa asilimia 64.7 ya wakazi 2,458,023 waliopo vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama. Na asilimia 64.6 katika miji mikuu ya wilaya na asilimia 88 ya wakazi wa Manispaa ya Mji wa Bukoba wanapata huduma ya maji safi na salama.
Exavery anasema zaidi ya vijiji 30 katika Wilaya ya Karagwe vitanufaika na mradi wa maji utakaohudumia mji wa Kayanga ambao chanzo chake ni Ziwa Lwakajunju, utakaogharimu shilingi milioni 70. Anaongeza kuwa wilayani Kyerwa zaidi ya vijiji 52 vitanufaika na mradi wa maji kutoka Ziwa Rushwa utakaogharimu shilingi bilioni 1.5. Zabuni kwa ajili ya kumpata mtaalamu mshauri itatangazwa karibuni, kwa ajili ya kufanya usanifu wa miradi yote miwili inayotekelezwa ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili.
Mhandisi Exavery anasema utekelezaji wa miradi ya maji ya Kabalenzi – Kanazi na Muhweza – Murugarama inaendelea wilayani Ngara na itakapokamilika itainua hali ya kiwango cha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ngara ambayo kwa sasa ni asilimia 63.