Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Maji imeikabidhi Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), hundi la shilingi milioni 20 kwaajili ya matibabu kwa watoto wenye changamoto mbalimbali za magonjwa ya moyo.
Hundi ya fedha hizo ilikabidhiwa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Angela Muhozya.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hundi hiyo, Katibu Mkuu Mwajuma, alisema ziara hiyo ni sehemu ya shamrashamra za wiki ya maji inayofanyika kila mwezi wa tatu kila mwaka.

“Sisi tunatambua ukubwa wa tatizo la moyo kwasababu hata sisi hivi karibuni tulimpoteza mfanyakazi mwenzetu ambaye alifariki ghafla mkoani Dodoma kwa hiyo tukisikia mtu anachangamoto ya moyo tunapata hisia kuhusu tatizo hilo,” alisema
Alisema Wizara ya Maji imeandaa utaratibu ambapo wafanyakazi wake watakuwa wakifika kwenye taasisi hiyo kwaajili ya kufanya vipimo vya moyo ili watakaobainika kuwa na tatizo watibiwe mapema.
Alisema waliamua kuweka utaratibu huo wa kupima afya mara kwa mara baada ya kubaini kuwa kuna watumishi wengi wanaosumbuliwa na moyo ambao wakipima mapema watatibiwa na kuokoa maisha.

Alisema Wizara ya Maji kupitia taasisi zake itaendelea kukusanya fedha kwaajili ya kusaidia watoto na watu wazima wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo maeneo mbalimbali nchini.
“Nimeambiwa kwamba mnapanga kuongeza idadi ya wataalamu wa moyo hilo ni jambo jema sana kwasababu ongezeko hilo litakuwa msaada mkubwa kwasababu watu wenye matatizo watatibiwa kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa,” alisema
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Angela Muhozya alishukuru Wizara hiyo kwa msaada huo na kuomba wadau wengine waige mfano huo kwani wahitaji wa matibabu ya moyo wako wengi.
Alisema huduma za moyo bado hazijafika kwenye maeneo mbalimbali nchini na kuongeza kuwa watoto wanaohitaji matibabu ya moyo wamekuwa wakigundulika wakiwa wamechelewa.

“Ndiyo maana tumeanzisha huduma yakwenda mikoa mbalimbali kila mwezi kutoa huduma za upimaji na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya mikoani ili waweze kugundua tatizo mapema ili wawahishwe JKCI watibiwe haraka,” alisema
Aidha, alisema wagonjwa wengi wanaowachukua kutoka mikoani wanakuwa wanahitaji huduma ya kibingwa ya upasuaji wa tundu dogo na tundu kubwa tiba ambayo gharama yake iko juu kutokana na vifaa vinavyotumika kwenye matibabu hayo na dawa.
“Matibabu ni gharama kubwa kwa hiyo tukipata wadau wakutusaidia kama nyinyi tunafurahi sana kwasababu wagonjwa wengi wanatoka familia za kipato cha chini sana kwa hiyo wakipata matibabu mapema wanakwenda kuendelea na kazi zao kama kawaida za kuzalisha uchumi,” alisema
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Stella Mongella alisema idadi kubwa ya watoto wanazaliwa wakiwa na shida kwenye moyo yakiwemo ya kuzaliwa nayo kama matundu, mishipa kubana na mishipa kuvurugika.

Alisema maradhi hayo yanaweza kumpata mtoto aliyetumboni kama mama mjamzito atapata shinikizo la damu na sukari kuwa nyingi pamoja na maambukizi mengine ya virusi mbalimbali.
“Zaidi ya matatizo ya kuzaliwa nayo mtoto anaweza kupata maradhi haya ukubwani kama moyo kuwa mkubwa na dalili ya mtoto mwenye shida ya moyo ni kama kukua kwa shida, kupumua kwa shida na kutoka jasho jingi na katika kliniki yetu hapa tunapata watoto 10 kila siku wenye shida ya moyo,” alisema
Alisema watoto wanaohitaji matibabu ya moyo ya upasuaji wa kufungua kifua au kupitia mishipa ni 500 kila mwaka na kwamba idadi imekuwa ikiongezeka kila mwaka na gharama zake ni kubwa kutokana na vifaa na dawa zinazotumika.
Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro, alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara kwani walipoambiwa wachangie matibabu ya watoto wenye changamoto ya moyo walitoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha wanatoa mchango wao.
“Kwa taarifa iliyotolewa na daktari bingwa haoa inaonyesha tatizo bado ni kubwa na safari bado ni ndefu sana kwa hiyo tunaomba tutakapokuja tena mtuunge mkono kwasababu huduma hizi za upasuaji ni endelevu na tunatamani kumaliza wote wenye changamoto ya moyo,” alisema
Mwakilishi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Evarlasting Lyaro, alisema huo ni mwanzo tu wa ushirikiano na JKCI na kwamba wataandaa MoU kwaajili ya kushirikiana kupima afya za wafanyakazi.

