Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi haijatekeleza agizo la Ofisi ya Waziri Mkuu,
kuwachukulia hatua watendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa uzembe na kukaidi agizo
la kushughulikia uporwaji ardhi na nyumba ya mkazi wa kijiji cha Nyihogo wilayani humo, Vicent
Shilla.
Agizo hilo la Desemba 31, 2015, linatokana na kashfa ya uporwaji ardhi na nyumba, mali ya
Shilla, vinavyodaiwa kumilikishwa kwa njia zisizo halali kwa Hawa Kanyalengwe, anayeshukiwa
kuwa ni raia wa Rwanda.
Hata hivyo, Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kahama, Charles Balele, ameliambia JAMHURI kuwa
madai dhidi ya uraia wa Kanyalengwe yalifanyiwa kazi kupitia uchunguzi uliohusisha Idara ya
Uhamiaji katika Wilaya ya Kahama na kubaini kuwa ni raia wa Tanzania.
Katika shauri la madai ya kuporwa ardhi na nyumba, Shilla amesema vilifanyika kwa kiwanja
chake namba 626, kitalu ‘A’ (HD) kikiwa na ukubwa wa mita 30 kwa 34.
Anasema wakati kiwanja hicho kikimilikishwa kwa Kanyalengwe, (Shilla) alikuwa jijini Dar es
Salaam.
Amesema tukio hilo lilitokea mwaka 2011 na kwamba miongoni mwa walioshiriki kufanikisha
‘dhuluma’ hiyo ni Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kahama, Charles Balele, na Ofisa Mtendaji wa kijiji
hicho, Simon Mabumba.
Shilla amesema ardhi hiyo ni sehemu ya eneo alilorithi kutoka kwa baba yao mzazi, Charles
Makulu, aliyefariki mwaka 2002, likiwa na ukubwa wa ekari tano na kugawanywa kwa watoto 10
akiwamo yeye.
Amesema awali, aliripoti kuporwa ardhi na nyumba hiyo katika kituo cha polisi Kahama Mjini na
kufunguliwa jalada namba KAH/RB/6886/2011.
Kwa mujibu wa Shilla, hatua hiyo ilisababisha kukamatwa kwa Kanyalengwe, na kufikishwa
katika kituo hicho ingawa aliachiwa muda mfupi baadaye.
Pia amedai aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kahama (OC-CID), Aziz Mayunga,
alimshauri akubaliane na ‘mporaji’ wa eneo lake ili alipwe shilingi milioni 3 kumaliza suala hilo,
hatua aliyohisi kuzingirwa na ‘harufu ya rushwa’.
Amesema wakati mgogoro huo ukiendelea, aliombwa na Balele ampatie barua ya toleo ili
ashughulikie hatimiliki ya ardhi yake, lakini hakuirudisha wala hakupata hati husika, badala yake
alishawishiwa kukubaliana na ‘mvamizi’ wa kiwanja chake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyihogo, Willbert Mwakabana, amelieleza JAMHURI kuwa eneo husika
linatambulika kuwa mali ya Shilla na kwamba alitoa ushahidi katika Baraza la Ardhi la kata hiyo,
lakini alipuuzwa na uamuzi kumpendelea mtu anayelalamikiwa.
“Ni eneo la Shilla na nyumba ilikuwa mali yake na suala hilo lilifikishwa kwenye kata, isipokuwa
kilichokuwa kimetawala ni mazingira ya rushwa na kugawa viwanja kiholela,” amesema.
Amesema “huu ni unyanyasaji, mwenye pesa anauziwa haki ya mtu mwingine na uporaji wa
kiwanja hiki ndivyo ulivyokuwa.”
Naye Mabumba anayetuhumiwa kufanikisha uporwaji unaodaiwa kufanywa kwa eneo hilo,
amesema suala hilo lilishughulikiwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la kata na wilaya
ambako Shilla alishindwa, hivyo hahusiki katika kashfa hiyo.
“Mkono wangu haukuhusika na uuzaji wa eneo la Shilla, na sisi tulipoitwa kama mashahidi na
ndugu zake walieleza kuwa wao ndiyo waliouza,” amesema huku akishindwa kuwataja anaodai
kuwa walihusika kuuza.
Shilla amesema aliwasilisha malalamiko yake katika ngazi tofauti za juu serikalini ikiwamo
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi lakini bado haki yake haijapatikana.
Juni 6, 2013, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilimwandikia barua
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, ikimtaka kusitisha uendelezaji wa
eneo hilo hadi mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi lakini akakaidi.
“Kabla ya upangaji, upimaji na hatimaye umilikishaji, mlipaswa kuzingatia maslahi ya
mwananchi aliyekuwa anamiliki eneo hilo kiasili au kimila,” imeeleza sehemu ya barua hiyo
yenye kumbukumbu namba LD/289839/91.
Desemba 31, 2015, Ofisi ya Waziri Mkuu ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, yenye kumbukumbu namba 2/FC.405/590/01, ikimtaka
achukue hatua dhidi ya watendaji waliohusika kwa makusudi kusababisha kero kwa mwananchi
huyo.
Barua hiyo imeeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imepokea malalamiko ya muda mrefu kutoka
kwa Shilla, kuhusu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama kumdhulumu ardhi yake
pamoja na kuvunjiwa nyumba aliyokuwa ameijenga katika eneo hilo.
“Kwa nyakati tofauti umewahi kumwandikia Mkurugenzi husika kuhusu kurekebisha kasoro hiyo
kwa kutenda haki kwa mlalamikaji kupitia barua zenye kumbukumbu namba LD/289839/47 ya
Machi 29, 2012, LD/289839/67 ya Januari 9, 2013,” inasomeka sehemu ya barua hiyo na
kuongeza;
Barua nyingine inatajwa kuwa ni LD/289839/91 ya Juni 6, 2013 na LD/289839/20 ya Machi 18,
2014, hata hivyo, inaonekana mhusika amekaidi kutekeleza maagizo ya wizara.
“Kwa kuzingatia hali hiyo, tunashauri wizara yako sasa ichukue hatua dhidi ya watendaji husika
kwa kukaidi maagizo hayo halali kutokana na kufanya uzembe wa makusudi na kusababisha
kero kwa mwananchi huyo,” imeagiza barua hiyo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwishoni mwa wiki, JAMHURI iliwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika, ambaye amesema suala hilo linahitaji kupata
maelezo kutoka kwa watu mbalimbali kabla ya kujibu.
“Suala lenyewe linahitaji maelezo kutoka kwa watu mbalimbali,” amesema Mwanyika, ambaye
hakutaka kuingia kwa undani licha ya muda mrefu tangu kutolewa kwa agizo hilo, badala yake
akataka aandikiwe maswali.