Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mtwara
Ikiwa ni Wiki ya Sheria nchini, Wizara ya Katiba na Sheria imetoa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na utawala Bora kwa viongozi na Watendaji wa Kata kwenye Halmashauri ya Mtwara vijijini na Mikindani.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo mkoani Mtwara,Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara ya katiba na sheria Abdulrahiman Msham amesema mafunzo hayo yanatolewa ili wananchi wawe na uelewa na masuala ya uraia.
“Tunatoa elimu hii ili kama Serikali ikiamua kufanya mabadiliko ya Katiba wananchi wawe na uelewa wa Katiba iliyopo na mapendekezo yao, tunataka wananchi wawe na uelewa wa Sheria mama ambayo ni Katiba Ikiwa ni pamoja na mapungufu yake kama yapo , ” ameeleza
Amesema kuna watu huenda na mlengo wa ujumla bila kuielewa Katiba hivyo kupitia mafunzo hayo, viongozi watapata uelewa na kwenda kutoa elimu kwa ya uraia na utawala bora kwa makundi mbalimbali.
Nao baadhi ya Watendaji walioshiriki mafunzo hayo wameeleza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa wa masula ya kikatiba juu ya masuala ya uraia na utawala bora ili kuwa na jamii yenye usawa na uwajibikaji.
Mtendaji wa kata Msanga Mkuu Berinda Mhina amesema, “Tutahakikisha wananchi wetu wanaelewa kwa undani masuala yote ya kikatiba ili kuwarahisishia kuielewa endapo mchakato wa Katiba utakuwa unafanyika , ” amesema
Naye Method Damiani Mtendaji wa kata Mtwara Vijijini amesema kupitia mafunzo hayo Wizara ya Katiba na Sheria itarajie matokeo chanya kwa kuwa wao kama viongozi wa jamii watawajibika kutoa elimu kwa makundi yote.