Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali kupitia Wizara yake imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa habari na kueneza taarifa sahihi kwa wananchi kupitia mikakati mbalimbali iliyotekelezwa ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 14 Jijini Dodoma, Prof. Kabudi amesema katika kipindi hicho, Serikali imefanikiwa kufanikisha jumla ya mikutano 43 kupitia Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, kuandaa vipindi maalum 20 vya televisheni vilivyolenga kuonyesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na makala maalum ya kuonyesha mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.
“Wizara kupitia Idara ya Habari – MAELEZO imeboresha miundombinu kwa kununua vifaa vya kurushia matangazo mbashara, magari ya kisasa na vifaa vya kurahisisha uzalishaji wa maudhui ya habari,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema Wizara hiyo imeendelea kuratibu waandishi wa habari hasa katika kipindi cha majanga kama vile maporomoko ya tope Hanang na ajali ya ghorofa Kariakoo.
Pia imefanikisha uratibu wa waandishi katika ziara za kitaifa na kimataifa, na kushiriki katika kuandaa mikakati ya mawasiliano kwa taasisi mbalimbali ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika kuendeleza sekta ya habari, Prof. Kabudi ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuratibu vikao kazi vinne vya Maafisa Habari na Uhusiano vilivyowezesha maafisa 400 kushiriki kila mwaka, kuandaa makongamano mawili makubwa ya sekta hiyo na kushirikiana na mashirika ya kitaifa na kimataifa kama UNESCO, TEF, TAMWA na MISA-Tan.
Pamoja na hayo amesema Serikali ilianzisha kampeni ya Tumekusikia Tumekufikia ambayo ilifikia mikoa 16, ikilenga kusambaza taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi za halmashauri na mikoa.
Waziri huyo amesisitiza pia kuwa kupitia Wizara yake, Serikali imeratibu mikutano ya Mawaziri na Taasisi 105 kuelezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, huku uhuru wa vyombo vya habari ukiongezeka na Tanzania kupanda kutoka nafasi ya 143 hadi ya 97 duniani kwa mwaka 2024.
“Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 yameondoa makosa ya kijinai kwa waandishi wa habari na wamiliki wa mitambo ya uchapishaji. Pia, tumefanikisha kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kwa mara ya kwanza Machi 3, 2025 – hatua ya kihistoria kwa sekta hii,” aliongeza.
Katika kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa kwa usawa, Serikali imeongeza usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na kupanua miundombinu ya utangazaji kwa wilaya 12 nchini kwa kununua mitambo ya kurushia matangazo ya redio.
Prof. Kabudi amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendeleza sekta ya habari kwa njia shirikishi, huru na yenye kuwajibika kwa maendeleo ya Taifa.