Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MRATIBU wa Mabadiliko ya Tabia katika jamii kutoka Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Grace Msemwa ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao la Wizara ya Afya lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ili kuweza kupata elimu, kupima afya pamoja na kupata chanjo.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho hayo yanayoendelea jijini Dodoma.

Amesema katika maonesho hayo Wizara ya Afya inatoa elimu na huduma mbalimbali ikiwemo upimaji wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti, uzazi wa mpango pamoja na huduma za chanjo ya homa ya ini, Covid 19 na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti.

“Huduma hizi zinatolewa bure kabisa, kwahiyo wananchi changamkieni fursa hii, kwasababu nje ya hapa kuna Huduma ni lazima zilipiwe. Kwa mfano chanjo ya Homa ya Ini ukienda Hospitali inatolewa kwa Sh. 30,000 lakini hapa inapatikana bure.

“Pia tuna wataalam wa saikolojia na afya ya akili na tunafanya uchunguzi na kutoa elimu kuhusu afya ya akili, huduma zote hizi zinatolewa bure kwahiyo tunawakaribisha wananchi wafike kwa wingi tuwahudumie,” amesema Msemwa.

Aidha amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo zaidi ya watu 1,000 wamepatiwa elimu ya masuala mbalimbali ya afya, kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa na kupatiwa chanjo.

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la wizara hiyo wameipongeza Wizara ya Afya kwa kutoa huduma hizo kwa kuwa zitawawezesha kutambua hali zao za kiafya.