Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wizara ya Afya nchini Somalia imeichagua Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kushirikiana kwenye masuala mbalimbali yanayohusu mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwa kubadilishana uzoefu katika maeneo ya mifumo, ununuzi, usambazaji na udhibiti ubora.

Hayo yamebainishwa na watendaji wa Wizara ya Afya kutoka nchini Somalia waliotembelea Bohari ya Dawa (MSD), ambapo mwakilishi wa ugeni huo Mohamed Abdulukadiri Hersi ameeleza kuwa hatua mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa katika mifumo inayotumika katika mnyororo mzima wa ugavi inayotumia tekinolojia ndio umewavutia zaidi kuja kujifunza kwa kujionea namna inavyofanya kazi na kuoana na mifumo mingine ya serikali.

Hersi ameongeza kuwa, Somalia ipo kwenye mpango wa kujenga upya mfumo wake wa ugavi wa bidhaa za afya, ikiwa ni pamoja na kuboresha utaratibu wa kufikisha bidhaa za afya kwa wananchi, hivyo kati ya nchi walizozichagua kuwa mfano ni Tanzania, ambapo kupitia MSD amesema wamemejifunza mengi ambayo watakwenda kuyatekeleza watakaporudi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, ameeleza kuwa wageni hawa wamekuja Tanzania kwa muda muafaka ambapo MSD imefanya mageuzi makubwa ya kiutendaji ikiwemo kujiendesha kibiashara, na kufanya maboresho mbalimbali katika mnyororo mzima wa ugavi wa bidhaa za afya, hivyo watajifunza mengi.