Mhandisi wa Maji, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Wawa Nyonyoli, ametangaza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa mji huo watapata maji safi na salama ifikapo Juni, mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa JAMHURI mjini hapa, Mhandisi Nyonyoli anasema kwamba mradi huo unaratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Anasema kwamba mradi huo upo katika Kijiji cha Nyamazugo, Sengerema mjini, ambako unagharimu dola milioni 14 za Marekani, jambo ambalo linamsukuma Mbunge wa jimbo hilo, William Ngeleja (CCM), kuipongeza Wizara ya Maji.
“Mpaka Juni, maji yatapatikana kwa zaidi ya asilimia 50 ya wakazi hawa, halafu mradi huu ukikamilika hapo Januari, mwakani asilimia 100 itakuwa inapata maji safi na salama,” anasema Nyonyoli, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa miradi ya maji wilayani humo.
Kwa upande wake, Ngeleja, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri na waziri kamili wa Nishati na Madini kwa kipindi cha takriban miaka mitano na nusu, ameichagiza Serikali kutimiza wajibu wake kwa kutoa fedha zote za miradi ya maji kama zilivyotengwa na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ngeleja alitolea mfano kwa kutaja miradi mbalimbali ya maji katika jimbo lake la Sengerema, ambayo imetengewa fedha na inayoendelea kutekelezwa kupitia bajeti za miaka ya 2013/14 na 2014/15.
Hata hivyo, mbunge huyo akafafanua kuwa kuna sehemu ya fedha hazijatoka kwa ukamilifu ambazo ni Nyasigu-Lubungo-Ngoma ‘A’ (Sh. bilioni 1.686), Kasomeko-Chamabanda (Sh. milioni 499.2), Chamabanda-Nyantakubwa (Sh. milioni 713.2) na Nyantakubwa-Kasungamile (Sh. milioni 250.5).
Nyingine ni Katunguru-Nyamtelela (Sh milioni 794.7), Nyamtelela-Nyamililo (Sh. milioni 30), Buyagu-Kalangalala-Bitoto (Sh. bilioni 1.3), Busisi/Kahumulo-Nyampande (Sh. milioni 408), Chifunfu (Sh. milioni 400), Kamanga-Nyamatongo (Sh. milioni 405), na Nyamazugo-Sengerema mjini (dola 14 milioni au Sh. bilioni 23). Kwa pamoja miradi hii itagharimu zaidi ya Sh. bilioni 29 za Tanzania.
“Kinachofurahisha zaidi ni kwamba miradi yote hii niliyoitaja hapa chanzo chake ni Ziwa Victoria, achilia mbali miradi mingine ya visima vifupi, vya kati na virefu inayoendelea kutekelezwa katika vijiji mbalimbali jimboni hapa kupitia bajeti ya Serikali na Mfuko wa Jimbo,” anasema Ngeleja.
Akifafanua zaidi Ngeleja anasema kwamba utekelezwaji wa miradi hiyo ya maji kutoka Ziwa Victoria ni jibu na ushahidi tosha kwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi waishio kando kando mwa Ziwa Victoria, ambao wamekuwa wakihangaishwa na kero ya maji wakati wanaishi karibu na chanzo cha maji cha uhakika.