Serikali inatambua umuhimu wa Sekta binafsi katika mchango wake kwenye Sekta ya Madini na inapongeza juhudi za sekta hiyo katika kuwekeza kwenye Sekta ya Madini ili kuongeza mchango katika Pato la Taifa.

Lengo la kukutana ilikuwa ni kuifanya Sekta ya Madini nchini iwe ya kuvutia katika uwekezaji na kuzinufaisha pande zote mbili, Serikali pamoja na wadau wote.

Alisema Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali katika hafla fupi Juni 2, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na wawekezaji pamoja na wachimbaji wakubwa katika Sekta ya Madini ili kufahamiana na kuwa na ukaribu kama Jumuiya moja yenye lengo la kuwezesha na kuimarisha Sekta ya Madini.

Aidha, amesisitiza kuwa, Wizara ya Madini na Serikali kwa ujumla inazifanyia kazi changamoto zote zinazowasilishwa na wadau na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikisha taasisi nyingine zinazohusika katika usimamizi wa Sekta ya Madini.

Hafla hiyo ilihusisha taasisi nyingine za Serikali ili kuonesha nia ya dhati ya Serikali ya kuweza kufanya kazi kwa pamoja na kwa ukaribu zaidi.

“Ninawahakikishia kwamba, Serikali inawasikiliza na kuweka fursa nyingine kwenye Sekta yetu ili wachimbaji wa madini pamoja na wawekezaji wafanye shughuli zao kwa manufaa zaidi,” alisisitiza Mahimbali.

Kwa upande wa Sekta binafsi kwa pamoja wameeleza furaha waliyonayo kuona Wizara ya Madini pamoja na Serikali kwa ujumla ya kuona umuhimu wa wawekezaji katika Sekta ya Madini kwa kuwaweka karibu kama familia kwa ajili ya ustawi wa sekta.

Kauli hizo zilitolewa na wawakilishi kutoka kwa Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Benedict Busunzu na Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Philibert Rweyemamu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wawekezaji na wachimbaji wakubwa na wa kati wa madini mbalimbali ikiwemo ya mkakati yanayopewa kipaumbele kwa sasa duniani.